Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Nusrat Shaaban Hanje

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. NUSRAT S. HANJE aliuliza: - Je, kuna mpango gani wa kumaliza tatizo la uhaba wa Walimu Shule za Sekondari na za Msingi katika Wilaya ya Ikungi?

Supplementary Question 1

MHE. NUSRAT S. HANJE: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu ya Serikali, Jimbo la Singida Mashariki lina uhaba mkubwa wa walimu hususan walimu wa masomo ya sayansi ambapo mpaka sasa tunapungukiwa walimu 449. Hapo tunajumlisha shule za Munkinya, Choda, Mkiwa, Ikungi, Mungaa, Dung’unyi, zote. Sasa ni kwa nini Serikali isiweke mkakati madhubuti kwa ajili ya kuhakikisha Jimbo la Singida Mashariki linapata walimu wa kutosha kwa sababu ni wilaya ambayo inabeba majimbo mawili?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili. Wilaya ya Ikungi ambayo ina majimbo mawili, imekuwa inatengewa fedha pungufu, sawa na wilaya nyingine ambazo zina jimbo moja, hususan kwenye miradi ya elimu. Ni kwa nini sasa Serikali isione umuhimu wa kuongeza fedha za miradi ya maendeleo katika Wilaya ya Ikungi kwa kuzingatia kwamba ina majimbo mawili na siyo jimbo moja (Singida Mashariki na Singida Magharibi)? Ahsante.

Name

Dr. Festo John Dugange

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wanging'ombe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali imeendelea kufanya jitihada za kupeleka walimu wa masomo ya sayansi, hisabati na masomo mengine katika halmashauri zote ikiwemo Jimbo la Singida Mashariki. Katika ajira zilizopita, kipaumbele kilikuwa walimu wa sayansi na ajira zote ambazo zinafuata, walimu wanaopewa kipaumbele ni wa sayansi kwa sababu tuna upungufu mkubwa katika maeneo mbalimbali kote nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali itaendelea kupeleka walimu wa sayansi wa kutosha kwa awamu ili kupunguza pengo la walimu katika hamashauri hiyo na Jimbo la Singida Mashariki.

Mheshimiwa Naibu Spika, pili, kuhusiana na Halmashauri ya Ikungi kuwa na majimbo mawili na kwamba inapewa fedha sawa na halmashauri zenye jimbo moja, fedha za Serikali zinapelekwa kwa halmashauri. Kigezo ni halmashauri, kwa kuzingatia idadi ya watu, ukubwa kijiografia na mambo mengine. Kwa hiyo, pamoja na kwamba ina majimbo mawili, lakini vigezo vingine vyote vinakwenda in favor kuhakikisha kwamba wananchi wanapata huduma wanazostahili. Ahsante.