Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Timotheo Paul Mnzava
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Korogwe Vijijini
Primary Question
MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA aliuliza: - Je, ni lini Serikali itaacha kuwafukuza na kuwavunjia vibanda wajasiriamali wanaofanya biashara barabara kuu ya Segera – Korogwe – Moshi?
Supplementary Question 1
MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru nina maswali mawili ya nyongeza.
Swali la kwanza, vijana waliokuwa wanatekeleza zoezi hili, walilifanya katika namna isiyo ya kistaarabu, namna ya kinyanyasaji na ya kuwaumiza na ya kuwaharibia na ya kuwafilisi katiba wajasiriamali wetu. Nataka nijue kama haya yalikuwa ni maelekezo ya Serikali?
Swali la pili, kwa sababu maeneo yote ambayo yameathirika kuanzia Bwiko – Segera – Hale, yana maeneo ambayo yanafaa kwa shughuli za kibiashara kwa kuzingatia taratibu za kiusalama. Kwa kuwa Mheshimiwa Waziri amesema shida ni vibali na mpangilio, Serikali iko tayari kutoa maelekezo kwa TANROADS Mkoa wa Tanga ili tukae nao waone namna ya kuwapanga vizuri wajasiriamali hawa kwenye barabara ili Watanzania wapate nafasi ya kujipatia riziki na kipato chao? (Makofi)
Name
Eng. Godfrey Msongwe Kasekenya
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Ileje
Answer
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Timotheo Paul Mnzava, Mbunge wa Korogwe Vijijini, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, watumishi wote wa Serikali wanatakiwa kufanya kazi kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu. Kama hilo lilitokea kwa upande wa Korogwe wakati zoezi hilo linafanyika, si maelekezo ya Serikali na halikubaliki kwani Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, imejipambanua kutoa haki na watumishi wa Serikali kuwatumikia wananchi kwa heshima na siyo kwa kuwanyanyasa ama kwa namna nyingine yoyote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kama hilo lilitokea hayakuwa maelekezo ya Serikali. Pengine nitumie nafasi hii kuwaelekeza Mameneja wote na watumishi wote wa Wizara ya Ujenzi, kuhakikisha kwamba wanatoa huduma kwa watumishi kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu pia kwa kuheshimu haki na heshima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili, nikubaliane na Mheshimiwa Mbunge kwamba kama yako maeneo ambayo yanastahili na yanaweza kupewa vibali, basi nimwombe Mheshimiwa Mbunge na nimuagize Meneja wa TANROADS Mkoa wa Tanga, waweze kukutana na Mbunge na wananchi ili waweze kuainisha maeneo ambayo wanadhani yanaweza yakapata vibali ili mradi tu hayataathiri usalama na shughuli za kawaida za kutumia barabara ya TANROADS, ahsante. (Makofi)
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved