Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Rehema Juma Migilla
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Ulyankulu
Primary Question
MHE. REHEMA J. MIGILLA aliuliza:- Je, Serikali ina mpango gani wa kuwasaidia watoto kupata matibabu baada ya kufuta Toto Afya Kadi huku tukisubiri Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote?
Supplementary Question 1
MHE. REHEMA J. MIGILLA: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Serikali nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; kwa kuwa mfumo wa bima ya afya kwa wote haujaanza kutumika na watoto wetu wanaendelea kuugua. Je, Serikali kwa sasa kwa nini isione kuna haja ya kuendelea kulipia ile shilingi 50,400 kwa watoto wetu ambao wapo chini ya miaka 18 ambao walikuwa wanajisajili kule bima? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tunafahamu kabisa wazazi wengi hawana uwezo wa kulipia bima hiyo ya najali na wekeza, lakini wana uwezo wa kulipia hiyo shilingi 50,000 au kuongeza kiwango kidogo kwa ajili ya matibabu ya watoto wao. Je, kwa nini Serikali haioni sasa…
SPIKA: Umeshauliza hilo swali la kwanza. Hilo sasa unarejea linakuwa la pili. Sasa nenda kwenye la pili usirejee la kwanza ulilouliza. (Makofi/Kicheko)
MHE. REHEMA J. MIGILLA: Mheshimiwa Spika, swali langu la pili; tunafahamu kabisa Sera ya Afya inasema watoto chini ya miaka mitano wanatibiwa bure, sasa hivi wazazi wengi wamekuwa watoto wao wakiugua chini ya miaka mitano anabeba mtoto wake mgongoni na kumpeleka hospitali yoyote ambayo ipo karibu na yeye.
Mheshimiwa Spika, wakifika kule anakuwa hana hata barua ya rufaa kwenye hiyo hospitali na akifika pale mtoto hatibiwi mpaka awe na barua ya rufaa. Je, hawa wahudumu wetu wa afya wanamwona kabisa mtoto yupo chini ya miaka mitano, lakini hawamtibu eti mpaka awe na barua ya rufaa hatuoni kama tuna mpango watoto wetu wafe? (Makofi)
Name
Dr. Godwin Oloyce Mollel
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Siha
Answer
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Spika, kwanza, nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa maswali yake mazuri. Moja, kwanza atambue imeshakuwa ni zaidi ya miaka 18 ni watoto kuanzia miaka 21 kurudi chini ndio waliokuwepo kwenye huo utaratibu. Pia, ajue tu Mheshimiwa Mbunge, kwenye nchi hii ukipiga hesabu miaka 21 mpaka kurudi chini sifuri wapo kama watoto 30,700,000.
Mheshimiwa Spika, wale waliopo kwenye Toto Afya Kadi walikuwa 200,000 tu maana yake unaweza kuona kwamba, pamoja tunazungumzia hawa 200,000 waliokuwepo kwenye Toto Afya Kadi, lakini kuna watoto zaidi ya 30,700,000 wapo ambao wamekuwa wakiendelea na wakipata huduma kama kawaida.
Mheshimiwa Spika, nimwambie tu Mheshimiwa Mbunge kufanya kwamba, sasa huu mpango mpya haujaondoa shilingi 50,400 bado ni shilingi 50,400. Kilichobadilika sasa wanaingia kwa makundi ili tuweze kutimiza zile taratibu na sheria ambazo zinatakiwa kwenye bima ya afya ili kuulinda mfuko. Kwa sababu kama ambavyo tumeshasema hapa Bungeni walikuwa wanachangia shilingi bilioni tano wanatumia shilingi bilioni 49 maana yake walikuwa wanatumia hela za watumishi wa umma, wanatumia hela za watu wengine ambao walishachangia. Mwisho wa siku, tunaweza tukawatibu tukajikuta tunakosa kusaidia wengine; hilo ni moja.
Mheshimiwa Spika, jambo la pili, nikwambie tu Mheshimiwa Mbunge, kwamba, kupitia taratibu nyingine na njia nyingine ambao hawa 30,000,000 wanapata huduma na hawapigi kelele pamoja na hiyo ya Toto Afya Kadi ambayo ni mpya. Nataka kumhakikishia Mbunge kwamba, Serikali itaendelea kutoa huduma na hao watoto hawatapata shida. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali lake la pili ni kwamba, kuna watoto chini ya miaka mitano. Ni kweli kumekuwepo na shida sehemu mbalimbali kuhusu watoto chini ya miaka mitano. Ni kweli hiyo huduma inatakiwa iwepo bure, lakini hatujaweza kutoa kwa 100%, lakini zaidi ya 70% wamekuwa wakisaidiwa. Bado kuna asilimia fulani ambayo haijaweza kupata hiyo bure kama inavyosema.
Mheshimiwa Spika, kumekuwa na shida kama unavyosema mtoto ambaye anaumwa tu kifua na kikozi tu, lakini unashangaa ameshapelekwa mpaka hospitali ya mkoa. Mara nyingi wataalamu wetu wanapenda kusisitiza waanze huku chini, kwa sababu kuna magonjwa mengine yanaweza yakatibiwa kwenye zahanati na vituo vya afya hakuna sababu ya kwenda kwenye hospitali za mikoa.
Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii kuwaambia waganga wetu wafawidhi wa Hospitali za Wilaya, Hospitali za Mikoa na hospitali nyingine watoto wanaotoka kwenye maeneo yaliyozunguka hospitali zetu wapokelewe na wahudumiwa kulingana na miongozo na taratibu za Serikali zinavyotaka. (Makofi)
SPIKA: Mheshimiwa Naibu Waziri, hao 30,000,000 ni watoto wa chini ya miaka mitano au 30,000,000 wanaohudumiwa na hospitali? Washa kisemeo.
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Spika, nachosema ni kwamba, ukienda kwenye Sensa yetu ukiiangalia, watu chini ya miaka 21 kurudi chini utaona …
SPIKA: Ndio wapo 30,000,000 na siyo hawa wadogo wa chini ya miaka mitano?
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Spika, ndiyo. Siyo hawa chini ya miaka mitano.
SPIKA: Haya. Ahsante sana, umeeleweka.
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Spika, ndio waliotakiwa kupata Toto Afya Kadi, lakini wamekuwa wakihudumiwa tu vizuri, kwa sababu waliopo kwenye Toto Afya Kadi ni 200,000 tu lakini hawa ndio 200,000 wanapigiwa kelele zaidi ya hawa 30,000,000 ambao wanahudumiwa vizuri na Serikali.
Copyright © Bunge Polis 2024. All Rights Reserved