Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Ameir Abdalla Ameir
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
House of Representatives
Primary Question
MHE. AMEIR ABDALLA AMEIR aliuliza: - Je, kwa kiasi gani ushirikiano kati ya TBS na ZBS unaleta matokeo chanya na kusaidia kutatua changamoto za wajasiriamali hususani kutoka Zanzibar?
Supplementary Question 1
MHE. AMEIR ABDALLA AMEIR: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, pamoja na majibu mazuri sana ya Mheshimiwa Waziri kwa ruhusa yako ningeomba kuuliza suala moja la nyongeza lenye kifungu (a) na (b) kama hivi ifuatavyo:-
(a) Kwa kuwa moja kati ya majuku ya msingi sana ya TBS na ZBS ni kulinda usalama wa chakula kwa mlaji. Swali langu ni kwamba je, tathimini ikoje sasa juu ya huu uwepo wa vifaa vyenye teknolojia ya kisasa vyenye uwezo wa kuchambua sampuli kwa uharaka sana wa vyakula vyetu ili kumuhakikishia Mtanzania kwamba anakula chakula chenye usalama na uhakika?
(b) Swali langu la pili ni kwamba je, kuna jitihada gani zozote au viashiria vyovyote vya mafanikio mpaka sasa kwa wafanyabiashara ambao wana-standard mark ya ZBS kuweza kupata soko la biashara zao kikanda na Kimataifa? Ahsante. (Makofi)
Name
Exaud Silaoneka Kigahe
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mufindi Kaskazini
Answer
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na kwanza na mimi nichukue nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Mbunge Mheshimiwa Ameir kwa kufuatilia sana kuhusiana na mashirikiano na ubora wa bidhaa kati ya Tanzania Bara na Zanzibar.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikuhakikishie wewe, lakini na Bunge lako Tukufu kwamba Tanzania imekuwa kati ya nchi ambazo zina maabara ya kisasa sana ya kupima ubora na viwango kwa ajili ya usalama katika chakula na bidhaa nyingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa taarifa yako tu wakati Kamati yako ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji na Mitaji ya Umma ilipotembelea TBS ilijionea dhahiri maabara ya kisasa katika jengo ambalo tumejenga kwa zaidi ya shilingi bilioni 20 na maabara ya kisasa ya zaidi ya shilingi bilioni 500 ambazo hizi zinatumika kupima ubora kwa ajili ya kuhakikisha bidhaa na hasa chakula zinakuwa na usalama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tuna teknolojia za kisasa na vifaa vya kisasa kabisa ambavyo vina hithibati ya Kimataifa vinavyopima ubora kwa ajili ya usalama wa chakula.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la pili kuhusiana na bidhaa zenye ubora ambazo kutokana na ushirikiano wa ZBS na TBS ambazo zinazaliwa kutoka kule Zanzibar, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwanza kwamba sisi kama nchi ni Wajumbe wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afika (SADC) ambapo kule kuna tuzo za Kimataifa kwa maana ya Kanda hiyo SADCAS na katika tuzo hizo za ubora tumekuwa tukishirikisha ZBS na TBS na wajasiriamali na wazalishaji wengi kutoka Zanzibar wamekuwa vinara wa kuonesha bidhaa bora zinazokidhi matakwa na soko la Kimataifa lakini la kikanda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano katika tuzo hizo moja ya kampuni ambazo zimepata tuzo ni Kampuni ya Zanzibar Milling Cooperation kupitia unga wake maarufu sana wanasema special boflo ambao umekuwa ukipata tuzo karibu miaka yote kwenye mashindano hayo. Hata wajasiriamali wadogo wa kawaida kwa mfano Zanzibar Zaidat Product amekuwa pia naye anapata tuzo nyingi za uzalishaji kwa bidhaa zake katika tuzo hizo ambazo zinashirikisha mataifa mengi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba ZBS na TBS wanashirikiana kuhakikisha bidhaa zinazozalishwa Tanzania Bara, lakini na Zanzibar zinakuwa na ubora kwa ajili ya kupata soko la Kimataifa, lakini na ndani ya nchi, nakushukuru.
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved