Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Neema Kichiki Lugangira
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. NEEMA K. LUGANGIRA aliuliza:- Je, nini mkakati wa Serikali katika kupunguza baadhi ya tozo na kufuta zingine ili kuleta unafuu kwa wavuvi?
Supplementary Question 1
MHE. NEEMA K. LUGANGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa majibu ya Serikali. Nikiwa kama Mlezi wa Chama cha Wavuvi, Mkoa wa Kagera natambua fika changamoto mbalimbali za wavuvi kwenye Ziwa Victoria; kwa hiyo nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi sasa kila halmashauri inatoza ushuru tofauti. Nitatoa mfano haraka haraka; Chato kwa kilo moja ya sangara wanatoza shilingi 100, kwa gunia la dagaa wanatoza shilingi 1,000. Sengerema, sangara ni shilingi 100 na gunia la dagaa ni shilingi 1,500. Bukoba Mjini, kilo ya sangara ni shilingi 100 na gunia la dagaa shilingi 2,000. Muleba kilo ya sangara shilingi 300 na dagaa kilo moja shilingi 100. Je, Wizara iko tayari kutoa mwongozo ambao utazielekeza na kuwezesha hizi halmashauri zitoze tozo inayofanana ili kutoendelea kuangamiza wavuvi wetu kwa kutoza tozo tofauti tofauti?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; katika hizi kanuni ambazo Mheshimiwa Naibu Waziri alizisema hapa, Kanuni ya Usafirishaji wa Samaki ya mwaka 2020 imetoa exemption, yaani imetoa msaada wa kodi pale ambapo mvuvi atakuwa anasafirisha chini ya kilo 30 za samaki kama kitoweo. Kwa maana kama chakula, hapaswi kulipa tozo wala hahitaji leseni; lakini hivi sasa halmashauri zinatoza wavuvi tozo pamoja na kudai leseni. Je, Serikali ipo tayari kutoa mwongozo ambao utaelekeza kanuni hizi zifuatwe ipasavyo?
Name
Alexander Pastory Mnyeti
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Misungwi
Answer
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na hili la kwanza, kwamba tozo zinatofautiana katika kila halmashauri. Ukweli ni kwamba kanuni hizi zinapangwa na halmashauri wenyewe. Halmashauri wamepewa mamlaka ya kupanga kanuni na sheria ndogo ambazo zinawaongoza katika halmashauri yao. Kwa hivyo, wao wanaangalia kulingana na mazingira yao, mazingira ya wavuvi wetu, mazingira ya wafanyabiashara wetu wa dagaa, samaki na mazao ya ziwani, wanaangalia namna ambavyo mazingira yao yanawapelekea kupanga kanuni hizo na wanazipeleka Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, kwenda kupitisha kanuni hizo kama zinakubalika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi Wizara tunachofanya ni kutoa mwongozo ili kanuni hizo zisivunje sheria kubwa ambayo ni sheria mama, ni Katiba ya Nchi na sheria inayoongoza masuala ya uvuvi. Kwa hiyo, kama kuna changamoto namhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba, Wizara ya Mifugo itakwenda kukaa na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa ili tuzipitie kanuni hizo. Kama zina changamoto kulingana na mazingira yanayohusika basi tutakwenda kuzirekebisha kadri itakavyowezekana. Ukweli ni kwamba kanuni na sheria ndogo hupangwa na halmashauri husika kwa faida ya halmashauri yenyewe kulingana na makusanyo na mazingira ya wafanyabiashara wao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu hili swali la pili, Wizara iko tayari kufuatilia ili kuona kama kuna mwananchi, mfanyabiashara ama mwananchi yoyote anayebeba kilo 30 na kusumbuliwa. Kwa sababu ukweli ni kwamba kilo 30 ni kwa ajili ya matumizi ya nyumbani. Kama kuna maeneo ambayo halmashauri wanatoza tozo ama wanakatisha ushuru kwa wafanyabiashara wadogo wadogo wa namna hii. Wako wafanyabiashara wenye kilo 30, wanakwenda kufanya biashara hiyo ni ruksa kwa sababu wako chini ya kanuni lakini wako walio na kilo 30 kwa ajili ya matumizi ya nyumbani. Kama kuna maeneo ambayo watu hao wanasumbuliwa, nitoe rai kwa halmashauri, Maafisa Mifugo wote na Maafisa Uvuvi kuacha mara moja kuwatoza faini ama kuwatoza tozo yoyote wananchi wa namna hii kwa sababu wako ndani ya sheria na sheria inawalinda kwamba hii ni kwa ajili ya matumizi ya nyumbani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama kuna taarifa zozote za siri, tuko tayari kuzipokea na kwenda kuzifanyia kazi. Ahsante.
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved