Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Josephat Sinkamba Kandege

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kalambo

Primary Question

MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE aliuliza:- Je, kuna utafiti wa kisayansi unaoonyesha kufunga shughuli za uvuvi Ziwa Tanganyika kuruhusu kuzaliana kwa Samaki kutakuwa na tija?

Supplementary Question 1

MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Kwa kuwa kwa kiasi kikubwa upungufu wa samaki unachangiwa na uvuvi haramu: Je, Serikali imejipangaje katika kuhakikisha inapambana na uvuvi huu?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili. Kwa kuwa, mwitikio wa umuhimu wa ufugaji kwa kutumia vizimba katika Ziwa Tanganyika upo chini sana: Je, Serikali ipo tayari kwa kushirikiana na Wabunge wanaotoka ukanda wa Ziwa Tanganyika kutoa elimu kwa wananchi ili waweze kuchangamkia fursa hii?

Name

Alexander Pastory Mnyeti

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Misungwi

Answer

NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naanza na hili swali la kwanza. Ni kweli, uvuvi haramu unachangia kwa kiasi kikubwa sana kupungua kwa samaki katika maziwa yetu, siyo tu Ziwa Tanganyika, bali maziwa yote yanayozunguka nchi yetu. Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi tayari imeshaweka mikakati madhubuti kuhakikisha uvuvi haramu unakwenda kukomeshwa katika maziwa yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mikakati ipo mingi na nisingependa sana kuisema kwa sababu mingi inahusisha masuala ya kiintelijensia. Tayari vijana wetu wa kijeshi wameshaanza kufanya operation katika maeneo mbalimbali kuhakikisha tunadhibiti uvuvi haramu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano mzuri ni kule Bahari ya Hindi. Wale Wabunge wanaotoka katika maeneo hayo, tayari wameona jitihada za Serikali kukomesha uvuvi kwa njia ya mabomu kama ambavyo Serikali imechukuwa hatua stahiki zinazotakiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ni kuhusiana na vizimba. Ni kweli, tumeshaanza kutoa elimu, na elimu haina mwisho, tunaendelea kutoa elimu kupitia wataalamu wetu. Mimi na Mheshimiwa Waziri tayari tumeshafika katika maeneo hayo kuendelea kutoa elimu kwa wavuvi wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tupo tayari kushirikiana na Waheshimiwa Wabunge tunapopata nafasi, siku za weekend tunakwenda kutoa elimu. Hata baada ya Bunge, tupo tayari kushirikiana na Waheshimiwa Wabunge kwenda kutoa elimu kwa wavuvi wetu ili waweze kuelewa namna sahihi ya kuchukua vizimba na boti kwa ajili ya mikopo ya riba nafuu ambayo Wizara imekuwa ikiendelea kuitoa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali ipo tayari kushirikiana na Waheshimiwa Wabunge kuhakikisha tunakwenda kutoa elimu kwa kusaidiana na Serikali, ahsante.

Name

Aida Joseph Khenani

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Nkasi Kaskazini

Primary Question

MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE aliuliza:- Je, kuna utafiti wa kisayansi unaoonyesha kufunga shughuli za uvuvi Ziwa Tanganyika kuruhusu kuzaliana kwa Samaki kutakuwa na tija?

Supplementary Question 2

MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Naibu Waziri anajua kwamba Ziwa Tanganyika sisi tunaotoka maeneo yale ndiyo shamba letu na ndiyo duka letu, hivyo unapopumzisha hilo ziwa kwa miezi mitatu, ningependa kufahamu, Serikali mmetenga kiasi gani kwa ajili ya kuwapatia wavuvi kwa kipindi hicho cha mpito?

Name

Alexander Pastory Mnyeti

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Misungwi

Answer

NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kipindi hiki cha miezi mitatu ni kweli, kama anavyosema Mheshimiwa Mbunge kuwa Ziwa Tanganyika kwa asilimia kubwa wanaozunguka eneo hilo, ndiyo shamba lao. Kwa kutambua hilo, Wizara imekuja na mkakati wa kuwakopesha wavuvi hao vizimba. Vizimba hivi vitasaidia kuongeza uzalishaji ambao umekuwa ukifanyika katika hilo Ziwa Tanganyika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kiukweli wavuvi wa Ziwa Tanganyika wamepokea jambo hili kwa mikono miwili na wapo tayari. Pia tayari tumeshapokea maombi mengi na tarehe 5/5/2024 Mheshimiwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi anakwenda kukabidhi vizimba kwa wale wote walioomba katika eneo la Ziwa Tanganyika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tupo tayari kuendelea kutoa vizimba kwa wale watakaoomba na milango ipo wazi waendelee kuomba. Huu ndiyo utakuwa mbadala pekee wa kuwasaidia wavuvi katika eneo hilo la Ziwa Tanganyika.