Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Godwin Emmanuel Kunambi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mlimba

Primary Question

MHE. GODWIN E. KUNAMBI aliuliza: - Je, ni lini Serikali itatatua mgogoro kati ya wananchi na TAWA katika Bonde la Mto Kilombero?

Supplementary Question 1

MHE. GODWIN E. KUNAMBI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kwa kunipa fursa ya kuuliza maswali madogo mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Jamhuri kwa niaba ya Mamlaka ya Uhifadhi kwa maana ya TAWA iliwashitaki Wenyeviti wawili wa vitongoji ndani ya Kijiji cha Mkangawalo, kesi ya jinai namba 281 kwa kosa la kufanya shughuli za kilimo kwenye hifadhi, na tarehe 27 Septemba, 2021 Mahakama iliwaacha huru watu hawa na kuagiza warudishiwe ardhi yao na mali zao kwa maana ya trekta walizonyang’anywa.

Je, ni lini Serikali sasa itarejesha mali zao? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, wananchi wa Jimbo la Mlimba ni wakulima, wafugaji na wavuvi. Mamlaka hii ya Uhifadhi kwa maana ya TAWA imekuwa ikiwasumbua mara kwa mara. Je, Waziri ni lini sasa atakuwa tayari kuambatana nami kwenda Jimboni pale Mlimba kwenda kushuhudia kero hizi na kuzitatua? Ahsante.

Name

Mary Francis Masanja

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Godwin Kunambi, Mbunge wa Jimbo la Mlimba kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala hili ambalo lilikuwa mahakamani na Mheshimiwa Mbunge ametuthibitishia hapa kwamba watuhumiwa hawa wameshaachiwa huru na mali zao zilishikiriwa na TAWA, nitoe tu ufafanuzi katika eneo hili, kwamba mtuhumiwa anapokamatwa ushahidi na vitu vyote vinapelekwa mahakamani. Na pale ambapo inathibitika kwamba mtuhumiwa ameshinda kesi, basi mtuhumiwa anarejeshewa mali zake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kama mali hizi ziko upande wa TAWA, nimuhakikishie tu Mbunge kwamba tutaenda kulishughulikia suala hili ili mali hizi zirejeshwe kwa watuhumiwa. Lakini ninavyofahamu tunapopeleka kesi hizi mahakamani, tunapeleka na vithibitisho vyote na vinakuwa chini ya Mahakama. Kwa hiyo, kama iko kwetu basi nimuhakikishie kwamba vitarejeshwa kwa wakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na suala hili la pili kwamba niko tayari kwenda kutoa ufafanuzi. Nimhakikishe tu Mheshimiwa Kunambi kwamba wananchi wa Mlimba watambue kwamba Serikali iko kazini na kama nilivyosema, Timu ya Kitaifa ambayo imeteuliwa na Baraza la Mawaziri iko uwandani, inafanya tathmini bila kufanya taharuki yoyote na inashikirisha mkoa, inashirikisha wilaya na wale wananchi tukimaanisha viongozi walioko kwenye maeneo hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukishatambua Serikali inapaswa kurejesha kama wale ambao tunatakiwa kuwaondoa hifadhini kwamba watalipwa ama hawastahili kulipwa, wananchi watapewa taarifa na baada ya hapo tutaanza kutatua hii migogoro kwa kushirikishana, hatutaenda kwa nguvu kwa kuwa Mheshimiwa Rais alishasema, hataki kuona taharuki.

Kwa hiyo, nimhakikishie tu Mbunge kwamba pamoja na kuwa ametaka niende kule, lakini kwa kuwa timu ya tathmini iko uwandani, tuiache ifanye kazi. Tunapoenda sasa kuongea na wananchi tuwe na kitu cha kuwaambia wananchi bila kuweka taharuki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie kwamba tutatatua tatizo hili na tutaambatana naye baada ya tathmini kukamilika.

Name

Saashisha Elinikyo Mafuwe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Hai

Primary Question

MHE. GODWIN E. KUNAMBI aliuliza: - Je, ni lini Serikali itatatua mgogoro kati ya wananchi na TAWA katika Bonde la Mto Kilombero?

Supplementary Question 2

MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana; ili kuepusha migogoro na kutengeneza sense of ownership kati ya wananchi wa Jimbo la Hai hususan wanaozunguka Mlima Kilimanjaro na KINAPA. Tuliandika barua ya kuomba fedha za CSR ili kutekeleza miradi kwenye vijiji vinavyozunguka Mlima Kilimanjaro, na tayari Mheshimiwa Naibu Waziri ulipokea, nilikuletea mwenyewe. Je, ni lini Serikali itatuletea fedha hizi?

Name

Mary Francis Masanja

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Saashisha, Mbunge wa Hai kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba Wizara kupitia taasisi zake huwa tunatoa CSR kwa jamii zinazozunguka hifadhi, na Mlima Kilimanjaro una jamii mbalimbali zinazozunguka hifadhi hiyo. Kwa kuwa hapa katikati tulikuwa tuna changamoto ya UVIKO–19 Wizara yetu ilikumbana na changamoto hiyo, hivyo hatukuweza kupeleka CSR kwa wananchi kama ambavyo tulikuwa tumepanga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge na wananchi wote wa Hai, kwamba sasa hivi utalii umeanza kuimarika vizuri. Tumeanza kupata wageni wengi, tuna uhakika kabisa kwamba ile sense of ownership ya wananchi wa Hai na maeneo mengine yanayozunguka hifadhi ya Mlima Kilimanjaro wataenda kuiona na watafaidika nayo kupitia CSR.

Name

Daniel Baran Sillo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Babati Vijijini

Primary Question

MHE. GODWIN E. KUNAMBI aliuliza: - Je, ni lini Serikali itatatua mgogoro kati ya wananchi na TAWA katika Bonde la Mto Kilombero?

Supplementary Question 3

MHE. DANIEL B. SILLO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa fursa niweze kuuliza swali moja la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa migogoro kati ya Hifadhi ya Tarangire na vijiji vya Gijedangu, Hayamango, Vilimavitatu na Salama ni vya muda mrefu.

Je, ni nini mkakati wa Serikali wa kuonesha kwamba migogoro hii inafika mwisho ili wananchi wetu waweze kufanya shughuli zao za kiuchumi? (Makofi)

Name

Mary Francis Masanja

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Sillo, Mbunge wa Babati kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ambavyo nimeeleza kwenye majibu ya nyongeza kwamba, maeneo yote ambayo yamezungukwa na hifadhi, Serikali itahakikisha wananchi wanafaidika na uhifadhi. Tunatambua kwamba hawa wananchi kwa asilimia kubwa wanatusaidia kusimamia maeneo haya. Sisi tuko huku makao makuu na pamoja na kuwa tuna wataumishi wetu walioko kwenye maeneo ya hifadhi, lakini askari peke yake hawawezi kulinda haya maeneo bila kushikirisha wananchi ambao ndiyo hasa wenye uchungu wa haya maeneo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimuhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba CSR ni moja ya priority ya Wizara ama Serikali kuhakikisha kwamba wananchi wanajisikia kwamba ni sehemu ya hifadhi. Hivyo, tutahakikisha kwamba wananchi wa jimbo lake wanaona umuhimu wa uhifadhi ili waendelee kutusaidia kusimamia maeneo haya yanayozunguka hifadhi ya Tarangire. Ahsante.