Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Josephine Tabitha Chagulla
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. JOSEPHINE T. CHAGULA aliuliza:- Je, lini Serikali itapeleka walimu katika shule za sekondari na msingi Wilayani Nyang’hwale?
Supplementary Question 1
MHE. JOSEPHINE T. CHAGULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana na nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri ya Serikali, lakini nina swali la nyongeza:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa, shule za sekondari za kata zimeonesha mafanikio makubwa sana katika ufaulu, lakini tatizo lililopo ni kufeli kwa somo la hesabu na mwanafunzi anapopata F ya hesabu inakuwa imemuharibia kabisa kombi yake.
Je, Serikali ina mpango gani sasa wa haraka wa kupeleka walimu wa somo la hesabu katika shule zetu hizi za kata, ili tuweze kupunguza au kutoa F hizo zinazojitokeza kwa watoto wetu?
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini swali la pili, kumekuwa na changamoto kubwa kwa walimu wetu wa shule za msingi na sekondari kupata uhamisho kuwafuata wenza wao na hasa hawa ajira mpya. Je, Serikali ina mpango gani sasa wa kuwapangia moja kwa moja walimu hawa kuwafuata wenza wao kwa vile wana vyeti vya ndoa, ili tuweze kutoa usumbufu huo wanaoupata walimu wetu hawa? Ahsante.
Name
Deogratius John Ndejembi
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Chamwino
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Mwenyekiti, nikijibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Chagula; la kwanza hili juu ya kuajiri walimu wa hesabu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema kwenye majibu yangu ya msingi, Serikali hivi karibuni itatangaza ajira za walimu. Na katika ajira hizo kipaumbele kitakuwa kwa walimu wa sayansi na hisabati ambao wataajiriwa. Kwa hiyo, nimuombe Mheshimiwa Mbunge na Waheshimiwa Wabunge wengine humu ndani, kuwa na subira pale ajira hizi zitakapotangazwa basi walimu hawa wa hesabu na sayansi wataajriwa na kwenda katika halmashauri mbalimbali hapa nchini, ili kuongeza nguvu katika shule zetu za kata ambazo Mheshimiwa Rais wetu, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amewekeza fedha nyingi zaidi ya bilioni 219 katika kuhakikisha kuna shule mpya za sekondari kwenye kata ambazo zilikuwa bado hazina shule hizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikienda kwenye swali lake la pili la uhamisho wa kuweza kuwafuata wenza; Serikali hutoa ajira kulingana na upungufu uliopo. Tathmini hufanyika nchi nzima kuangalia maeneo mbalimbali ambayo yana upungufu wa walimu kisha ndipo kibali hutolewa kwa ajili ya kuajiri wale walimu kwenda kuziba yale mapengo. Kwa hiyo, mtu anapoomba ajira anaenda kwenye eneo kuziba pengo ni lazima atumikie kwanza mwaka mmoja kwa ajili ya kuweza kuthibitishwa kazini akiwa katika eneo lile ambalo amepangiwa. Baada ya kuthibitishwa kazini baada ya ule mwaka mmoja anatakiwa aendelee kuwepo kwenye kile kituo cha kazi kwa miaka mingine isiyopungua miwili ambayo jumla inakuwa ni miaka mitatu ndipo aweze kuona ni namna gani anahama katika kituo kile na kwenda kituo kingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ajira hizi si kwamba, ni njia tu ya kuingilia kwenye ajira ya Serikali halafu aweze kuhama na kuhamia maeneo mengine na mara nyingi wanaotaka kuhama huwa wanahamia kwenye majiji na Manispaa, wale waliokuwa pembezoni huwa mara nyingi wanataka kuhama. Sasa tukisema mtu tu akishapata check number aweze kuomba uhamisho na kumfuata mwenza wake ina maana maeneo ya pembezoni mwa nchi yetu kutaendelea kuwa na upungufu wa idadi ya walimu ambao wanahitajika. (Makofi)
Name
Daniel Baran Sillo
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Babati Vijijini
Primary Question
MHE. JOSEPHINE T. CHAGULA aliuliza:- Je, lini Serikali itapeleka walimu katika shule za sekondari na msingi Wilayani Nyang’hwale?
Supplementary Question 2
MHE. DANIEL B. SILLO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwa kuwa, mahitaji ya walimu wa shule za msingi katika Jimbo la Babati Vijijini ni 2,349 na waliopo ni 1,379 hivyo kuwa na upungufu wa walimu 970. Je, Serikali ina mpango gani wa kuongeza walimu katika shule za msingi?
Name
Deogratius John Ndejembi
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Chamwino
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Mwenyekiti, nikijibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Sillo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka wa fedha 2021/2022 na 2022/2023 Serikali iliajiri walimu na katika ajira hizo Jimboni kwa Mheshimiwa Sillo nako walipata walimu wapya, walienda katika shule za msingi na shule za sekondari. Kama nilivyosema kwenye majibu yangu ya msingi, Serikali inaendelea kutoa ajira mpya na hivi karibuni zitatangazwa na baada ya kupatikana hawa waajiriwa wapya tutaweka kipaumbele vilevile kule kwa Mheshimiwa Sillo.
Name
Minza Simon Mjika
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. JOSEPHINE T. CHAGULA aliuliza:- Je, lini Serikali itapeleka walimu katika shule za sekondari na msingi Wilayani Nyang’hwale?
Supplementary Question 3
MHE. MINZA S. MJIKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naishukuru sana Serikali yangu kwa kutujengea shule nyingi za sekondari na msingi katika Mkoa wa Simiyu, lakini kuna upungufu mkubwa wa walimu. Je, ni lini Serikali italeta walimu wa kutosha katika Mkoa wetu wa Simiyu?
Name
Deogratius John Ndejembi
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Chamwino
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itapeleka walimu zaidi katika Mkoa wa Simiyu pale ambapo ajira hizi ambazo nimesema zitatangazwa hivi karibuni zitakamilika mchakato wake na wao wenyewe katika Mkoa wa Simiyu watapata mgawo wa walimu hao wapya.
Name
Hussein Nassor Amar
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Nyang'hwale
Primary Question
MHE. JOSEPHINE T. CHAGULA aliuliza:- Je, lini Serikali itapeleka walimu katika shule za sekondari na msingi Wilayani Nyang’hwale?
Supplementary Question 4
MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kuniona. Kwanza niipongeze Serikali kwa kuendelea kupunguza upungufu wa walimu katika Wilaya ya Nyang’hwale.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri, uko tayari kumuelekeza Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya Nyang’hwale azipitie shule zote zikiwemo za sekondari na msingi kuangalia uwiano wa walimu ‘ke’ na ‘me’ kwa sababu, kuna baadhi ya shule za msingi zina wanawake peke yake na baadhi ya shule za msingi zina wanaume peke yake, ikiwemo Shule ya Msingi ya Mama Samia.
Name
Deogratius John Ndejembi
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Chamwino
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Mwenyekiti, nikijibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Amar:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, nipo tayari kumuelekeza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Nyang’hwale kuweza kufanya tathmini hiyo na ninaomba kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, kuchukua nafasi hii kumuelekeza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Nyang’hwale kuanza kufanya tathmini hii, kama alivyoshauri Mheshimiwa Amar na kuona ni namna gani anafanya msawazo wa ikama ndani ya halmashauri yake katika walimu. (Makofi)
Name
Saashisha Elinikyo Mafuwe
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Hai
Primary Question
MHE. JOSEPHINE T. CHAGULA aliuliza:- Je, lini Serikali itapeleka walimu katika shule za sekondari na msingi Wilayani Nyang’hwale?
Supplementary Question 5
MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, katika Wilaya ya Hai tunaishukuru Serikali imetujengea shule tatu mpya kwa hivyo, kuongeza mahitaji ya watumishi pamoja na kujengewa vituo vitano vya afya. Je, ni lini sasa Serikali itatuletea watumishi kwenye maeneo haya ya elimu na afya?
Name
Deogratius John Ndejembi
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Chamwino
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Mwenyekiti, nikirejea majibu yangu ya msingi, nikijibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Saashisha Elinikyo Mafuwe:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali italeta watumishi hawa, hasa walimu katika hii ajira mpya ambayo itatangazwa hivi karibuni, basi Wilayani Hai nako mtapata mgawo katika walimu hao.
Name
Josephine Johnson Genzabuke
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. JOSEPHINE T. CHAGULA aliuliza:- Je, lini Serikali itapeleka walimu katika shule za sekondari na msingi Wilayani Nyang’hwale?
Supplementary Question 6
MHE. JOSEPHINE J. GENZABUKE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante; je, Serikali ina mpango gani mahususi wa kupeleka walimu katika maeneo ya pembezoni, ikiwa ni pamoja na Mkoa wa Kigoma?
Name
Deogratius John Ndejembi
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Chamwino
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeendelea kufanya tathmini ya upungufu wa walimu waliopo kote nchini, yakiwemo maeneo ya pembezoni, kama vile Mkoa wa Kigoma na kwenye ajira hizi mpya ambazo zitatolewa Serikali itaendelea kuweka kipaumbele hasa katika maeneo ya pembezoni ambayo yana uhitaji mkubwa wa walimu, ikiwemo Mkoani Kigoma.
Name
Sophia Hebron Mwakagenda
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. JOSEPHINE T. CHAGULA aliuliza:- Je, lini Serikali itapeleka walimu katika shule za sekondari na msingi Wilayani Nyang’hwale?
Supplementary Question 7
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la uhamisho kwa walimu wanawake au wanaume kufuata wenza wao ni suala muhimu sana kwa ajili ya maadili, lakini pia, kulinda ndoa za walimu hawa. Mnaonaje Serikali kuhakikisha wale ambao wamefunga ndoa kweli, waende wakafuate wenza wao kuepukana na matatizo na maambukizi na mambo mengine kama hayo?
Name
Deogratius John Ndejembi
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Chamwino
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilipokuwa nikijibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Chagula, utumishi wa umma unaongozwa kwa sheria, taratibu na kanuni na miongozo mbalimbali iliyomo katika utumishi wa umma. Na mtu anapokuwa ameajiriwa katika utumishi wa umma anafuata zile sheria, taratibu na kanuni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Sheria inasema ajira mpya atafanya kazi kwa mwaka mmoja kisha atafanyiwa assessment na kuthibitishwa kazini. Baada ya kuthibitishwa kazini ni lazima atumikie nafasi kwa muda usiopungua miaka miwili katika lile eneo ambalo yupo, baada ya hapo anaruhusiwa kuomba uhamisho kwenda katika eneo lolote la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, lakini hilo linategemea pia na uwepo wa nafasi kule anakotaka kwenda kwamba, ule mshahara wake ile bajeti je, imetengwa kwa muajiri yule anayetaka kuhamia.
Kwa hiyo, Serikali haikatishi mtu tamaa kuweza kuhama, lakini pia, inatakiwa kufuata sheria, taratibu na kanuni na miongozo iliyopo ya utumishi wa umma.