Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Abeid Ighondo Ramadhani
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Singida Kaskazini
Primary Question
MHE. ABEID R. IGHONDO aliuliza:- Je, Serikali ina mkakati gani wa kukomesha mapenzi ya jinsia moja nchini pamoja na ukatili dhidi ya watoto?
Supplementary Question 1
MHE. ABEID R. IGHONDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushuku kwa kunipa fursa ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Kwanza, nashukuru kwa majibu hayo, japo naamini kwamba Mheshimiwa Waziri ama Serikali itakubaliana nami kwamba tatizo hili la mmomonyoko wa maadili nchini ni kubwa kuliko hatua ambazo tunachukua. Sasa naomba kuuliza maswali yafuatayo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza. Je, Serikali inachukua hatua gani za makusudi za kuhakikisha tunachukua hatua dhidi ya watu wanaojihusisha na masuala haya ya mapenzi ya jinsia moja pamoja na mashirika ama watu wanao-support ama wanaosaidia kuenea kwa jambo hili hapa nchini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili. Sasa Serikali ina mpango gani wa kuleta Muswada hapa Bungeni ili tuweze kutunga sheria ya kudhibiti masuala ya mapenzi ya jinsia moja hapa nchini?
Name
Mwanaidi Ali Khamis
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Answer
NAIBU WAZIRI WA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WANAWAKE NA MAKUNDI MAALUM: Mheshimiwa Mwenyekiti, kitendo cha kujihusisha na mapenzi ya jinsia moja ni kosa la jinai kwa Kifungu Na. 154 cha Sheria, na Kanuni za Adhabu Sura ya 16 inatambua mtu yeyote ambaye atapatikana na hatia ya kosa hilo ataadhibiwa kifungo cha miaka 30. Ikithibitika na mtendewa aliridhia kufanyiwa kitendo, basi atahusika na kosa hilo hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili, sheria na kanuni na adhabu zipo. Kinachotakiwa ni kufanyiwa marekebisho. Bunge la Kumi na Mbili, Mkutano wa Kumi na Moja, Kikao cha Sita aliagiza Serikali kushirikiana na Tume ya Sheria kuhakikisha kwamba tunafanya utafiti kwa kushirikiana na Tume ya Sheria ambayo mabadiliko yatakayofanyika yafikishwe katika Bunge lako Tukufu. Tume inaendelea na kazi hiyo, na mara baada ya kumalizika, Muswada huo utaletwa Bungeni ili kujadiliwa na kupitishwa. (Makofi)
Name
Jesca Jonathani Msambatavangu
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Iringa Mjini
Primary Question
MHE. ABEID R. IGHONDO aliuliza:- Je, Serikali ina mkakati gani wa kukomesha mapenzi ya jinsia moja nchini pamoja na ukatili dhidi ya watoto?
Supplementary Question 2
MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kujua, Serikali ina mkakati gani wa kushirikiana na taasisi za kidini na wataalam ili kuwasaidia wale walioathirika na mapenzi ya jinsia moja?
Name
Mwanaidi Ali Khamis
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Answer
NAIBU WAZIRI WA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WANAWAKE NA MAKUNDI MAALUM: Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ya Awamu ya Sita ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ina malezi, makuzi na utamaduni wa Mtanzania. Kwa hiyo, Serikali kwa kushirikiana na vyombo vya dini tunahakikisha kwamba tunatoa elimu ambayo itawasaidia wananchi ili kujikinga na vitendo hivyo vya jinsia moja na kuondoa mmomonyoko wa maadili ili nchi yetu iendelee kuwa salama, ahsante.
Name
Esther Nicholus Matiko
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. ABEID R. IGHONDO aliuliza:- Je, Serikali ina mkakati gani wa kukomesha mapenzi ya jinsia moja nchini pamoja na ukatili dhidi ya watoto?
Supplementary Question 3
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwepo na kukithiri kwa ukatili dhidi ya watoto hasa kubakwa na kulawitiwa, na sababu mojawapo ni watuhumiwa wanapewa dhamana na hivyo kuharibu ushahidi kabisa. Ni kwa nini Serikali isiwanyime watuhumiwa hawa dhamana kama inavyofanya kwa wale wa armed robbery? (Makofi)
Name
Dr. Eliezer Mbuki Feleshi
Sex
Male
Party
Ex-Officio
Constituent
None
Answer
MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana. Bila kuathiri majibu ya maswali yanayoendelea kutolewa na Mheshimiwa Naibu Waziri, napenda kwanza nimpongeze kwa majibu ambayo ameyatoa kwa maswali haya ya mwisho ambayo yamekuwa na mlengo wa ukiukwaji wa sheria ambazo zinahusu morality, yaani ukiukwaji wa haki kwa watu wanaotendewa kwa makosa ya kujamiiana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tulipenda kuomba Bunge hili Tukufu lielewe kwamba makosa yote yanatungwa na yanakuwa ni makosa ya jinai yanapotungwa na Bunge hili. Kama alivyosema Naibu Waziri, baada ya maswali kuwa mengi sana kwenye Bunge hili kuhusiana na nini kifanyike, mwaka 2023 Bunge lilitoa maelekezo kwa Serikali kwamba, ifanye utafiti wa kina kupitia Law Reform Commission, ambapo kazi hii inaendelea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kwa swali la Mheshimiwa Esther Matiko, yote ambayo yanaendelea, yanahusisha jamii yetu na makundi mbalimbali, hivyo, hakuna tofauti yoyote kwa sababu uhalifu wowote unapofanyika, mtoa taarifa anatakiwa atoe taarifa yake kwa mujibu wa Kifungu cha Saba cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, na baada ya taarifa ya jinai kutolewa, basi upelelezi unaanza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la dhamana linashughulikiwa kwa mujibu wa kifungu cha 148 cha Sheria yetu ya Mwenendo wa Mashauri ya Jinai. Inapokuja sasa kwamba kuna mazingira ya kupinga dhamana, mwendesha mashtaka ambaye ndiye anaiwakilisha Jamhuri, anawasilisha pingamizi kwa mujibu wa sheria na linasikilizwa. Wapo wengi ambao hawapewi dhamana kwa sababu ya vitendo walivyovifanya ambavyo viko kinyume na kustahili wao kupewa dhamana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, dhamana ni haki ya Kikatiba na ni haki kwa mujibu wa sheria isipokuwa kwa makosa ambayo Kifungu cha 148(5) imezuia makosa hayo yasidhaminike. Kwa hiyo, kwa makosa yote yanayodhaminika, dhamana hupingwa kuendana na mazingira ambayo nayasema na hulazimika Mahakama yenye dhamana ipewe hoja na ifanye maamuzi. Nashukuru.
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved