Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Question

Term Session Sitting Sector Ministry Qn No Date
2020-2025 Session 11 Sitting 24 Lands, Housing and Human Settlement Development Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi 313 2023-05-12

Name

Joseph George Kakunda

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Sikonge

Primary Question

MHE. JOSEPH G. KAKUNDA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itaweka alama za mipaka kutenganisha maeneo ya hifadhi na vijiji 975 vilivyotolewa kwenye Hifadhi?

Name

Geophrey Mizengo Pinda

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kavuu

Answer

NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Joseph George Kakunda, Mbunge wa Sikonge kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kazi ya kuweka alama za mipaka kutenganisha maeneo ya Hifadhi na Vijiji 975 vilivyotolewa kwenye hifadhi imefanyika katika baadhi ya hifadhi na bado kazi hiyo inaendelea. Hifadhi zilizowekewa alama za mipaka mpaka sasa ni pamoja na eneo la kilomita za mraba 1,500 za Hifadhi ya Pori Tengefu Loliondo vigingi 422 vya alama vilishawekwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, Hifadhi ya Pori la Akiba la Wamimbiki alama 277 na kilomita 156 za mkuza zimetengenezwa. Hifadhi ya Pori la Akiba Swagaswaga alama 226 kati ya 250 na kilomita 27 za mkuza zimetengezwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, Hifadhi ya Pori la Akiba Mkungunero alama 99 kati ya 157 na kilomita 35.8 za mkuza zimetengenezwa. Hifadhi ya Taifa ya Ruaha alama 650 na kilomita 177 za mkuza zimeishatengenezwa pamoja na Bonde la Usangu, alama 632 zimewekwa kwenye eneo lenye urefu wa kilomita 316 kati ya 350 na mkuza wenye kilomita za mraba 177 umechongwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mkoani Tabora, alama za mipaka zimeshawekwa kwenye vijiji vitano vya Mwendakumila, Mwaharaja, Chemkeni, Uhindi na Nsimbo vya Wilaya ya Kaliua vilivyokua kwenye hifadhi ya Ulyankulu.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatoa maelekezo kwa Wakuu wa Mikoa kwa kushirikiana na Taasisi zinazohusika na usimamizi wa hifadhi, kuendelea na utekelezaji wa uamuzi wa Baraza la Mawaziri ikiwemo kazi ya kuweka mipaka kwa kutumia alama za kudumu zinazoonekana ili kuimarisha ulinzi katika maeneo hayo, ahsante.