Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Ritta Enespher Kabati

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. DKT. RITTA E. KABATI aliuliza: - Je, Serikali inawasaidiaje wakulima wa parachichi Iringa ili waweze kulima kilimo chenye tija?

Supplementary Question 1

MHE. DKT. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Waziri kwa majibu yake mazuri na naomba niulize maswali mawili madogo ya nyongeza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa tarehe 8 Agosti huwa ni siku ya wakulima nchini, na siku hiyo wakulima wengi hupata fursa ya kukutana kuonesha maonesho na kujifunza, na kwa kuwa Serikali imesimamisha haya maonesho karibu mwaka mmoja na nusu sasa.

Je, nini kauli ya Serikali kuhusiana na kusimamishwa Maonesho haya ya Nanenane nchini? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili; kwa kuwa kumekuwa na vikwazo vingi sana barabarani kwa magari yanayosafirisha bidhaa hizi za mazao yanayoharibika kama nyanya, parachichi na kadhalika na kusababisha hasara kubwa sana kwa wakulima.

Je, Serikali ina mpango gani sasa wa kutoa vibali maalum kwa ajili ya magari yanayosafirisha mazao haya kwa saa 24, kwa sababu kuna magari makubwa ambayo yanazuiwa, saa 12 yanaambiwa yasisafirishe mazao kupeleka hata nje ya nchi kama South Africa? (Makofi)

Name

Hussein Mohamed Bashe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nzega Mjini

Answer

WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Ritta Enespher Kabati, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, zao la parachichi na mfumo mzima wa parachichi katika nchi yetu haukuwa na mwongozo. Kwa hiyo Serikali sasa hivi iko kwenye hatua za mwisho na tutazindua mwongozo wa kusimamia zao la parachichi kuanzia shambani mpaka sokoni na utaratibu wote.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kupitia Bunge lako tukufu wakati tunafanya mawasiliano ndani ya Serikali kati ya Wizara ya Kilimo, TRA na watu wa TANROADS kwa maana ya Wizara ya Miundombinu ili ku-develop stika maalum ambazo zitasimamia mazao ya horticulture, magari yote yanayobeba mazao ya horticulture yatakuwa na stika maalum. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninataka nipitie Bunge lako tukufu kuziomba Mamlaka za Serikali za Mitaa kwamba mazao ya parachichi na mazao ya mbogamboga ni perishable, ni vizuri kutokuweka vikwazo visivyokuwa na ulazima barabarani kwa kipindi hiki ambacho tunaandaa mwongozo ambao utasimamiwa ndani ya Serikali katika ngazi zote.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo huu utaratibu wa kuwazuia kusafiri usiku nadhani siyo sahihi na ninapenda kupitia Bunge lako tukufu kuwaomba viongozi wa mikoa wa-facilitate transportation ya mazao ya kilimo hata kama ni usiku namna gani. Kama mtu anasafiri aendelee na kusafirisha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimalizie kipengele cha pili kuhusu Nanenane; ni kweli Serikali ilisimamisha Nanenane kwa muda, na ninataka kupitia Bunge lako tukufu kuwatangazia Watanzania na wakulima kwamba Nanenane tunarudisha na mwaka huu Kitaifa itafanyika Mkoa wa Mbeya. Serikali iko kwenye kufanya total reform ya mfumo wa Nanenane. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, na ningepitia Bunge lako tukufu kuzitaka Mamlaka za Serikali za Mitaa; shughuli za Nanenane zitasimamiwa na Wizara ya Kilimo na sekretarieti za mikoa. Taasisi iliyokuwa inaitwa TASO ambayo ilikuwa imejimilikisha kusimamia Nanenane haitahusika na wala haihusiki na masuala ya Nanenane na viwanja vya Nanenane. Suala hili litasimamiwa na Serikali, Wizara ya Kilimo na Mamlaka za Mikoa kwa maana ya mikoa husika.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali sasa hivi tuko kwenye hatua za mwisho za kuandaa mfumo mpya wa shughuli za Nanenane, na Tanzania tutakuwa na kitu tunaitwa Tanzania International Agricultural Trade Show ambapo tutakuwa na eneo moja ambalo nchi nzima kila mwaka kimataifa litakuwa linafanyika hapo na mikoa itakuwa inafanya shughuli za kikanda. (Makofi)

Name

Deodatus Philip Mwanyika

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Njombe Mjini

Primary Question

MHE. DKT. RITTA E. KABATI aliuliza: - Je, Serikali inawasaidiaje wakulima wa parachichi Iringa ili waweze kulima kilimo chenye tija?

Supplementary Question 2

MHE. DEODATUS P. MWANYIKA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi kuuliza swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, siku za karibuni kumekuwa na taarifa ambazo zimekuwa zikitapakaa kwenye mitandao pamoja na picha zikionesha kwamba parachichi ya Tanzania haikidhi viwango, jambo ambalo siyo kweli. Nini kauli ya Serikali kuhusiana na suala hili? (Makofi)

Name

Hussein Mohamed Bashe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nzega Mjini

Answer

WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, nataka niwahakikishie Watanzania na niwahakikishie wateja wote wanaonunua parachichi za Tanzania kuwa parachichi za Tanzania zinakidhi vigezo vya kimataifa na ndiyo maana tumekuwa sasa hivi tukifungua masoko mapya na hivi karibuni tumefungua soko la India, na ni Tanzania pekee ambayo imepata import duty exemption ya parachichi yake katika soko la India, hili ni jambo la kwanza.

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili; tunazo international certification institutions ndani ya nchi yetu. Kwa hiyo, parachichi yetu inapotoka nje ya mipaka inakuwa na certifications za kimataifa zote ambazo zinakubalika katika soko la dunia. Kumekuwa na tatizo la competitors wetu na mimi nataka niwaombe exporters wa Tanzania wahakikishe wanapo-export parachichi ya Tanzania inaondoka na trademark iliyoandika Produce of Tanzania ili kuweza kui-protect image ya parachichi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ushindani upo, watu watataka ku-distort image yetu. Niwaombe Watanzania, yeyote anayepata taarifa yenye mashaka kuhusu product ya Tanzania awasiliane na Wizara ya Kilimo na sisi tutakuwa tayari kui-protect bidhaa yetu popote pale.