Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Yustina Arcadius Rahhi

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. YUSTINA A. RAHHI aliuliza:- Je, Serikali ina mpango gani wa utambuzi wa mifugo baada ya kusitisha zoezi la utambuzi kwa kutumia hereni za mifugo? MWENYEKITI: Mheshimiwa Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mheshimiwa Alexander Mnyeti majibu.

Supplementary Question 1

MHE. YUSTINA A. RAHHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa majibu mazuri ya Serikali, nina maswali mawili ya nyongeza. Kwanza ni kweli Serikali ilisitisha zoezi hili la utambuzi wa mifugo kwa kutumia hereni za kieletroniki mwaka jana 2022, Novemba tarehe kama hii, ili kuipa Wizara kufanya tathmini ya upungufu. Kutokana na umuhimu wa zoezi la utambuzi wa mifugo ambacho ndicho kinachoweza kuondoa migogoro kati ya wafugaji, na kusababisha mifugo kuhamahama na kuingiliana pamoja na wizi wa mifugo; changamoto ambayo iko kwa wafugaji wadogo zaidi kuliko wa mashamba makubwa, ambapo ufugaji kule uko salama na idadi yake inafahamika: Ni lini sasa Serikali itafanya zoezi hili kwa wafugaji wa kawaida na wadogo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili, kuna changamoto ya takwimu ya uhakika ya mifugo. Ni lini Serikali itafanya sensa ya mifugo ili tuwe na takwimu halisi ya mifugo katika nchi yetu? Ahsante.

Name

Alexander Pastory Mnyeti

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Misungwi

Answer

NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, kwanza nianze na hili la hereni kwamba ni kweli Serikali ilisitisha na sasa mwaka mmoja umepita. Serikali imesitisha baada ya zoezi hili kulalamikiwa sana na wadau, hasa wafugaji wadogo wadogo. Sasa Serikali ilichokifanya ni kuainisha changamoto zile ambazo wafugaji wanazilalamikia na kutafuta majawabu sahihi. Baada ya kupata hayo majawabu sahihi, na kwa kuwa zoezi hili lilizuiliwa na Mheshimiwa Waziri Mkuu, tulichokifanya Wizara ni kumwandikia Mheshimiwa Waziri Mkuu kwamba sasa tunashughulikia changamoto zote ambazo wafugaji wameziainisha, kwamba majibu yake sasa tayari tunayo na Mheshimiwa Waziri Mkuu tayari amesharuhusu tuendelee na zoezi hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nikuhakikishie kwamba zoezi hili litaanza mara moja, hivi punde kadiri ambavyo maelekezo ya Mheshimiwa Waziri Mkuu yalivyotolewa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili amelisema hapa kuhusu sensa. Ni kweli kwamba sensa hii huwa inafanyika kila baada ya miaka mwili. Sensa ya mwisho ilifanyika mwaka wa fedha 1920 na mwaka huu sasa tutafanya sensa 2023 kwa ajili ya kubaini idadi halisi ya mifugo tuliyonayo katika Taifa letu. Sensa hii tunashirikiana na watu wa NBS, wanaoshughulika na masuala ya takwimu kuhakikisha kwamba takwimu tunazozipata zinalenga kwenye kuleta tija katika Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha. (Makofi)