Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Hassan Selemani Kaunje

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Lindi Mjini

Primary Question

MHE. HASSAN S. KAUNJE aliuliza:- Ilani ya Chama cha Mapinduzi 2015 - 2020, imeeleza juu ya uendelezaji wa utalii kwa Ukanda wa Kusini kama Program Maalum:- Je, ni lini Serikali imepanga kuanza mpango huo maalum?

Supplementary Question 1

MHE. HASSAN S. KAUNJE: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwanza kwa majibu ya ziada ya Mheshimiwa Naibu Waziri. Swali langu la msingi ilikuwa ni lini, kwa maana ni mwaka gani katika miaka hii mitano au bajeti ipi hizi program za Maendeleo ya Sekta ya Utalii Kusini zitaanza?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili, kwa maana ya vivutio alivyovitaja, sambamba na vivutio vingine vya fukwe za Kisuele na Mitema ambazo ni bora kuliko zote katika ukanda wa Pwani ya Afrika Mashariki, kuanzia Somalia mpaka South Africa: Je, yuko tayari kuviwekea vipaumbele katika kuvitangaza kupitia taasisi zake zinazotangaza utalii wa nchi hii?

Name

Eng. Ramo Matala Makani

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tunduru Kaskazini

Answer

NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nampongeza Mheshimiwa Kaunje, kwa namna ambavyo ameanza kwa kasi kubwa kuweza kutetea eneo la Kusini ili utalii sasa uweze kuelekea upande wa ukanda huo, kwa maana ya Southern Circuit badala ya hali ambayo iko hivi sasa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu suala la lini; nimezungumzia Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano kwenye jibu langu la msingi, lakini pia nimetaja mradi wa Regrow ambao nilisema na wenyewe ni mradi ambao unakwenda kuboresha utalii katika ukanda wa kusini. Sasa kuhusu lini, nataka kusema, kuhusu mradi wa Regrow tayari mradi huo umeshaanza na uko katika hatua za awali na miradi mingine ambayo itakuwa inaunga mkono jitihada za utalii kusini itaweza kupangwa katika bajeti zijazo, wakati kwa sasa hivi tunatekeleza mradi huu wa Regrow ambao wenyewe tunautekeleza kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu fukwe za Mitema na nyinginezo kuweza kupewa kipaumbele, kama nilivyojibu kwenye swali la msingi, kwamba Mikoa ya Lindi na Mtwara ina utajiri mkubwa sana wa fukwe za bahari, tofauti na maeneo mengine ambako kuna fukwe za Maziwa; Lindi na Mtwara kuna utajiri mkubwa sana wa fukwe za bahari.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, katika Mpango wa Maendeleo wa Miaka mitano, ambao unaanza na mpango huu wa mwaka wa kwanza wa 2016/2017, hatua ya kwanza tunayokwenda kuifanya ni kutembelea maeneo hayo yote na kuweka matangazo ya kutosha ili kuweza kuwavutia wawekezaji mbalimbali kuweza kuboresha miundombinu katika maeneo hayo ili fukwe hizo ziweze sasa kushiriki katika Sekta ya Utalii kwa tija zaidi.