Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Ameir Abdalla Ameir
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
House of Representatives
Primary Question
MHE. AMEIR ABDALLA AMEIR aliuliza: - Je, ni kwa kiasi gani BAKITA na BAKIZA zinaondoa changamoto za matumizi ya Lugha ya Kiswahili Kitaaluma na kijamii?
Supplementary Question 1
MHE. AMEIR ABDALLA AMEIR: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri ningeomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza ya ziada na kiada kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Lugha ya Kiswahili imekua kimawanda na kwa upana wake, mwaka 2004 kimeanza kutumika katika mikutano rasmi ya Bunge la Afrika pia Bunge la Afrika Mashariki, Bunge la SADC na pia Kiswahili kimetangazwa siku adhimu duniani kila mwaka tunakiadhimisha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mabadiliko haya makubwa ya kijamii ya Lugha ya Kiswahili, kiuchumi, kiteknolojia na kisayansi hatuoni kwamba sasa imefika wakati kuwe na sera inayojitosheleza ya Lugha ya Kiswahili, badala ya ile Sera ambayo imeegemea ndani ya Sera ya Utamaduni? (Makofi)
Swali langu la pili ni kwamba, Kiswahili hivi sasa tumekibidhaisha ni mikakati gani ya hivi sasa na baadaye ambayo itatumika kukifanya Kiswahili kuwa ni bidhaa bora yenye viwango kifasaha na kiusanifu? Ahsante. (Makofi)
Name
Hamis Mohamed Mwinjuma
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Muheza
Answer
NAIBU WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza la nyongeza la Mheshimiwa Ameir Abdalla Ameir ni kwamba kweli kulionekana kuna haja ya kuwa na Sera inayojitegemea ya Kiswahili badala ya kukiacha Kiswahili kisimamiwe na Sera Mama ya Utamaduni. Majadiliano yalikuwa yanaendelea hata miongoni mwetu wenyewe, pamoja na kuonekana kwamba Kiswahili kinahitaji kusimamiwa na Sera yake binafsi pia kukaonekana kwamba kuna uwezekano Sera Mama ya Utamaduni itapwaya sana kama Kiswahili kitaondolewa kusimamiwa na Sera hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge majadiliano hayo hayajafa yanaendelea na pengine hivi karibuni tutaoa mwongozo wa namna ambavyo tunataka kulifanya jambo hili na pengine Kiswahili kitapata Sera yake binafsi ya kukisimamia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili kuhusiana na kubidhaisha Kiswahili. Ni kweli baada ya Kiswahili kutangazwa kuwa miongoni mwa lugha za kazi, mahitaji ya vitabu, machapisho na magazeti yameongezeka sana na hivyo wigo wa soko la Waandishi wa Kiswahili umepanuka sana nao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kupitia BAKITA na BAKIZA tunahakikisha ya kwamba Kiswahili kinabidhaishwa kwa kupelekwa sehemu mbalimbali Duniani na hivi navyoongea vipo vituo 43 kwa ajili ya kufundishia Kiswahili Dunia. Vituo 16 kati ya hivyo vikiwa nje ya nchi na 11 vikiwa katika Balozi zetu mbalimbali Duniani kama Ufaransa, Uturuki, Uholanzi, Italia, Korea Kusini, Umoja wa Falme za Kiarabu, Mauritius, Sudan, Nigeria, Cuba na Zimbabwe. Hali kadhalika kwa sasa BAKITA na BAKIZA wameendelea kuadhimisha siku ya Kiswahili Duniani ambayo ni tarehe 07 Julai ya kila mwaka na mwaka jana ilifanyika Zanzibar, pia hiyo ni kutii wito wa UNESCO ambao walipitisha siku hiyo kuwa siku ya Kiswahili Duniani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hivyo nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge ya kwamba tunafanya kila ambalo lipo ndani ya uwezo wetu kuhakikisha Kiswahili kinasambaa zaidi na mikakati tuliyonayo ni kuhakikisha tunakuwa na vituo vingi zaidi vya kufundishia Kiswahili katika nchi mbalimbali Duniani, ahsante.
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved