Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Rashid Abdallah Shangazi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mlalo

Primary Question

MHE. RASHID A. SHANGAZI (K.n.y. MHE. RUTH H. MOLLEL) aliuliza:- Mheshimiwa Rais amepunguza idadi ya Wizara kutoka 23 hadi 18 ili kupunguza gharama za uendeshaji:- Je, ni kiasi gani cha fedha za walipa kodi zilizookolewa kwa kuwa na idadi ndogo ya Wizara.

Supplementary Question 1

MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ambayo yanamhusu Mbunge wa mwendokasi aliyetoka, naomba niulize maswali mawili ya nyongeza. Kwa kuwa Wizara ya Utumishi, imeshindwa kutoa vibali kwa Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto ambayo inatugharimu takribani milioni 28 kuhudumia watumishi 58. Je, ni lini Wizara hii itatoa kibali kwa Halmashari ya Wilaya ya Lushoto?
Swali la pili, kwa kuwa pesa hizi ambazo Halmashauri ya Lushoto inazitumia, kulipa mishahara zilikuwa ziende kwenye makundi maalum hasa ya vijana na akinamama, zile asilimia tano. Je, Wizara haioni kwamba pesa hizi kutumika kulipa watumishi inakinzana na dhana nzima ya utawala bora?

Name

Angellah Jasmine Mbelwa Kairuki

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Nominated

Answer

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kwamba maswali haya naona yametoka nje kabisa na swali hili la msingi. Kuhusiana na lini sasa Ofisi ya Rais, Utumishi itatoa kibali kwa Halmashauri ya Lushoto, kwa ajili ya kibali cha ajira, niseme tu kwamba kwa sasa Serikali bado inaendelea na mchakato na pindi vibali hivyo vitakapokuwa tayari, basi taasisi husika zitaweza kufahamishwa na wataendelea na michakato hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na swali lake la pili, kwamba kutokana na vibali hivi kuchelewa, imepelekea Halmashauri ya Wilaya yake kuweza kutumia mapato yake ya ndani au own source kwa ajili ya kulipa mishahara. Niseme tu kwamba kila mwaka na Halmashauri zote na mamlaka za ajira wanafahamu mchakato wa ajira, kila mwaka mamlaka ya ajira inatakiwa iwasilishe ikama yake.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, tumekuwa tukishuhudia huwa wanawasilisha ikama, ikama inaidhinishwa na baadaye Halmashauri inaenda kinyume kabisa na kuwaajiri watu wake kwa kupitia fedha zao za ndani. Niseme
tu kwamba kwa kweli suala hili limekuwa likileta changamoto na tuombe sana Halmashauri zijikite zaidi katika ikama ambazo zinaidhinishwa na Serikali kwa kutumia mishahara ya Serikali.

Name

Japhet Ngailonga Hasunga (CPA)

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Vwawa

Primary Question

MHE. RASHID A. SHANGAZI (K.n.y. MHE. RUTH H. MOLLEL) aliuliza:- Mheshimiwa Rais amepunguza idadi ya Wizara kutoka 23 hadi 18 ili kupunguza gharama za uendeshaji:- Je, ni kiasi gani cha fedha za walipa kodi zilizookolewa kwa kuwa na idadi ndogo ya Wizara.

Supplementary Question 2

MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kuniona. Ningependa kuuliza swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa kuna taasisi nyingi za Serikali ambazo zinafanya kazi zinazofanana na hii inasababisha kwamba bado gharama ziendelee kubaki kuwa kubwa. Serikali ina mpango gani wa kupitia upya taasisi zake zote ili kuhakikisha kwamba zile zinazofanana zinaunganishwa, kusudi kuweza kupunguza matumizi zaidi?

Name

Angellah Jasmine Mbelwa Kairuki

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Nominated

Answer

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa niseme tu kwamba, kama alisikiliza vizuri jibu langu la msingi, hiyo ndiyo azma na mwelekeo wa Serikali. Hata hivyo, nimpongeze na kumshukuru sana, kwa namna ambavyo amekuwa akifuatilia masuala mazima ya utumishi wa umma.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimhakikishie kwamba tayari Katibu Mkuu Kiongozi, kupitia Ofisi ya Rais, alishatoa maelekezo kwa Wakuu wote wa Taasisi za Umma na tayari Taasisi zote, Wizara zote zimekwishawasilisha mapendekezo katika Ofisi ya Rais, kuhusiana miundo na mgawanyo wa majukumu ambayo wao wangeipendelea.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunachokifanya hivi sasa tayari Ofisi ya Rais tumeishaunda timu ya wataalam na wameanza kupitia ili kuangalia endapo majukumu yaliyopo kwa taasisi fulani fulani, kama yanaweza kuhalalisha uwepo wake. Lakini vile vile kuangalia ni majukumu gani, nitolee tu mfano ziko Wizara unakuta zimeunganishwa Wizara mbili, Wizara moja ilikuwa tayari ina kitengo chake cha mawasiliano, ina kitengo chake cha mambo ya teknohama, lakini na Wizara nyingine vile vile, ilikuwa na kitengo kama hicho na idara zingine zinazofanana na mambo haya.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ni dhahiri kabisa kwamba ni lazima itabidi kufanyia mapitio idara moja tu ndiyo iwepo. Vile vile watumishi hao wengine itabidi waangaliwe sasa ni wapi watapelekwa, katika sehemu zingine ili waweze kuleta tija zaidi na kupunguza gharama kwa Serikali.