Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Hussein Nassor Amar

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nyang'hwale

Primary Question

MHE. HUSSEIN N. AMAR aliuliza: - Je, ni lini upembuzi yakinifu utakamilika na kuanza ujenzi wa barabara ya Kahama – Nyang’hwale – Busisi?

Supplementary Question 1

MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Kwanza kabisa sijaridhika sana na haya majibu, lakini kwa kuwa Mheshimiwa Waziri anasema kwamba mzabuni tayari ameshapatikana…

SPIKA: Mheshimiwa ngoja, hujaridhika kwamba ni majibu hayana..., yaani siyo ya kweli, hayana uhalisia ama? Kwa sababu kanuni zetu zinataka swali lijibiwe kikamilifu. Hujaridhika kwa namna gani?

MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Spika, majibu haya hayana uhalisia.

SPIKA: Fafanua.

MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Spika, naomba nifafanue. Kwa kuwa Mheshimiwa Waziri amesema kwamba mzabuni tayari amepatikana na anaenda kupata Msanifu Mshauri na kuianza kazi hiyo mwaka 2024 na kumaliza 2025. Kwa nini nasema kwamba halipo sawasawa, fedha ambayo ilikuwa imetengwa kwa ajili ya usanifu kwa mwaka wa fedha 2021 na kutolewa mwaka 2022, fedha hiyo ilitengwa shilingi milioni 300 na kutolewa shilingi milioni 150 kwa ajili ya kuanza kazi hiyo mwaka 2022.

Mheshimiwa Spika, leo ananiambia anaenda kupatikana Msanifu mwaka 2024 na kumaliza kazi hiyo mwaka 2025, hapa majibu haya yanakinzana.

Mheshimiwa Spika, niendelee?

Name

Eng. Godfrey Msongwe Kasekenya

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ileje

Answer

NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Hata katika jibu langu la msingi, siyo kwamba Mhandisi Mshauri amepatikana. Ila tayari zabuni ya manunuzi kumpata huyo Mhandisi Mshauri, ndiyo tunakwenda kutangaza.

Mheshimiwa Spika, kwenye bajeti ya 2022/2023 tulitenga bajeti kwa ajili ya kuanza kazi hiyo. Hiyo bajeti ambayo imetupelekea sisi kuanza kutangaza na hata katika mwaka huu wa fedha pia kwenye vitabu vyetu vya bajeti, bado tumetenga katika kuendelea kufanya hiyo kazi ya usanifu wa kina wa barabara hiyo, ahsante.

SPIKA: Sawa, hapo kwenye jibu lako panaposema hivyo, kazi zitakamilika mwezi Februari, 2025. Ni kazi zipi, hizi za usanifu ama za ujenzi?

NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Spika, ni kazi za usanifu, kwa barabara ilivyo haiwezi ikafanyika…

Name

Hussein Nassor Amar

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nyang'hwale

Primary Question

MHE. HUSSEIN N. AMAR aliuliza: - Je, ni lini upembuzi yakinifu utakamilika na kuanza ujenzi wa barabara ya Kahama – Nyang’hwale – Busisi?

Supplementary Question 2

MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Spika, sawa.

Mheshimiwa Spika, kwenye kikao cha ushauri wa barabara cha mkoa, mwaka 2022 niliambiwa zimeshatoka shilingi milioni 150 na kazi ya upembuzi yakinifu imeanza…

SPIKA: Mheshimiwa Nassor, ngoja. Ili taarifa zetu zikae vizuri kule ulipoambiwa siyo Serikali Kuu inayokuwepo, ni nyinyi watu wa mkoa ule ndiyo mpo kule. Kwa hiyo nilitaka ufafanuzi huu ili taarifa zetu zikae vizuri, kwa hiyo Mheshimiwa Naibu Waziri amefafanua kwamba kazi zitakazokamilika ni hizi zinazoendelea mpaka sasa.

Sasa kile kikao kule, wewe ulikuwepo ila mimi sikuwepo wala Mheshimiwa Naibu Waziri, kwa hiyo hawezi kufafanua kuhusu kile ulichoambiwa kule. Kwa hiyo tuanzie hiki cha leo hapa Mheshimiwa, uliza maswali yako mawili ya nyongeza.

MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Spika, hata kwenye Hansard wakiangalia 2022 ni kwamba imeshatengwa fedha shilingi milioni 150 na kwenye vitabu vya bajeti ilionyesha kabisa kwamba zimeshatengwa na zimetolewa. Sasa hii leo wananiambia ni Msanifu anayeenda kupatikana 2024. Wakati kule tumeambiwa kwamba Msanifu ameshaanza kazi.

SPIKA: Sawa, sasa kwa maelezo yako mwenyewe hapo unasema zimetengwa na zimeshatolewa kwenye bajeti.

MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Spika, ndiyo.

SPIKA: Kwenye bajeti, nafikiri huwa tunatenga ama?

MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Spika, zilitengwa shilingi milioni 300 kwa 2020/2021 na mwaka 2022 ni kwamba tayari zikawa zimeshatolewa shilingi milioni 150.

SPIKA: Sawa, sasa kwa sababu kwenye jibu la msingi Mheshimiwa Naibu Waziri, ametaja. Kwa sababu swali lako linasema, je ni lini upembuzi yakinifu utakamilika na kuanza ujenzi wa barabara ya Kahama - Nyang’hwale - Busisi, jibu la msingi linasema utakamilika Februari, 2025. Nilitaka kujiridhisha hapo uliposema, hujaridhika na majibu. Sasa uliza maswali yako ya nyongeza kuhusu hili ambalo umeliuliza kwenye swali lako la msingi.

MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Spika, basi swali la pili; kwa kuwa ahadi hiyo imechukua muda mrefu, mtoto amezaliwa na amefikisha miaka 14 tangu mwaka 2010 ahadi hii imeahidiwa na Viongozi Wakuu wa Nchi, mpaka leo hii tuna miaka 13 tunakaa tunaambiwa maneno haya. Sisi wana Nyang’hwale tunataka majibu ya Serikali. Hivi ni kweli 2024 unavyosema na 2025 namwomba Mheshimiwa Waziri, baada ya Bunge hili twende akawaambie wananchi dhamira ya Serikali ya kukamilisha ahadi hii. (Makofi)

Name

Innocent Lugha Bashungwa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Karagwe

Answer

WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Spika, kwanza nikushukuru kwa kunipa nafasi, lakini pia nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri. Mheshimiwa Naibu Waziri anafanya kazi nzuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kaka yangu Mheshimiwa Hussein Amar, naomba hoja yake niichukue. Nimpongeze, juzi tulikuwa tuna kikao, Mheshimiwa Hussein Amar pamoja na Mheshimiwa Iddi, Mbunge wa Jimbo la Msalala, tulikaa na Barrick, kuna barabara ya kutoka Kahama kwenda Bulyanhulu kwenda Geita. (Makofi)

Mheshimiwa Amar, aliomba lami itakapofika kwenye geti la Barrick akaomba kipande cha kwenda Jimboni kwake tukae na Barrick ili kama kutakuwa kuna bakaa tujenge kile kipande. Kwa hiyo kaka yangu Mheshimiwa Amar naomba aendelee kuwa na confidence na Serikali. Hoja yake tumeichukua kwa kadri fedha zitakapopatikana na suala la usanifu tutaweka jitihada, lakini dhamira ya Serikali ni kujenga lami kwenye barabara zote ambazo upembuzi yakinifu umekamilika. Tupo pamoja Mheshimiwa Mbunge na nampongeza kwa namna ambavyo anapambana kwa wananchi wa Jimbo la Nyang’hwale. (Makofi)