Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Jafari Chege Wambura
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Rorya
Primary Question
MHE. JAFARI W. CHEGE aliuliza: - Je, lini Serikali itahamisha Mabaraza ya Ardhi kwenda kwenye Mfumo wa Mahakama?
Supplementary Question 1
MHE. JAFARI W. CHEGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi. Wilaya ya Rorya haina Baraza la Ardhi la Wilaya jambo linalosababisha wananchi kusafiri umbali mrefu zaidi ya kilomita 60 mpaka 100 kwenda Tarime kufuata huduma hii, ambapo kwa umbali huo wakati mwingine wananchi hukata tamaa kushughulikia haki zao za kimsingi na za kisheria za utatuzi wa migogoro ya ardhi. Je, Mheshimiwa Waziri haoni sasa kuna umuhimu wa kuanzishwa Baraza la Ardhi la Wilaya ya Rorya?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili, kumekuwa na minong’ono mingi ya wananchi kuhusu kukithiri kwa vitendo vya rushwa kwenye utatuzi wa migogoro kwenye Mabaraza ya Ardhi ya Wilaya. Nataka kujua mpango mkakati milionao kama Serikali kuhakikisha kwamba vitendo hivi vya rushwa ambavyo vinanyima haki kwa wananchi, Serikali mmejipanga vipi kushughulika navyo ili angalau wananchi waweze kupata haki zao za kimsingi katika maeneo haya? Nashukuru sana. (Makofi)
Name
Jerry William Silaa
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Ukonga
Answer
WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Jafari Wambura Chege, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli nia hasa ya kuanzisha mabaraza haya yalikuja wakati wa ripoti ya Profesa Issa Shivji katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma za kutatua migogoro ya kisheria katika kipindi ambacho Mahakama zilikuwa hazina ufanisi wa kutosha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyojibu kwenye swali langu la msingi, kwa sasa Mahakama zetu zimeboreshwa sana, zina mifumo ya kisasa na zimesambaa nchi nzima na ndiyo nia ya Serikali kuondoa Mabaraza haya kwenye Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kupeleka kwenye Wizara ya Katiba na Sheria chini ya Mhimili wa Mahakama. Katika kufanya hivyo, moja itatatua tatizo ambalo sasa wanalipata wananchi wa Rorya la kusafiri umbali mrefu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiri kwamba kumekuwa na malalamiko mengi hata kwa Waheshimiwa Wabunge humu ndani kuhusu tuhuma za rushwa kwenye Mabaraza haya. Wizara ilishatoa taarifa kwenye Kamati ya Bunge na ninaomba nitoe taarifa mbele ya Bunge lako Tukufu, pale tutakapopata taarifa mahsusi za Baraza ambalo limefanya shauri kwa kutumia maamuzi ambayo yanaonekana yameshawishiwa na rushwa, tutachukua hatua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa nimekubaliana na Mheshimiwa Chege, Wizara inaendelea na taratibu za kuongeza Wenyeviti wa Mabaraza. Mpaka sasa tuna wilaya 36 ambazo zina mabaraza ikiwepo Wilaya ya Rorya, na pale tutakapopata Mwenyekiti wa Baraza, nimwahidi kwamba tutampeleka Mwenyekiti na Baraza litaanzishwa kwenye Wilaya ya Rorya.
Name
Dr. David Mathayo David
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Same Magharibi
Primary Question
MHE. JAFARI W. CHEGE aliuliza: - Je, lini Serikali itahamisha Mabaraza ya Ardhi kwenda kwenye Mfumo wa Mahakama?
Supplementary Question 2
MHE. DKT. DAVID M. DAVID: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. Mwaka huu 2024, Januari Mheshimiwa Waziri wa Ardhi alikuja Same kushughulikia matatizo ya ardhi na mipaka katika Kata za Ruvu, Makanya na Bangalala na alituma wataalam wakaangalia matatizo yalivyo. Je, Mheshimiwa Waziri atarudi lini tena Same kwenye Kata za Bangalala, Makanya na Ruvu ili kushughulikia matatizo hayo?
Name
Jerry William Silaa
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Ukonga
Answer
WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakiri kwamba tarehe 26 Januari, 2024 nilifika Wilaya ya Same kwenye Jimbo la Mheshimiwa Dkt. David Mathayo. Kweli timu imeshakwenda na taarifa wameshaniwasilishia, na ninamwomba subira Mheshimiwa Dkt. David Mathayo, amekuwa akifuatilia kwa karibu sana, na pia nawaomba subira wananchi wa Jimbo la Same Magharibi, pindi nitakapomaliza bajeti yangu mwisho wa mwezi huu, Juni mwanzoni nitaongozana na Mheshimiwa Mathayo, tutaenda kutoa taarifa hiyo kwa wananchi, naomba wawe wavumilivu. (Makofi)
Name
Hawa Subira Mwaifunga
Sex
Male
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. JAFARI W. CHEGE aliuliza: - Je, lini Serikali itahamisha Mabaraza ya Ardhi kwenda kwenye Mfumo wa Mahakama?
Supplementary Question 3
MHE. HAWA S. MWAIFUNGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, mabaraza haya ndiyo yamekuwa chanzo cha kurefusha migogoro ya ardhi nchini. Ni lini sasa mtaleta sheria ili mabaraza haya yaweze kuondolewa na kesi hizi ziweze kuendelea kwenye Mahakama zetu?
Name
Jerry William Silaa
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Ukonga
Answer
WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Hawa Mwaifunga, Mbunge kwamba, ni kweli kuna mlolongo mrefu kama alivyosema Mheshimiwa Chege. Mabaraza hayapo wilaya zote, wapo Wenyeviti wanaolazimika kufanya mabaraza zaidi ya wilaya moja na hii inachelewesha haki kwa wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimthibitishie Mheshimiwa Mbunge kuwa Serikali inamalizia mikakati ya hatua za mwisho za kuhamishia mabaraza haya kwenye mhimili wa Mahakama na pindi itakapokuwa tayari tutaleta sheria Bungeni kwa ajili ya kutekeleza utaratibu huo. (Makofi)
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved