Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Term | Session | Sitting | Sector | Ministry | Qn No | Date |
---|---|---|---|---|---|---|
2015-2020 | Session 4 | Sitting 2 | Natural Resources and Tourism | Wizara ya Maliasili na Utalii | 26 | 2016-09-07 |
Name
Dr. Shukuru Jumanne Kawambwa
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bagamoyo
Primary Question
MHE. DKT. SHUKURU J. KAWAMBWA aliuliza:-
Kumekuwa na mgogoro wa muda mrefu wa mipaka kati ya TANAPA na vijiji na vitongoji jirani vinavyowazunguka.Je, Serikali ina mpango gani wa kumaliza mgogoro huu kati ya TANAPA na vitongoji vya Kitame, Razaba, Gama-Makani katika Kata ya Makurunge?
Name
Eng. Ramo Matala Makani
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Tunduru Kaskazini
Answer
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Shukuru Kawambwa, Mbunge wa Bagamoyo kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, migogoro yote mitatu iliyotajwa na Mheshimiwa Mbunge inahusiana na hifadhi ya Taifa Saadani iliyoanzishwa kisheria kwa Tangazo la Serikali Namba 281 la mwaka 2005.
Mheshimiwa Mwenyekiti, migogoro baina ya Kitongoji cha Kitame, Kijiji cha Makurunge na hifadhi umetokana na malalamiko kwamba wananchi hawakushirikishwa katika zoezi la uwekaji wa mipaka hivyo kusababisha yaliyokuwa maeneo yao kuingizwa ndani ya hifadhi bila ridhaa yao. Hata hivyo, kumbukumbu zinaonyesha kwamba kuwa wananchi walishikikishwa kikamilifu kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu ikiwa ni pamoja na kufanyika kwa mkutano wa kijiji mama cha Makurunge ambacho kitongoji hiki ni sehemu yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mgogoro baina ya shamba la Razaba na hifadhi umetokana na utata wa takribani eneo la hekta 3,441 alilopewa mwekezaji Bagamoyo Eco-Energy kwa hati miliki namba 123097 ya terehe 9 Mei, 2013 ili amiliki na kuendesha shughuli za kilimo cha miwa katika eneno ambalo kiuhalisia limo ndani ya hifadhi ya Taifa ya Saadani. Juhudi za kutatua mgogoro huu ziliendelea kufanyika kwa takribani miaka minne kwa kuhusisha ngazi za Vijiji, Wilaya, Mkoa na Wizara zinazohusika na hatimaye kutolewa maelekezo kupitia agizo la Mheshimiwa Waziri Mkuu agizo ambalo lilizingatia athari za mazingira zilizotishia uwepo wa hifadhi ya Saadani iwapo kilimo cha miwa kingeruhusiwa katika eneo linalozungumziwa.
Mgogoro baina ya Gama -Makani na hifadhi unatokana na malalamiko ya wananchi kuwa baadhi ya waliofidiwa wakati wa uanzishwaji wa hifadhi katika eneo hilo hawakuwa wamiliki wazawa wa maeneo hayo. Hata hivyo taarifa zinaonyesha kuwa mchakato wa malipo ya fidia ulifuata taratibu muhimu ikiwemo ushirikishwaji wa karibu wa uongozi wa Wilaya ya Bagamoyo, Serikali za Kata na Serikali za Vijiji husika ambao ulizingatia ilivyohitaji la kuwalipa wananchi waliostahili na si vinginevyo. Pamoja na maelezo haya, Serikali imekwishaunda timu ya pamoja ya wataalam ambayo inaendelea na kazi ya kutafuta suluhisho la migogoro ya ardhi nchini ikishirikisha Wizara mbalimbali kama ilivyoahidiwa wakati wa Bunge la Bajeti lililoahirishwa mwezi Juni, 2016.
Copyright © Bunge Polis 2024. All Rights Reserved