Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Minza Simon Mjika
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. MINZA S. MJIKA aliuliza:- Je, lini Serikali itajenga zahanati katika Kata ya Binza – Maswa?
Supplementary Question 1
MHE. MINZA S. MJIKA: Mheshimiwa Naibu Spika, nina maswali mawili ya nyongeza, kwanza ninapenda kushukuru kwa majibu mazuri ya Serikali. Swali langu la kwanza; Kata ya Binza ina vijiji saba, vile vijiji saba vina idadi ya watu 8,787 hawana kituo cha afya kabisa na wanahangaika sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; wananchi wale wamejitahidi wana kiwanja na wamesomba tripu 30 za mawe. Je, Serikali inawasaidiaje kuhusu kukamilisha? Ahsante. (Makofi)
Name
Dr. Festo John Dugange
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Wanging'ombe
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza ninawapongeza sana wananchi wa Kata ya Binza kwa kuanza kuchangia michango yao kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha afya. Ninaomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, kwamba Serikali imeweka vigezo vya muhimu ili eneo liwe lina sifa ya kuwa na kituo cha afya; moja ni idadi ya wananchi na mbili ni umbali kutoka kituo cha afya cha jirani zaidi. Kwa hiyo, ikiwa kata hii inakidhi hivyo vigezo ninamhakikishia Mheshimiwa Mbunge, nitafuatilia na niweze kuona namna ambayo tutaweka kwenye mpango kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha afya. Ahsante sana.
Name
Omari Mohamed Kigua
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kilindi
Primary Question
MHE. MINZA S. MJIKA aliuliza:- Je, lini Serikali itajenga zahanati katika Kata ya Binza – Maswa?
Supplementary Question 2
MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Naibu Spika, ninashukuru kwa kunipa nafasi. Ninashukuru Serikali ilitoa fedha kujenga Kituo cha Afya cha Mswaki, lakini kwa bahati mbaya ni kwamba fedha zilizotolewa hazijakamilisha kituo hicho. Je, Mheshimiwa Naibu Waziri, uko tayari kutuma watu wako kwenda kuangalia ni kiasi gani kinatakiwa ili kituo cha afya kikamilike? Ahsante sana.
Name
Dr. Festo John Dugange
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Wanging'ombe
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ilitoa fedha kwa awamu mbili; vipo vituo vya afya ambavyo vilipewa shilingi milioni 250; lakini kuna vituo vya afya ambavyo vimepewa milioni 500 kwa ajili ya kukamilisha majengo yaliyoelekezwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ninaomba nitumie nafasi hii nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge Kigua, kwamba ikiwa kituo hicho cha afya kimepewa milioni 500 na majengo yale yana mapungufu hayajakamilika tutakwenda kufanyia tathmini; kwanza kujiridhisha na thamani ya fedha. Pili, kuona kiasi gani cha fedha kinahitajika kwa ajili ya ukamilishaji ili tupate ndani ya mapato ya ndani ya halmashauri au tupate Serikali Kuu kwa ajili ya kuhakikisha kwamba kituo kinakuwa na ukamilifu unaotakiwa.
Name
Prof. Patrick Alois Ndakidemi
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Moshi Vijijini
Primary Question
MHE. MINZA S. MJIKA aliuliza:- Je, lini Serikali itajenga zahanati katika Kata ya Binza – Maswa?
Supplementary Question 3
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Naibu Spika, ninashukuru sana, eneo la Old Moshi lina kata nne na halina kituo cha afya kabisa. Katika vile vituo vya kimkakati kila jimbo nilipendekeza kituo cha afya kijengwe katika Kata ya Old Moshi, Mashariki. Je, ni lini Serikali itatoa pesa kujenga kituo hiki cha kimkakati? (Makofi)
Name
Dr. Festo John Dugange
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Wanging'ombe
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli eneo la Old Moshi ambalo Mheshimiwa Profesa Ndakidemi amekuwa akifuatilia mara kadhaa kuhakikisha kwamba wananchi wanapata kituo cha afya na aliwasilisha katika orodha ya vituo vya afya 214, katika eneo hilo la Old Moshi.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba nimhakikishie kwamba Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan ameshatoa maelekezo ili fedha ipelekwe kwenye kila jimbo kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha afya cha kimkakati na kwa hivyo na sisi tutahakikisha kwamba fedha zikitoka tunapeleka kwenye Kata ya Old Moshi kwa ajili ya ujenzi wa kituo hicho cha afya. (Makofi)
Name
Asia Abdulkarim Halamga
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. MINZA S. MJIKA aliuliza:- Je, lini Serikali itajenga zahanati katika Kata ya Binza – Maswa?
Supplementary Question 4
MHE. ASIA A. HALAMGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Je, ni lini Serikali itaunga mkono jitihada za wananchi wa Kata ya Masqaroda, Wilaya ya Hanang kwa kuwa kwa sasa wana jengo la OPD pekee yake na jengo la mama na mtoto na majengo mengine hamna?
Name
Dr. Festo John Dugange
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Wanging'ombe
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, lengo la Serikali ni kuhakikisha vituo vyote vya afya vinakuwa na miundombinu toshelevu kwa ajili ya kutoa huduma za afya ngazi ya kituo cha afya.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninatumia nafasi hii kuwapongeza wananchi wa Kata ya Masqaroda katika Halmashauri ya Hanang, lakini niwahakikishie tu kwamba ikiwa wameanza kwa ujenzi wa jengo la OPD, Serikali itawaunga mkono kukamilisha majengo mengine ili kile kituo cha afya kiwe na majengo yanayotosha. Ahsante sana. (Makofi)
Name
Luhaga Joelson Mpina
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kisesa
Primary Question
MHE. MINZA S. MJIKA aliuliza:- Je, lini Serikali itajenga zahanati katika Kata ya Binza – Maswa?
Supplementary Question 5
MHE. LUHAGA J. MPINA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, nimerejea Bungeni. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la nyongeza, kwa kuwa tuna vijiji zaidi ya 6,000 hapa Tanzania havina zahanati. Je, Serikali ina mkakati gani wa haraka sana wa kuhakikisha kwamba wananchi hawa wanapata huduma za matibabu kwa kujenga zahanati na kumalizia zahanati ambazo wananchi walishajitolea kwa nguvu kazi? (Makofi)
Name
Dr. Festo John Dugange
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Wanging'ombe
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali hii ina thamini sana huduma za afya kusogezwa karibu na wananchi na ndio maana kupitia mpango wa maendeleo ya Afya ya Msingi tuliainisha maeneo yote ya vijiji na mitaa yenye sifa ya kujenga vituo vya afya. Katika miaka hii mitatu ya fedha tangu mwaka 2021/2022 mpaka sasa Serikali imeshapeleka fedha kwa ajili ya ujenzi wa jumla ya maboma 1,254 ya zahanati nchini kote.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, kwamba tunahakikisha vijiji vyote vyenye sifa ya kupata zahanati vinaendelea kujengewa zahanati, lakini mitaa yote yenye sifa ya kupata zahanati pia inaendelea kujengewa zahanati hizo kwa awamu.