Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Eng. Stella Martin Manyanya

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Nyasa

Primary Question

MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA aliuliza:- Je, kwa nini ukumbi wa VETA Nyasa haujawekwa vipooza joto?

Supplementary Question 1

MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwanza namshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yenye matumaini makubwa, lakini nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; kwa kuwa chuo cha VETA, Nyasa wakati huo kilikuwa na changamoto kubwa ya ulipaji wa fidia na kwa sababu kipo maeneo ambayo ni ya kimkakati, kwa hiyo eneo lake ni dogo kiasi kwamba uendelezaji wa chuo hicho unakuwa mgumu kwa hatua zinazofuata. Hakuna kiwanja cha mpira, lakini pia kwa fani nyingine kama za utalii ni ngumu kuendeleza hapo. Je, serikali ina mpango gani wa kuweza kuongeza eneo la chuo hicho?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; naomba kwa kuwa Wizara ni hiyo hiyo moja kupitia mradi wa EP4R, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ilijenga jengo la utawala na maktaba ya ghorofa katika Shule ya Sekondari Mbamba Bay ambayo kila siku nalisemea hilo jengo.

Je, ni lini jengo hili litaweza kukamilika na ikibidi Mheshimiwa Waziri sasa ifikie mahali wakatembelee wakaone hali halisi? (Makofi)

Name

Omary Juma Kipanga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mafia

Answer

NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Manyanya, Mbunge wa Nyasa, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na suala la eneo la chuo chetu cha VETA kuwa dogo, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge mimi pamoja na timu yangu ya wataalam wa VETA tutafanya ziara katika chuo hicho ili kujiridhisha na ukubwa wa hilo eneo. Kama kutakuwa na uhitaji wa kuongeza eneo, nimwondoe hofu, tulishalifanya jambo hilo katika Chuo chetu cha Kipawa ambacho kilikuwa na eneo dogo, tumeweza kuongeza eneo, basi na hapa katika Chuo chetu hiki cha VETA tutafanya ziara lakini vilevile tutahakikisha kwamba kama kutakuwa na eneo linahitajika kuongeza, Serikali itaweza kuongeza eneo hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika swali la pili katika shule hiyo aliyoitaja ya Sekondari ya Mbambabay kwamba Serikali ilishapeleka fedha kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu. Pia, kuna hili jengo la utawala ambalo halijakamilika, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, Wizara yangu kwa kushirikiana na wenzetu wa TAMISEMI, tutafanya ziara katika eneo hilo. Vilevile, tumuagize Mkurugenzi wa Halmashauri ya Nyasa kuweza kufanya tathmini ya jengo hilo, kuona ni kiasi gani cha fedha kinahitajika ili basi Serikali iweze kupata tathmini hiyo na kuweza kuifanyia kazi ili jengo hili liweze kukamilika, nakushukuru.