Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Question

Term Session Sitting Sector Ministry Qn No Date
2020-2025 Session 11 Sitting 6 Finance and Planning Wizara ya Fedha na Mipango 77 2023-04-13

Name

Boniphace Mwita Getere

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bunda

Primary Question

MHE. BONIPHACE M. GETERE aliuliza: -

Je, kuna mkakati gani wa kupata mkopo wa fedha wa muda mrefu kwa masharti nafuu ili kulipa madeni sumbufu ya awamu zote sita?

Name

Hamad Hassan Chande

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kojani

Answer

NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Boniphace Mwita Getere, Mbunge wa Bunda kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kusimamia deni la Serikali kupitia Sheria ya Mikopo, Dhamana na Misaada, Sura 134 iliyobainisha vigezo vya kuzingatia wakati wa kutafuta fedha za mikopo kutoka ndani na nje ya nchi ili kugharamia shughuli za Serikali, hususan miradi ya maendeleo. Sheria hiyo pia inatumika kama nyenzo ya kudhibiti ongezeko la deni la Serikali kwa kulipa mikopo iliyoiva na kutoa kipaumbele kwa mikopo yenye masharti nafuu.

Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha awamu zote sita Serikali imeendelea kukopa na kulipa mikopo kulingana na mtiririko wa malipo kwa kila mkopo na hakuna mikopo ambayo Serikali imeshindwa kulipa. Aidha, malipo ya madeni yote ikiwemo madeni sumbufu yanaendelea kulipwa kupitia mpango na bajeti za Serikali za kila mwaka, ahsante.