Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Cecil David Mwambe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ndanda

Primary Question

MHE. CECIL D. MWAMBE (K.n.y. MHE. LATHIFAH H. CHANDE) aliuliza:- Mji wa Liwale umebakia kuwa ni Wilaya pekee ya Mkoa wa Lindi ambayo haijanufaika na umeme wa uhakika wa gesi asilia. Umeme unaotumika ni wa jenereta mbili za diseli za kW 800:- Je, ni kwa nini Serikali isitenge fedha ili kuiunganisha Wilaya nzima ya Liwale na umeme wa gesi asilia?

Supplementary Question 1

MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, nina maswali mawili ya nyongeza kwa Wizara ya Nishati na Madini. Kwa vile Wilaya za Masasi, Nanyumbu na hasa Masasi Mjini, Kijiji cha Ndanda pamoja na Chikundi, kuna tatizo sana la umeme kukatika kila mara na umeme huu ndiyo ambao tunaambiwa sasa unapelekwa Liwale. Je, Mheshimiwa Waziri anawahakikishiaje wakazi wa Liwale kuwa na umeme wa uhakika, wasije wakapata matatizo ambayo wakazi wa Masasi wanayapata kila mara?
Swali la pili, tuliambiwa watakapoanza kutumia umeme wa gesi, basi hata gharama za kuunganisha, lakini pia na gharama za kuwafikia wale wakazi umeme toka siku ambazo wamelipia zitakuwa ni chache sana. Katika hali ya kushangaza kuna wakazi wa maeneo ya Nachingwea, pia Ndanda na hizo Wilaya nyingine nilizozitaja wanaweza kukaa hata miezi mitatu au minne bila kuunganishiwa umeme toka tarehe waliyolipa. Pia, kuna vijiji vingi ambavyo vinapitiwa na nguzo kuu za umeme zinazokwenda Liwale na Masasi Mjini; Unawaambiaje wakazi wa Masasi juu ya mambo haya mawili?

Name

Dr. Medard Matogolo Kalemani

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Chato

Answer

NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa kuna changamoto za upatikanaji wa umeme hasa katika maeneo ya Masasi na Nanyumbu, siyo Masasi tu hata maeneo mengine ya Liwale pamoja na Nachingwea. Hata hivyo, juhudi zilizofanyika ni kubwa. Nimhakikishie Mheshimiwa Cecil Mwambe kwamba kazi inaendelea. Hata hivyo, kwenye Awamu ya Pili ya REA ni vijiji kwa Wilaya zote alizotaja 152 vimepatiwa umeme.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa kuna vijiji mia moja na kumi na moja (111) kwa Wilaya zote havijapata umeme. Mkakati uliopo kwa niaba ya wananchi wa maeneo ya Masasi, Nanyumbu, Nachingwea na maeneo ya karibu yatapelekewa umeme kwenye REA Awamu ya Tatu inayoanza mwezi Oktoba, Novemba hadi Disemba mwaka huu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na suala la uhakika wa umeme kwa wananchi wa Masasi nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge na nakushukuru sana kwa sababu umekuwa ukifuatilia jambo hili. Suala la upatikanaji wa umeme kwa Wilaya za Masasi na maeneo ya jirani linafanyiwa kazi na kwa kweli litatatulika kwa muda mfupi sana kuanzia sasa.
Mheshimiwa Naibu Spika, gharama za umeme; kwanza kabisa nichukue nafasi hii kuwaeleza wananchi kwamba gharama za umeme kwa kweli zinashuka. Ni kweli kabisa baada ya kuanza kutumia gesi asilia gharama za umeme zimeshuka na kwa nchi nzima. Gharama za umeme kwa miradi ya REA ni sh. 27,000 na hiyo ni nchi nzima.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, gharama za kulipa umeme kwa wananchi wanaotumia gesi asilia, hasa kwa Mikoa ya Lindi na Mtwara na maeneo ya jirani, hata kwa kazi wanazounganishiwa na TANESCO ni za chini; badala ya sh. 177 kwa mikoa hiyo miwili ni sh. 99. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge tutaendelea kutumia gharama hizo kwa Mikoa ya Lindi, Mtwara pamoja na Wilaya nyingine za Masasi na Nanyumbu.