Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Eng. Atashasta Justus Nditiye
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Muhambwe
Primary Question
MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE aliuliza:- Mwezi Septemba, 2015 Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli, aliwaahidi wananchi wa Kata za Busonzu, Busagara na Murungu ambao wamepakana na Hifadhi ya Taifa ya Muyowosi kwamba mpaka kati ya wananchi hao na hifadhi hiyo, utarekebishwa ili wananchi wapate eneo kwa ajili ya kilimo. Je, utekelezaji wa ahadi hiyo utaanza lini?
Supplementary Question 1
MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru, pamoja na majibu mazuri ya Serikali, nina maswali mawili ya nyongeza.
Kwa miaka mingi sana hadi mwaka jana mwanzoni, wananchi waliruhusiwa kufanya shughuli za uvuvi ndani ya hifadhi pamoja na ufugaji nyuki. Lakini toka mwaka jana mwanzoni Serikali ilipiga marufuku na wananchi wakiingia kule wananyanyaswa sana ikiwa ni pamoja na kupigwa na wafanyakazi wa Idara ya Wanyamapori na Wahifadhi.
Je, ni lini Serikali itaruhusu wananchi, waendelee kufanya shughuli za uvuvi na ufugaji nyuki, kwa kuwa kwa kufanya hivyo, itajenga mahusiano mazuri kati ya Serikali na wananchi?
Swali la pili, sehemu kubwa ya hifadhi hiyo ya Moyowosi haina alama kwenye mipaka yake na kwa kuwa wananchi wanakuwa wakinyanyaswa sana kwa ajili ya kufanya shughuli zao ambazo walikuwa wamekwisharuhusiwa na Serikali, ni lini sasa Serikali itakuwa tayari kuweka alama hizo za mipaka? Ahsante.
Name
Eng. Ramo Matala Makani
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Tunduru Kaskazini
Answer
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza wakati Serikali imetoa ruhusa ya kufanya shughuli zile za uvuvi na ufugaji nyuki, ruhusa ile ilizingatia masharti ya kitaalam kwamba shughuli hizi za kibinadamu kwa kiwango hicho ambacho kiliruhusiwa kilikuwa hakiathiri shughuli za uhifadhi katika eneo linalohusika na kwamba utaratibu huo, utaendelea kutumika pale itakapoonekana kwamba kuna umuhimu wa kufanya hivyo kwa ushauri wa wataalam.
Hivyo basi, ningeweza kusema kwamba tutakwenda kuangalia eneo hili specifically sasa hivi, mahsusi lakini kwa kuwa nimeishatangulia kusema kwamba Serikali tayari inao mpango wa kushughulikia masuala haya kimkakati zaidi, basi nimuombe Mheshimiwa Mbunge avute subira kidogo, twende tukayaangalie yote hayo kwa pamoja.
Mheshimiwa Naibu Spika, sehemu ya pili ya swali lake, kuhusiana na kwamba eneo kubwa au sehemu kubwa haina alama, hii ni mojawapo ya changamoto ambayo inasumbua masuala ya uhifadhi kwenye maeneo yetu kwamba maeneo mengi alama zake ziko kwenye kumbukumbu za kitaalam, unazungumzia coordinates kwa mfano. Coordinates kwa mtumiaji wa kawaida mwanakijiji ambaye anapakana na eneo hilo si alama ya kutosha kuweza kumfanya mwananchi huyo aweze kutii Sheria vizuri zaidi.
Kwa hiyo, tunaposema tunakwenda kushughulikia kimkakati zaidi, ni pamoja na kwenda kuweka alama za kudumu lakini zinazoonekana vile vile. Lakini pia zitakazoshirikisha wananchi wanaoishi au jamii zinazoishi kwenye maeneo hayo, ili tukubaliane kwamba kuanzia hapo sasa huo ndio mpaka, na mpaka huo utakuwa unaonekana vizuri, na kila mmoja atalazimika kuuheshimu.
Name
Halima Abdallah Bulembo
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE aliuliza:- Mwezi Septemba, 2015 Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli, aliwaahidi wananchi wa Kata za Busonzu, Busagara na Murungu ambao wamepakana na Hifadhi ya Taifa ya Muyowosi kwamba mpaka kati ya wananchi hao na hifadhi hiyo, utarekebishwa ili wananchi wapate eneo kwa ajili ya kilimo. Je, utekelezaji wa ahadi hiyo utaanza lini?
Supplementary Question 2
MHE. HALIMA A. BULEMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii. Tumekuwa tukiona mapori mengi ya hifadhi yakiingiliana na makazi ya watu katika jamii na mapori hayo yamekuwa yametengwa kwa muda mrefu sana.
Je, Serikali haioni umuhimu wa kugawa mapori haya ya hifadhi yaliyotengwa kwa muda mrefu kwa wananchi, ili waweze kufanya shughuli za kijamii kama kilimo, na mifugo na hii itaweza kuwaondolea adha ya migogoro ya wafugaji na wakulima?
Name
Eng. Ramo Matala Makani
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Tunduru Kaskazini
Answer
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza Serikali inayo taarifa na inatambua kwamba iko kiu kubwa ya wananchi wanaoishi kwenye maeneo yanayopakana na hifadhi kwamba pengine wangechukua maeneo yale ili waweze kuyatumia katika shughuli zingine za kibinadamu, ikiwemo kilimo, ufugaji, pamoja na shughuli zingine. Lakini ni kweli pia sisi sote ni wananchi na nchi ni moja na kwamba sababu za kuifadhi maeneo hayo zilizingatia pia uhitaji wa mahitaji yetu ambayo ni ya kudumu ya muda mrefu zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu utaratibu ule, wa kuweza kuyatwaa maeneo haya na kuyatumia kama Hifadhi, yalikuwa ni maamuzi yetu sisi sote pamoja, kama nilivyojibu kwenye swali la msingi, tulishirikisha Vijiji, Wilaya pamoja na Mikoa ili kuweza kukubaliana kwamba maeneo hayo yahifadhiwe kwa sababu ambazo zina maslahi mapana zaidi, si kwa Taifa tu, lakini pia hata kwa wananchi ambao ni wa nchi nzima na sio wale wanaoishi kwenye maeneo yale tu pale walipo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, narejea tena kusema kwamba kwa sababu umepita muda mrefu tangu maeneo hayo yalipotwaliwa kuwa kama hifadhi, pengine mazingira yamebadilika, pengine kuna sababu ambazo zinaweza zikaonekana kwamba zina uzito zaidi hivi sasa, ndio maana nimesema Serikali inakwenda kulishughulikia suala hili kimkakati, itakuwa ni pamoja na kushirikisha wananchi upya, wote twende tukaangalie na tupime kwamba je, sasa tuseme nchi hii isiwe na hifadhi kabisa? Maeneo yote tutwae kwa ajili ya shughuli zingine za kibinadamu? Pengine hiyo itakuwa ni upande mmoja haiwezekani.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia tukisema kwamba kinyume chake kwamba maeneo yale ya hifadhi yote yabaki kama yalivyo, pengine kuna maeneo tunatakiwa kufanya marekebisho kidogo. Sasa tukatae kwa sababu kuna Sheria, hata kama kuna ukweli kwamba kwa sasa hivi kuna sababu za msingi, pengine na yenyewe itakuwa si sahihi. Ndio maana tunasema kwamba sasa Serikali pamoja na wananchi wanaoishi kwenye maeneo hayo, na pengine wananchi kwa nchi nzima wakitoa maoni tutakwenda kufika mahali sasa tukubaliane kwamba maeneno yapi tunahifadhi, kwa sababu zipi ambazo zitakuwa ni kwa maslahi ya taifa. Niwakumbushe sio kwa maslahi tu ya Taifa, sisi kama nchi tumesaini pia mikataba ya kimataifa, kuhusu masuala ya uhifadhi.
Mheshimiwa Naibu Spika, muda hautoshi ningeweza kusema zaidi lakini napenda kuishia hapa, tunakwenda kufanya zoezi hili kwa pamoja, kutatua kero hizi kwa namna ambayo itakuwa ni endelevu, na ya kudumu.
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved