Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Noah Lemburis Saputi Mollel
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Arumeru-Magharibi
Primary Question
MHE. NOAH L. S. MOLLEL aliuliza: - Je, lini Serikali itawalipa fidia wananchi wa Kata ya Oldonyosambu ambao maeneo yao yalichukuliwa na Jeshi?
Supplementary Question 1
MHE. NOAH L. S. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu ya Serikali ambayo hayajaridhisha, nitakuwa na maswali mawili madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Eneo la Oldonyosambu la wananchi limechukuliwa mwaka 1983 wakapewa Jeshi na Serikali ikawaahidi Wananchi wa Oldonyosambu kwamba watapewa maeneo katika Eneo la Oljoro ikiwemo pamoja na wananchi wa Kata ya Mlangarini ambao walitakiwa kulipwa fidia yao mwaka jana mpaka sasa hawakuweza kupewa fidia.
Je, nini kauli ya Serikali kuwapa wananchi haki yao kwa maana ya fidia ili kuondokana na migogoro na wananchi?
Swali la pili, kwa kuwa maelezo ya Mheshimiwa Waziri yanahitaji utafiti kwenye majibu yake. Je, yuko tayari baada ya Bunge hili kuambatana na mimi kuelekea Jimboni kwenda kuzungumza na wale wananchi ili waweze kupata majibu halisi? (Makofi)
Name
Dr. Stergomena Lawrence Tax
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Nominated
Answer
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba ni dhamira ya Serikali kuhakikisha migogoro yote ya ardhi inatatuliwa na ndiyo maana Serikali iliunda Kamati ya Mawaziri wa Wizara Nane ambayo imekuwa ikifanya kazi na taarifa ya kina ilitolewa pia jana kwa kiasi fulani na kwa upande wetu kama Jeshi tulikuwa na migogoro 87 tumeishaitatua migogoro asilimia 90.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo hili alilolieleza la Mlangarini ni moja ya maeneo ambayo tumekwishayafanyia kazi. Ni kweli tulishafanya uthamini, tulishafanya upimaji na Wizara ya Fedha ilishafanya uhakiki. Kwa hiyo, hatua iliyosalia ni kuwalipa wananchi hao fidia yao na nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba wananchi wao watalipwa fidia yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu eneo ambalo liko kwenye swali la msingi ambalo ni Oldonyosambu, kama alivyoomba na kama nilivyoeleza kwamba kwa vile suala hili linatufikia kwa mara ya kwanza, halimo hata katika mpango wetu wa migogoro, basi Wizara tutatuma wataalamu kama nilivyokwishasema, pia niko tayari kuambatana nae baada ya kupata hii taarifa ya wataalam ili tuone tunaumaliza namna gani mgogoro huu. (Makofi)
Name
Sophia Hebron Mwakagenda
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. NOAH L. S. MOLLEL aliuliza: - Je, lini Serikali itawalipa fidia wananchi wa Kata ya Oldonyosambu ambao maeneo yao yalichukuliwa na Jeshi?
Supplementary Question 2
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Kwa kuwa, shida kubwa sana katika Jeshi inayotokea na wananchi katika masuala ya ardhi ni Jeshi kutokuwa na hatimiliki kwa baadhi ya makambi. Ni lini Serikali mtajipanga kuwapatia Hati Majeshi haya ili kusudi wasigombane na wananchi? (Makofi)
Name
Dr. Stergomena Lawrence Tax
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Nominated
Answer
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli yalikuwepo maeneo ambayo hatukuwa na hatimiliki, tulikuwa na maeneo ambayo yalihitaji uhakiki wa mipaka, kwa hiyo zoezi hili kama nilivyosema katika ile migogoro 87 limekwishafanyika. Kwa hiyo, tumekwishapima, tumekwisha hakiki na baadhi ya maeneo tayari tumekwishawasilisha Wazira ya Ardhi ili tuweze kupata Hatimiliki, kwa hiyo, tuna imani hili linakwenda kuisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu hii migogoro ni endelevu kila itakapotokea tutaendelea kuitatua kadri itakavyojitokeza. (Makofi)
Name
Athumani Almas Maige
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Tabora Kaskazini
Primary Question
MHE. NOAH L. S. MOLLEL aliuliza: - Je, lini Serikali itawalipa fidia wananchi wa Kata ya Oldonyosambu ambao maeneo yao yalichukuliwa na Jeshi?
Supplementary Question 3
MHE. ATHUMAN A. MAIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Ni lini Serikali italipa fidia kwa wananchi waliochukuliwa maeneo yao hivi karibuni katika Kata ya Mabama, Wilaya ya Uyui? (Makofi)
Name
Dr. Stergomena Lawrence Tax
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Nominated
Answer
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na naomba nijibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kata Mabama nafikiri huu ni mgogoro ambao unakuja kwa sasa hivi, kwa hiyo sisi tutakachokifanya ni kupata uhakika na baada ya kupata uhakika kama kweli wananchi eneo lao limevamiwa, basi taratibu zitafanywa za uhakiki na kama wanastahili fidia watalipwa fidia yao.
Name
Dennis Lazaro Londo
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mikumi
Primary Question
MHE. NOAH L. S. MOLLEL aliuliza: - Je, lini Serikali itawalipa fidia wananchi wa Kata ya Oldonyosambu ambao maeneo yao yalichukuliwa na Jeshi?
Supplementary Question 4
MHE. DENNIS L. LONDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, pale Mikumi tuna Kikosi cha Jeshi na moja ya mgogoro ambao wanao Wanakijiji wa Kijiji cha Vikweme na vitongoji ambavyo zinazunguka Vikweme pale Mikumi walitoa eneo lao kwa ajili ya mazoezi ya Jeshi, lakini Jeshi limechukua mpaka maeneo ya wananchi na taarifa hizo Serikali inayo. Je, ni nini kauli ya Serikali?
Name
Dr. Stergomena Lawrence Tax
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Nominated
Answer
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama alivyosema ni kwamba suala hili tumekuwa tukilishughulikia kwa pamoja, kwa hiyo tutaendelea kulishughulikia ili liweze kufikia hatma.
Copyright © Bunge Polis 2024. All Rights Reserved