Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Joseph Zacharius Kamonga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ludewa

Primary Question

MHE. JOSEPH Z. KAMONGA aliuliza: - Je, Serikali ina mpango gani wa kupandisha hadhi Zahanati za Madope na Ludende kuwa Vituo vya Afya?

Supplementary Question 1

MHE. JOSEPH Z. KAMONGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi. Pamoja na majibu ya Serikali, ninayo maswali mawili madogo ya nyongeza. Swali la kwanza; wananchi wa Kijiji cha Chanjale kilichopo Kata ya Lumbila, baada ya kuona wanatembea kilometa 22 kufuata huduma za zahanati, mwaka 2014 walianza kujenga zahanati yao, lakini hadi leo haijakamilika. Je, ni ipi kauli ya matumaini kutoka kwa Serikali juu ya Zahanati hii ya Chanjale ili wananchi waweze kupata huduma?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; wananchi wa Kata ya Madope ambao wako 9,000 wanakaribia 10,000 na wao walianza jitihada za kujenga kituo cha afya ambacho Serikali ilituma wataalam kutoka Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kwenda kukagua, wakaahidi kuwa watapeleka fedha kutoka Benki ya Dunia, lakini mpaka leo ikiwa ni mwaka wa pili bado hiyo fedha haijaenda. Je, ni lini Serikali itapeleka fedha hiyo ili kukamilisha Kituo cha Afya cha Kata ya Madilu?

Name

Dr. Festo John Dugange

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wanging'ombe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naomba kutumia nafasi hii kuwapongeza wananchi wa Kijiji cha Chanjale kwa kuchangia nguvu zao kwa ajili ya ujenzi wa zahanati. Naomba kuwapa habari njema kwamba, Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesikia kilio chao kupitia kwa Mheshimiwa Mbunge wa jimbo hilo, Mheshimiwa Kamonga. Ifikapo tarehe 30 Aprili, ile fedha shilingi milioni 20, itakuwa imepelekwa katika Kijiji cha Chanjale kwa ajili ya kukamilisha ile zahanati.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile Mheshimiwa Rais amepeleka shilingi milioni 50 katika Kijiji hicho cha Chanjale kwa ajili ya ununuzi wa vifaatiba ili zahanati hii ikikamilika ianze kutoa huduma kwa wananchi. Natumia nafasi hii kumwelekeza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Ludewa kwamba, ifikapo tarehe 30 Juni, 2024 zahanati ile iwe imekamilika ili tarehe 1 Julai, 2024, wananchi wa Chanjale waanze kupata huduma za afya katika zahanati hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la pili, ni kweli kwamba, wananchi wa Kata ya Madilu wanahitaji kituo cha afya na tayari Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa imepeleka wataalam. Namhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba, kituo kile kipo kwenye orodha ya vituo ambavyo vitapewa fedha kupitia Mfuko wa Benki ya Dunia ambapo tunaamini kabla ya Mwezi Juni mwaka huu fedha zitakuwa zimefika na kazi za ujenzi zitaanza kutekelezwa. Ahsante. (Makofi)

Name

Selemani Moshi Kakoso

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mpanda Vijijini

Primary Question

MHE. JOSEPH Z. KAMONGA aliuliza: - Je, Serikali ina mpango gani wa kupandisha hadhi Zahanati za Madope na Ludende kuwa Vituo vya Afya?

Supplementary Question 2

MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Kijiji cha Kamsanga kina zahanati ambayo ina vigezo vinavyoipa hadhi ya kuwa kituo cha afya. Je, ni lini Serikali itaipandisha hadhi zahanati hiyo ya Kijiji cha Kamsanga?

Name

Dr. Festo John Dugange

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wanging'ombe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kupokea hoja ya Mheshimiwa Kakoso kuhusiana na uhitaji wa kuipandisha hadhi Zahanati ya Kamsamba kuwa Kituo cha Afya. Sisi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, kupitia Mganga Mkuu wa Mkoa na halmashauri tutafuatilia tathmini ya kukidhi vigezo na baadaye tutaweka mpango, ili fedha ikipatikana tuweze kuipandisha hadhi kuwa kituo cha afya, kama itakidhi vigezo vinavyotakiwa. Ahsante.

Name

Esther Lukago Midimu

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. JOSEPH Z. KAMONGA aliuliza: - Je, Serikali ina mpango gani wa kupandisha hadhi Zahanati za Madope na Ludende kuwa Vituo vya Afya?

Supplementary Question 3

MHE. ESTHER L. MIDIMU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza swali la nyongeza. Zahanati ya Sunzula, Wilaya ya Itilima inahudumia wananchi wengi sana. Je, ni lini Serikali itaipandisha hadhi zahanati hiyo kuwa kituo cha afya? (Makofi)

Name

Dr. Festo John Dugange

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wanging'ombe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, upandishaji wa hadhi zahanati kuwa vituo vya afya, unatokana na kukidhi vigezo ambavyo, kwanza, ni idadi ya wananchi wanaohudumiwa. Pili, ni eneo la zahanati yenyewe. Tatu ni umbali wa zahanati hiyo kutoka kituo cha afya kilicho karibu zaidi. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, tutaifuatilia zahanati hiyo ili kuona kama inakidhi vigezo hivyo na kama ni kata ya kimkakati basi tuweze kuanza mpango kwa ajili ya kuipandisha hadhi zahanati hiyo. Ahsante.

Name

Joseph Kasheku Musukuma

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Geita

Primary Question

MHE. JOSEPH Z. KAMONGA aliuliza: - Je, Serikali ina mpango gani wa kupandisha hadhi Zahanati za Madope na Ludende kuwa Vituo vya Afya?

Supplementary Question 4

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Nimeuliza zaidi ya mara tano, je, ni lini Mheshimiwa Waziri atatoa pesa kiasi cha shilingi milioni 500 ili kuweza kukamilisha Zahanati ya Nkome, ambayo Waziri anaifahamu, zahanati ambayo kwa mwezi inazalisha wastani wa watoto 420? (Makofi)

Name

Dr. Festo John Dugange

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wanging'ombe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza Mheshimiwa Musukuma na pia nawapongeza wananchi wa kata hiyo kwa kweli, kasi ya kuleta watoto ni kubwa sana, watoto 400 kwa mwezi ni kasi kubwa sana. Sisi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa tumefika pale, mimi mwenyewe nilifanya ziara na tumeweka mpango wa kutafuta fedha ili vituo kama vile vipandishwe hadhi kuwa vituo vya afya. Namhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba, Serikali ipo kazini inatafuta fedha, mara ikipatikana tutakwenda kujenga kituo cha afya katika eneo lile. Ahsante sana.

Name

Cecilia Daniel Paresso

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. JOSEPH Z. KAMONGA aliuliza: - Je, Serikali ina mpango gani wa kupandisha hadhi Zahanati za Madope na Ludende kuwa Vituo vya Afya?

Supplementary Question 5

MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Upandishaji hadhi wa baadhi ya zahanati hapa nchini kuwa vituo vya afya unafanywa na Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na huwa ni mchakato mrefu sana. Je, ni kwa nini Serikali isifikirie kukaimisha madaraka hayo kwenye Sekretarieti za Mikoa kwa kutumia vigezo vilevile baada ya kufanya tathmini ili kufupisha mlolongo huu mrefu?

Name

Dr. Festo John Dugange

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wanging'ombe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba, hakuna mlolongo mrefu wa kupandisha hadhi zahanati kuwa vituo vya afya kwa sababu, wanaohusika ni Mganga Mkuu wa Halmashauri kupitia CHMT na Mkurugenzi. Wanafanya tathmini, wanawasilisha kwa Mganga Mkuu wa Mkoa kupitia RAS na baadaye wanawasilisha Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kazi ambayo Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa inaifanya ni kutoa idhini, lakini mchakato wote unafanyika katika ngazi ya halmashauri. Tutaendelea kuboresha mchakato huo ili vituo ambavyo vinakidhi haja viweze kupandishwa hadhi kwa wakati. Ahsante sana.

Name

Salma Rashid Kikwete

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Mchinga

Primary Question

MHE. JOSEPH Z. KAMONGA aliuliza: - Je, Serikali ina mpango gani wa kupandisha hadhi Zahanati za Madope na Ludende kuwa Vituo vya Afya?

Supplementary Question 6

MHE. SALMA R. KIKWETE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Awali ya yote naomba kuwapa pole Watanzania kwa kadhia iliyowakumba ya mafuriko ikiwemo Mbeya na Lindi Manispaa. Swali langu, je, ni lini Kituo cha Afya cha Kitomanga kitapandishwa hadhi kwa kuwa kinakidhi vigezo vyote? Tamko hili la kupandishwa hadhi ni la miaka mingi, zaidi ya nane, iliyopita. Je, ni nini kauli ya Serikali kwa Kituo cha Kitomanga, ukizingatia Jimbo la Mchinga halina hospitali hata moja? (Makofi)

Name

Dr. Festo John Dugange

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wanging'ombe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza Mheshimiwa Mama Salma Kikwete, amefuatilia mara nyingi kuhusiana na haja ya kupandisha Kituo cha Afya cha Kitomanga kuwa Hospitali ya Halmashauri. Namhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba, hili tumelipokea, tumeanza kulifanyia kazi na mara tutakapokamilisha utaratibu huo tutamletea taarifa rasmi kwamba, ni lini tunaanza kuongeza majengo ambayo yanastahili kuongezwa ili kituo kiwe na ngazi ya hospitali. Ahsante sana.