Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Issa Jumanne Mtemvu
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kibamba
Primary Question
MHE. ISSA J. MTEMVU aliuliza: - Je, ipi kauli ya Serikali juu ya kutokamilika kwa Miradi ya Maji katika Jimbo la Kibamba?
Supplementary Question 1
MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Kwanza nashukuru kwa majibu mazuri na tuendelee kumpongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kututekelezea miradi hiyo mitatu katika kipindi chake cha miaka mitatu. Pamoja na majibu hayo, naomba niulize maswali ya mawili (a) na (b) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Spika, ukamilishaji wa miradi iliyotamkwa kwenye majibu ya msingi ni ukamilishaji wa matanki au vihifadhia maji, lakini ili mradi ukamilike ni lazima usambazaji wa mabomba kwenda kwa wananchi ukamilike ili thamani ya fedha itimie. Sasa yapo maeneo kama CCM ya zamani Mpijimagohe, Torino kwa Mvungi, kwa Mzee Kadope na maeneo ya kwa Yusuph Michungwani.
Ni lini Serikali itatekeleza ahadi yake ya muda mrefu kupeleka mabomba hapa katika maeneo hayo?
(b) Mheshimiwa Spika, Mtaa wa Msumi hasa Msumi Center na Darajani ni muda mrefu hawajawahi kuyaona maji safi na salama, lakini tayari Serikali imefanya utafiti wake na kutekeleza mradi au ina nia ya kutekeleza mradi wa shilingi bilioni 13.9. Je, ni lini sasa Serikali inatoa commitment kwa wananchi wa Kibamba ya kuanza kutekeleza mradi huo ambao mmeshaufanyia tathmini?
Name
Kundo Andrea Mathew
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bariadi
Answer
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mtemvu, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli kabisa Mheshimiwa Mbunge amekuwa akifuatilia miradi hii kwa niaba ya wananchi wake wa Jimbo la Kibamba na kwa kweli anaendelea kufanya kazi nzuri. Sasa kupitia mradi wa kuboresha huduma za maji katika Mkoa wa Dar es Salaam, Serikali imepenga kiasi cha shilingi bilioni 33 ambapo ndani ya fedha hizo kuna shilingi bilioni 13.9 kwa ajili ya kutekeleza mradi katika maeneo ya Msakuzi, Makobe, Msumi A, B, C, Tegeta, Mpindi na Magohe. Maeneo yote hayo yatakuwa ndani ya mradi huo wa kuboresha huduma ya maji katika Mkoa wa Dar es Salaam.
Mheshimiwa Spika, mradi huu utakapokamilika pamoja na maeneo ya Tegeta, utaweza kunufaisha wakazi takribani 166,548. Kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Mbunge aendelee kuvuta subira katika bajeti hii itakapopitishwa, basi mradi huo utaanza mara moja. Katika maeneo ya usambazaji wa mabomba, yote hayo yapo ndani ya mradi huu wa kuboresha huduma ya maji katika Mkoa wa Dar es Salaam. Nakushukuru sana.
Name
Deodatus Philip Mwanyika
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Njombe Mjini
Primary Question
MHE. ISSA J. MTEMVU aliuliza: - Je, ipi kauli ya Serikali juu ya kutokamilika kwa Miradi ya Maji katika Jimbo la Kibamba?
Supplementary Question 2
MHE. DEODATUS P. MWANYIKA: Mheshimiwa Spika, ahsante, nini kauli ya Serikali kuhusiana na Mradi wa Maji Igongwi wa kupeleka maji kwenye kata tatu ambao umekamilika lakini bado maji hayawafikii walengwa?
Name
Kundo Andrea Mathew
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bariadi
Answer
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mwanyika kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli kabisa mradi huu umeshakamilika, lakini ni katika hatua ya kwanza. Hatua ya pili ni kuhakikisha sasa maji yanawafikia wananchi. Kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Mbunge atupe nafasi kusudi mkandarasi aendelee na hatua ya mwisho ili wananchi wapate maji. Ahsante sana.
Name
Dr. Angeline Sylvester Lubala Mabula
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Ilemela
Primary Question
MHE. ISSA J. MTEMVU aliuliza: - Je, ipi kauli ya Serikali juu ya kutokamilika kwa Miradi ya Maji katika Jimbo la Kibamba?
Supplementary Question 3
MHE. DKT. ANGELINE S. L. MABULA: Mheshimiwa Spika, wananchi waishio katika Visiwa vya Besi na Tefu hawana maji safi na salama kwa maana ya maji ya bomba. Ni lini Serikali itawapelekea maji safi na salama?
Name
Kundo Andrea Mathew
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bariadi
Answer
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Angelina Mabula, Mbunge wa Ilemela, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Kisiwa cha Base ni moja ya visiwa vidogo vidogo ambavyo viko katika Ziwa Victoria, lakini Ofisi ya Bonde la Ziwa Victoria walifanya tathmini na kugundua kwamba hakuna maji ardhini. Tunachokifanya kwa sasa kupitia Mamlaka ya Maji Mwanza, MWAWASA wanaenda kuanzisha mradi mdogo ili waweze kuchakata maji kutoka Ziwa Victoria kwenda katika kisiwa hicho ambacho zaidi kinakaliwa na wavuvi.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Mbunge aendelee kushirikiana na Serikali kuhakikisha katika mwaka huu wa fedha 2024 tutaanza mradi huo na hatimaye wananchi wa kisiwa hicho watapata maji. Ahsante sana. (Makofi)
Name
Neema William Mgaya
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. ISSA J. MTEMVU aliuliza: - Je, ipi kauli ya Serikali juu ya kutokamilika kwa Miradi ya Maji katika Jimbo la Kibamba?
Supplementary Question 4
MHE. NEEMA W. MGAYA: Mheshimiwa Spika, lini Serikali itatatua changamoto ya maji iliyopo ndani ya Wilaya ya Makete kule Mfumbi? Ahsante.
Name
Kundo Andrea Mathew
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bariadi
Answer
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Neema Mgaya, Mbunge wa Njombe, Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, naomba baada ya kikao chako hiki cha Bunge, kwa sababu ni eneo specific ambalo amelitaja, tuweze kuonana ili niweze kujua na kuona kama limetengwa. Kama halijatengwa, basi tuone Serikali tunafanya nini ili kuhakikisha wananchi wa maeneo hayo wananufaika. Ahsante sana.
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved