Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Japhet Ngailonga Hasunga (CPA)

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Vwawa

Primary Question

MHE. JAPHET N. HASUNGA aliuliza:- Je, lini Serikali itatoa fedha kumalizia ujenzi wa maboma ya shule za msingi na sekondari yaliyojengwa kwa nguvu za wananchi Mbozi?

Supplementary Question 1

MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwa kuwa wananchi wamejitolea kwa kiwango kikubwa sana katika ujenzi wa maboma haya na waliahidiwa kwamba Serikali itakamilisha na maboma hayo ni mengi sana, je, Serikali haioni umuhimu wa kutenga bajeti maalum ili kukamilisha majengo hayo kuwaunga mkono wananchi hawa? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili; kwa kuwa katika maeneo mengi sasa hivi Serikali imekuwa ikipeleka fedha kwa ajili ya ujenzi wa madarasa mapya, ni kwa nini Serikali isipeleke fedha kukamilisha haya madarasa ambayo yameshaanzishwa na wananchi badala ya kuanza madarasa mapya? (Makofi)

Name

Deogratius John Ndejembi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Chamwino

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Spika, nikijibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Hasunga, la kwanza kwa nini isitengwe bajeti maalum kwa ajili ya ukamilishaji wa maboma haya?

Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema kwenye majibu yangu ya msingi, Serikali imekuwa ikishirikiana na wadau mbalimbali na wananchi wenyewe katika kuhakikisha kwamba maboma yaliyojengwa kwa nguvu za wananchi nchini kote yanakamilishwa. Hivi sasa Serikali hii ya Awamu ya Sita ya Dkt. Samia Suluhu Hassan ipo katika mchakato wa kutafuta fedha kwa ajili ya kwenda kuunga mkono jitihada za wananchi nchini kote waliojenga maboma yao ikiwemo kule jimboni kwa Mheshimiwa Hasunga ambapo kuna maboma zaidi ya elfu moja na mia tano kwa ajili ya kwenda kuyakamilisha.

Mheshimiwa Spika, nikienda kwenye swali lake la pili; kwa nini hizi fedha zinazokwenda sasa kwenye kujenga madarasa, kwenye kujenga shule mpya zisiende kwa ajili ya kumalizia yale maboma?

Mheshimiwa Spika, Serikali imekuwa ikijenga shule na madarasa kupitia miradi mbalimbali, ambayo ni vigezo vya miradi ile kuhakikisha kwamba inajenga madarasa mapya inajenga shule mpya na kupimwa kulingana na matokeo yale yanayotokana na ujenzi ili tuweze kupata fedha nyingine nyingi zaidi kwa ajili ya kujenga shule nyingine nyingi na madarasa mengine mengi.

Mheshimiwa Spika, nirejee katika majibu yangu ya swali lake la nyongeza la kwanza, Serikali hii ya Awamu ya Sita ya Dkt. Samia Suluhu Hassan ipo katika mchakato wa kutafuta fedha kwa ajili ya kuunga mkono jitihada za wananchi nchini kote waliojenga maboma ya madarasa. Vilevile kuna fedha ile ya maendeleo ambayo Halmashauri inatakiwa kutenga na ndiyo kazi yake hii, Wakurugenzi kuhakikisha kwamba wanaunga mkono jitihada za wananchi kwa kutumia fedha ile ya maendeleo kwenye halmashauri zao.

Name

Shabani Omari Shekilindi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Lushoto

Primary Question

MHE. JAPHET N. HASUNGA aliuliza:- Je, lini Serikali itatoa fedha kumalizia ujenzi wa maboma ya shule za msingi na sekondari yaliyojengwa kwa nguvu za wananchi Mbozi?

Supplementary Question 2

MHE. SHABANI O. SHEKILINDI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Shule za msingi Kwai, Kweboma zimechoka mno; je, ni lini Serikali itapeleka fedha za ukarabati katika shule hizo? (Makofi)

Name

Deogratius John Ndejembi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Chamwino

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Spika, Serikali hii ya Awamu ya Sita ilitenga zaidi ya bilioni 230 kote nchini kwa ajili ya ukarabati wa shule za msingi zilizochoka na ujenzi wa shule mpya za msingi, zikiwemo nyingine kule Jimboni kwa Mheshimiwa Shekilindi. Hizi shule alizozitaja za Kwai na kwingineko Serikali itaendelea kutafuta fedha na kadri ya upatikanaji wa fedha itapeleka fedha kwa ajili ya ukarabati wa shule hizi.