Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Florent Laurent Kyombo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nkenge

Primary Question

MHE. FLORENT L. KYOMBO aliuliza:- Je, lini Bajeti ya Barabara za Wilaya ya Missenyi zenye Mtandao wa Kilometa 921 itaongezwa ili barabara hizo zitengenezwe kwa ubora?

Supplementary Question 1

MHE. FLORENT L. KYOMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru kwa majibu ya Serikali, lakini ninaipongeza Serikali. Ni kweli awali Wilaya ya Missenyi ilikuwa inapata bajeti ya shilingi milioni 700 na leo tunapata shilingi bilioni 2.4. Pamoja na hayo ninayo maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, pamoja na bajeti hiyo kuongezeka lakini bado mtandao wa barabara ambao unatekelezwa kila mwaka ni kilometa 145 ambao ni sawa na 15% ya mtandao mzima ndani ya Wilaya ya Missenyi wa kilometa 921. Je, sasa Serikali haioni kwamba hiyo asilimia ni ndogo sasa, ni muda muafaka wa kutuongezea bajeti ili angalau kiwango cha asilimia ya utekelezaji wa bajeti kila mwaka iweze kutekelezwa?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; Wilaya ya Missenyi ni Wilaya ambayo inapata mvua katika kipindi cha mwaka 75% na iko katika Uwanda wa Chini ambao unakusanya maji mengi kutoka maeneo mbalimbali na hivyo barabara ndani ya Wilaya ya Missenyi kuhitaji kuinuliwa na hiyo inahitaji gharama kubwa sana. Je, hiyo siyo sababu Serikali ione haja ya kuongeza bajeti ndani ya Wilaya ya Missenyi ili barabara zitengenezwe na kuweza kupitika kwa kipindi cha mwaka mzima? Ahsante.

Name

Zainab Athuman Katimba

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwanza kwa kumpongeza Mheshimiwa Mbunge, amekuwa akifanya kazi kubwa sana ya kuwasemea wananchi wake na katika muktadha huu kuwasemea katika kuhakikisha wanapata miundombinu iliyo bora ya barabara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kama nilivyojibu kwenye swali la msingi kwamba, Serikali imekuwa ikiongeza bajeti kila mwaka. Kama nilivyosema mwaka 2020/2021 kulikuwa na bajeti ya shilingi milioni 700 lakini tunavyozungumza mwaka huu 2023/2024 tuna bajeti ya shilingi bilioni 2.4.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, kuna ongezeko pia la urefu wa barabara ambazo zimejengwa katika kipindi hicho kutokea kipindi cha mwaka 2020/2021 ambapo kulikuwa na kilometa 35.5 tu za barabara hizi za lami. Tunavyozungumza mwaka huu, 2023/2024 tumefikia kilometa 146. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, Serikali itaendelea kuhakikisha inatenga fedha kila mwaka kuboresha miundombinu ya barabara katika Wilaya ya Missenyi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali la pili la Mheshimiwa Mbunge, ni kweli Wilaya ya Missenyi inatuamisha maji. Miundombinu mingi inatuamisha maji na ni kutokana na jiografia ya Wilaya hii. Kutokea kipindi cha mwaka 2021/2022, Serikali imekuwa ikitoa fedha kwa ajili ya kuinua vipande tofauti tofauti vya barabara na hasa vile ambavyo ni korofi ili kuondoa maji kutuama. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2021/2022, kipande cha kilometa 2.4, Barabara ya Mabuye – Itara kilinyanyuliwa kwa jumla ya shilingi milioni 298. Mwaka 2022/2023 kilometa 3.2 zilinyanyuliwa katika kipande cha Barabara cha Mabuye – Itara kwa jumla ya shilingi milioni 205, lakini mwaka 2023/2024, kuna kipande cha kilometa nane cha Byeju – Nkerenge ambacho kimetumia shilingi milioni 170 kimenyanyuliwa lakini kwa wakati huu bado Serikali inaendelea kunyanyua kipande cha Kagera Sugar – Bubare, barabara hiyo, cha kilometa 8.5 kwa jumla ya shilingi milioni 160. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, Serikali itaendelea kutenga fedha kuhakikisha kwamba inaondoa changamoto hizi za kutuama maji kwenye barabara katika wilaya yako Mheshimiwa Mbunge. (Makofi)

Name

Dr. John Danielson Pallangyo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Arumeru-Mashariki

Primary Question

MHE. FLORENT L. KYOMBO aliuliza:- Je, lini Bajeti ya Barabara za Wilaya ya Missenyi zenye Mtandao wa Kilometa 921 itaongezwa ili barabara hizo zitengenezwe kwa ubora?

Supplementary Question 2

MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana kwa kunipa hii nafasi. Changamoto ya ufinyu wa bajeti kwenye ujenzi wa barabara kule Missenyi inafanana sana na hali ilivyo kule Arumeru Mashariki ambako tuna mtandao wa barabara wa kilometa 800. Pia, hali ya kijiografia ni ngumu kiasi kwamba fedha ambazo zinapatikana inakuwa ni shida, hazitoshelezi kujenga zile barabara. Je, Serikali ina mpango gani wa kuongeza hiyo bajeti ili iweze kufanya barabara zitengenezeke? Ahsante sana. (Makofi)

Name

Zainab Athuman Katimba

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua kwamba miundombinu ya Barabara, lakini jiografia ya eneo la Arumeru Mahsariki ni ya milimani. Kumekuwa na changamoto pia katika miundombinu na Mheshimiwa Mbunge tumekuwa tukizungumza naye mara kwa mara kuhusiana na barabara zake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, dhamira ya Serikali ni kuhakikisha kwamba inajenga barabara hizi za wilaya ziwe katika hali ambayo inapitika mwaka mzima. Nikuhakikishie, Serikali itaendelea kutenga fedha kuhakikisha kwamba inajenga na kuhudumia barabara zilizoko katika Jimbo lako la Arumeru Mashariki. (Makofi)

Name

Jackson Gedion Kiswaga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kalenga

Primary Question

MHE. FLORENT L. KYOMBO aliuliza:- Je, lini Bajeti ya Barabara za Wilaya ya Missenyi zenye Mtandao wa Kilometa 921 itaongezwa ili barabara hizo zitengenezwe kwa ubora?

Supplementary Question 3

MHE. JACKSON G. KISWAGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Weekend hii nimekuwa jimboni na nikapita katika daraja moja ambalo lilijengwa na TARURA na bahati mbaya nikaona limekatika sana katika Kijiji cha Nyamihuu. Je, Serikali ina mpango gani sasa wa kutuongezea bajeti ili sasa turekebishe madaraja yote yaliyokatika katika Jimbo la Kalenga? (Makofi)

Name

Zainab Athuman Katimba

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua kwamba, kutokana na mvua nyingi ambazo zimekuwa zikinyesha nchini, miundombinu ya barabara imepata athari. Mheshimiwa Mbunge amezungumza kuhusiana na suala la daraja hili la Nyamihuu katika Jimbo lake la Kalenga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie kwamba, kipaumbele cha Serikali kwa wakati huu ni kuhakikisha Serikali inarudisha mawasiliano kwenye maeneo yote ambayo mawasiliano yamekatika na inafanya hivyo kwa udharura. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, baada ya kipindi hiki cha maswali na majibu, mimi na yeye tutazungumza tuone kama daraja hili lipo katika kiwango hicho na linahitaji udharura, basi kuna kila haja ya Serikali kuweka nguvu kuhakikisha inaenda kurekebisha daraja hilo na miundombinu mingine ambayo inakata mawasiliano kwa sababu, lengo la Serikali ni kuhakikisha maeneo yote ambayo mawasiliano yamekatika Serikali inarudisha mawasiliano. (Makofi)