Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Mariamu Nassoro Kisangi

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. MARIAM N. KISANGI K.n.y. MHE. DKT. FAUSTINE E. NDUGULILE aliuliza:- Je, kuna mkakati gani wa Serikali kuongeza wigo wa barabara za lami katika Wilaya ya Kigamboni?

Supplementary Question 1

MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa majibu mazuri. Pamoja na majibu mazuri ninayo maswali miwili ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza. Kwa kuwa, hali ya Barabara za Kigamboni ni mbaya sana, watu wanashindwa kwenda kufanya kazi. Barabara ya kutoka Mji Mwema kwenda Kimbiji Pemba Mnazi haipitiki kabisa. Barabara ya Kibada – Pemba Mnazi mpaka Tundwi Songani haipitiki kabisa, hali ambayo inafanya wananchi wa Kigamboni sasa washindwe kufanya kazi na pia, kupandishiwa nauli za daladala. Je, Serikali ina mpango gani wa muda mfupi kuhakikisha barabara hizo zinakwenda kupitika na watu wanaendelea na shughuli zao?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili. Kwa kuwa, mzunguko wa lami wa barabara za Kigamboni ni mdogo sana ukizingatia sasa Kigamboni ni eneo ambalo lina viwanda na ni eneo ambalo linakua kiuchumi, je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha wanajenga barabara mpaka kufika kwenye viwanda hivyo, ili wawekezaji wetu waweze kufanya kazi zao vizuri sana? Ahsante.

Name

Zainab Athuman Katimba

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwanza nampongeza Mheshimiwa Mbunge kwa kuuliza maswali yenye tija sana. Naomba nimhakikishie kwamba, Serikali inatambua umuhimu mkubwa sana wa miundombinu ya barabara hizi za TARURA. Natumia nafasi hii kumwagiza Meneja wa TARURA wa Wilaya aweze kwenda kufanya tathmini kuona anachosema Mheshimiwa Mbunge kwa sababu, kama barabara hizi hazipitiki, kipaumbele cha Serikali ni kuhakikisha inarudisha mawasiliano sehemu ambazo hamna mawasiliano.

Kwa hiyo, naomba nitumie nafasi hii kumwagiza Meneja aweze kwenda kufanya tathmini ya barabara alizozitaja Mheshimiwa Mbunge kwenye eneo la Mji Mwema, Kibada na Pemba Mnazi ili kuona hali ilivyo na hatua za dharura ziweze kuchukuliwa kuleta mawasiliano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali lake la pili, namhakikishia Mheshimiwa Mbunge ukiacha kwamba, Serikali inatenga fedha katika bajeti ya TARURA, lakini nakuhakikishia kwamba, kupitia Mradi wa DMDP ambao ni mradi utakaojenga barabara zenye urefu wa kilometa 250 Jimbo la Kigamboni na lenyewe litakuwa ni mnufaika mkubwa sana wa mradi huu. Kwa hiyo, ukiacha tu ujenzi ambao utafanyika kupitia TARURA, pia huu Mradi wa DMDP ambao unagharimu US Dollar milioni 438 utaleta tija kubwa sana katika miundombinu ya Jimbo la Kigamboni.