Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Fatma Hassan Toufiq
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. FATMA HASSAN TOUFIQ aliuliza:- Sheria ya Kutambua Haki ya Msaada wa Kisheria (Legal Aid) ambayo pia inawatambua wasaidizi wa kisheria (paralegals) mchakato wake umeanza tangu mwaka 2010 kwa kuwashirikisha wadau mbalimbali wakiwemo taasisi zisizo za Kiserikali, lakini sheria hii imekuwa ni ya muda mrefu na sasa ni zaidi ya miaka sita bado haijatajwa wala kuletwa Bungeni. Je, Serikali ina mkakati gani wa haraka wa kuhakikisha sheria hii inatungwa?
Supplementary Question 1
MHE. FATMA HASSAN TOUFIQ: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, kwa kuwa Serikali imeshakamilisha hatua za kuwasilisha muswada huu, je, ni lini muswada huu utawasilishwa Bungeni?
Swali la pili, je, Serikali ina mpango wowote wa kuandaa mtaala wa Wasaidizi wa Kisheria ili wote waweze kupata mafunzo kulingana na mtaala huo? Ahsante. (Makofi)
Name
Dr. Harrison George Mwakyembe
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kyela
Answer
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Fatma Toufiq kwa maswali yanayogusa wananchi wa kawaida na hili suala kwa kweli hata sisi kama Wizara tunaona ni muhimu na ndiyo maana tumelifuatilia kwa karibu na Serikali imeridhia tuweze kuja na muswada huo ambao utajadiliwa na Bunge.
Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge baada ya taratibu kukamilika, muswada huu hautakuja moja kwa moja Bungeni hapa lakini utapitia katika Kamati, pia tutakuwa na mjadala wa muda mrefu kabla ya kuja na text ambayo Waheshimiwa Wabunge mtakuja kuijadili.
Mheshimiwa Naibu Spika, pili, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba maandalizi ya kutosha tumeyafanya, kwa mfano, sasa hivi tuna mitaala kabisa iliyowekwa kwa ajili ya kuwafundisha hawa Wasaidizi wa Sheria. Ni kazi kubwa imefanywa na Chama cha Wanasheria Tanganyika na ninaomba nimhakikishie tu kwamba tumejiandaa vizuri sana kubeba hili jukumu.
Tunasema hivyo kwa sababu Ibara ya 13 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaongelea kuhusu usawa mbele ya sheria. Tunaamini Muswada huu unatupeleka Watanzania karibu zaidi katika kukidhi mahitaji ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano ili uwepo usawa wa kutosha kabisa mbele ya sheria.
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved