Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Mohammed Said Issa
Sex
Male
Party
ACT
Constituent
Konde
Primary Question
MHE. MOHAMED SAID ISSA aliuliza:- Je, lini Serikali itakuwa na Hospitali Kuu ya Taifa moja ambayo itatoa huduma zote za afya bila kutegemea hospitali nyingine?
Supplementary Question 1
MHE. MOHAMED SAID ISSA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Serikali imekiri kwamba kuna baadhi ya matibabu ya kibingwa na ubingwa bobezi bado hayapatikani. Je, ni lini Serikali itakamilisha utaratibu wa upatikanaji wa matibabu hayo? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili, kwa kuwa mifumo ya Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na ile ya Jakaya Kikwete haisomani na hivyo kupelekea baadhi ya huduma ambazo zinapatikana upande mmoja haziwezi kwenda upande wa pili. Je, ni lini Serikali itahakikisha mifumo hiyo inasomana ili kuokoa maisha ya wananchi? (Makofi)
Name
Ummy Ally Mwalimu
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Tanga Mjini
Answer
WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa maswali mazuri ya Mheshimiwa Mohamed Said Issa kwamba ni lini sasa tutaanzisha huduma ambazo hazipatikani za ubingwa bobezi. Niseme kwamba tunaendelea kuanzisha huduma mpya kadri zinavyopatikana na utaalam unavyopatikana. Tunawashukuru Wabunge jana waliweza kutupitishia bajeti yetu ndiyo maana unaona sasa kuna huduma mpya ikiwemo za kufanya upasuaji mgumu kwa kutumia roboti, lakini pia na masuala mengine. Kwa hiyo, tutafanya kwa kadri ya upatikanaji wa utaalam na rasilimali fedha.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo kubwa ambalo nataka kusema, sasa hivi karibu huduma zote zote za ubingwa na ubingwa bobezi zinapatikana katika Hospitali yetu ya Taifa Muhimbili, kinachotukwamisha kidogo ni miundombinu na tunataraji kutumia zaidi ya shilingi bilioni 500 kuijenga upya miundombinu ya Hospitali ya Muhimbili.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kuhusu mifumo ya Muhimbili na Jakaya Kikwete kutosomana, ni kweli nakubaliana naye na jambo ambalo jana pia walitupitishia tunaenda kusimika mfumo mpya wa TEHAMA ambapo sasa hospitali zote zitakuwa zinasomana. Siyo tu masuala ya vipimo kati ya Muhimbili na Jakaya Kikwete, lakini hata kama umefanya kipimo Bombo Tanga nimepewa rufaa kuja Muhimbili kipimo changu na majibu yangu ya Bombo Tanga yataonekana Hospitali ya Taifa Muhimbili. (Makofi)
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved