Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Dr. Florence George Samizi
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Muhambwe
Primary Question
MHE. DKT. FLORENCE G. SAMIZI aliuliza:- Je, ni lini Serikali itatekeleza ahadi ya ujenzi wa Barabara ya Kibondo Mjini yenye urefu wa Kilometa sita kwa kiwango cha lami kama ilivyotolewa na Rais wa Awamu ya Tano?
Supplementary Question 1
MHE. DKT. FLORENCE G. SAMIZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ninaishukuru Serikali kwa majibu mazuri, hata hivyo ninayo maswali ya nyongeza. Swali la kwanza; Jimbo la Muhambwe lina mtandao wa barabara wa kilometa 636 na kati ya hizo 636, ni hizo kilometa tano tu za Kibondo Mjini ndiyo ambazo zina lami na lami hiyo tuliitekeleza kwa pesa za kutoka kwenye Bodi ya Mfuko wa Maendeleo ambazo kwa bajeti hii ya 2024/2025, pesa hizo tumeondolewa hazitakuwepo. Je, Serikali haioni sasa iko sababu ya kuturudishia hizi shilingi milioni 800 kutoka kwenye Bodi ya Mfuko wa Maendeleo ya Barabara ili tuweze kuendeleza kujenga barabara za lami Kibondo Mjini? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; mvua zilizoendelea hapo awali hapa nchini nazo zimeathiri sana barabara za Jimbo la Muhambwe hususan Barabara ya Lukaya – Kigina ambayo haipitiki kabisa na Kata ya Rugongwe ndiyo kata inayoongoza kwa mazao. Pia, barabara ya Kibondo kwenda Murungu, daraja la Nyavyumbu limekatika kabisa. Je, ni lini Serikali itatuletea pesa za dharura ili tuweze kutengeneza hizi barabara zilizokatika angalau wananchi waweze kupita mahali hapo ili kupunguza athari? Ahsante. (Makofi)
Name
Zainab Athuman Katimba
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwanza kwa kumpongeza Mheshimiwa Mbunge, Dkt. Florence Samizi kwa kazi kubwa anayoifanya ya kuwatetea wananchi wake wa jimboni kwake. Mheshimiwa Mbunge, ninaomba nikuhakikishie kwamba, Serikali inatambua umuhimu mkubwa sana wa kuboresha miundombinu ya barabara katika jimbo lako. Ndiyo maana katika mwaka wa bajeti 2023/2024, Serikali ilitenga jumla ya shilingi bilioni 4.4 kwa ajili ya ujenzi na matengenezo ya barabara katika jimbo lako.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Mwaka wa Fedha 2024/2025, Serikali imetenga jumla ya shilingi bilioni 3.3 kwa ajili ya ujenzi na matengenezo ya barabara, jumla ya kilometa 110, lakini ujenzi wa makalavati 32. Kwa hiyo, lengo la Serikali ni kuhakikisha kwamba inaboresha miundombinu ya barabara katika Wilaya ya Kibondo na nikuhakikishie, Serikali itaendelea kutenga fedha kuhakikisha inaboresha miundombinu ya barabara hizi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali la pili la Mheshimiwa Mbunge, Mheshimiwa Mbunge amezungumza kuhusiana na fedha za dharura na kukatika kwa mawasiliano katika Barabara ya Lukaya – Kigina. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, Serikali imeshatoa jumla ya shilingi milioni 105 kwa ajili ya kufanya jitihada za kidharura katika jimbo lako hili. Fedha hizo zinaenda kujenga box culverts lakini inaenda kufanya matengenezo katika maeneo yale ambayo yamepata athari kubwa ya mawasiliano, athari kubwa ya mvua, lakini pia kurejesha mawasiliano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie pia Mheshimiwa Mbunge, katika Mwaka wa Fedha 2024/2025, Serikali imetenga jumla ya shilingi milioni 11 kwa ajili ya kuendelea kufanya matengenezo katika sehemu korofi za barabara hiyo. Mheshimiwa Mbunge, kwa ujumla wake, lengo la Serikali ni kuhakikisha kwamba inaboresha miundombinu katika barabara zetu hizi za wilaya. Serikali itaendelea kuhakikisha inatafuta, inatenga na kuleta fedha kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya barabara hizi ikiwemo katika jimbo la Mheshimiwa Mbunge. (Makofi)
Name
Stanslaus Shing'oma Mabula
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Nyamagana
Primary Question
MHE. DKT. FLORENCE G. SAMIZI aliuliza:- Je, ni lini Serikali itatekeleza ahadi ya ujenzi wa Barabara ya Kibondo Mjini yenye urefu wa Kilometa sita kwa kiwango cha lami kama ilivyotolewa na Rais wa Awamu ya Tano?
Supplementary Question 2
MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Barabara ya kutoka Mkuyuni – Igelegele – Mahina – Mandu ni ahadi ya Mheshimiwa Rais toka mwaka 2021. Nimekuwa nikiuliza barabara hii kila leo na leo ni mara ya sita. Mara ya mwisho Mheshimiwa Naibu Waziri alituahidi mvua zitakapokamilika barabara hii itatangazwa na kuanza kujengwa kwa sababu kila hatua imeshakamilika. Je, ni nini kauli ya Serikali juu ya kuhakikisha barabara hii inaanza kujengwa mara moja na kuwapunguzia adha wananchi wa maeneo karibia kata sita za barabara hiyo?
Name
Zainab Athuman Katimba
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli Mheshimiwa Mbunge amekuwa akiiulizia sana hii barabara hapa Bungeni lakini hata huko mtaani tukikutana bado huwa anaulizia mustakabali wa ujenzi wa barabara hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, ahadi za Viongozi Wakuu (ahadi ya Mheshimiwa Rais) aliyoitoa mwaka 2021 ni kipaumbele katika utekelezaji wa mipango ya Serikali na tayari fedha zimeshatengwa kwa ajili ya kuanza kujenga barabara hii. Nikuhakikishie Mheshimiwa Mbunge, kawaambie wananchi wako tunakuja kujenga barabara hii. (Makofi)
Name
Abeid Ighondo Ramadhani
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Singida Kaskazini
Primary Question
MHE. DKT. FLORENCE G. SAMIZI aliuliza:- Je, ni lini Serikali itatekeleza ahadi ya ujenzi wa Barabara ya Kibondo Mjini yenye urefu wa Kilometa sita kwa kiwango cha lami kama ilivyotolewa na Rais wa Awamu ya Tano?
Supplementary Question 3
MHE. ABEID R. IGHONDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana kwa kuniona. Ninataka kujua ni mpango gani sasa wa Serikali kuweka lami katika Barabara inayotoka Singida Mjini – Kinyeto – Merya – Sagara kwa kiwango cha lami ambayo ni ahadi ya Mheshimiwa Rais Marehemu Hayati Dkt. Magufuli, lakini pia ni ahadi ya Mheshimiwa Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan?
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata juzi pia alipopita Katibu Mkuu Dkt. Nchimbi, wananchi walimlilia barabara hii iwekwe lami. Sasa, ni lini sasa Serikali itatekeleza ahadi hii kwa wananchi ambao barabara hii ni ya muhimu sana kiuchumi kwa wananchi wale? Ahsante. (Makofi)
Name
Zainab Athuman Katimba
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua umuhimu wa Barabara hii ya Singida Mjini kuelekea Sagara na hasa katika kuchochea maendeleo na kuchochea uchumi. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kama nilivyosema hapo awali, ahadi za Viongozi Wakuu ni kipaumbele namba moja katika kutekeleza au katika mipango ya utekelezaji wa shughuli za Kiserikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, tutafuatilia barabara hii ili fedha ziweze kuja kwa ajili ya kuijenga kwa kiwango cha lami.
Name
Jeremiah Mrimi Amsabi
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Serengeti
Primary Question
MHE. DKT. FLORENCE G. SAMIZI aliuliza:- Je, ni lini Serikali itatekeleza ahadi ya ujenzi wa Barabara ya Kibondo Mjini yenye urefu wa Kilometa sita kwa kiwango cha lami kama ilivyotolewa na Rais wa Awamu ya Tano?
Supplementary Question 4
MHE. JEREMIAH M. AMSABI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na mvua nyingi zilizonyesha katika Jimbo la Serengeti, Barabara za Bwitengi – Miseke na Mugumu – Machochwe zimeharibika sana. Je, Serikali ina mpango gani wa kufanya marekebisho ya haraka? Ahsante sana.
Name
Zainab Athuman Katimba
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, Serikali inatambua madhara makubwa ambayo yametokea kwenye barabara zetu hizi za wilaya ambayo yamesababishwa na mvua. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, Serikali inatambua na tayari inafanya jitihada kuhakikisha kwamba inarudisha mawasiliano maeneo ambayo mawasiliano yamekatika, lakini inaboresha na kufanya ukarabati wa barabara kwenye maeneo yale ambayo yameharibika na barabara hazipitiki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lengo ni kuhakikisha kwamba barabara hizi, mtandao huu wa barabara za wilaya unakuwa ni mtandao wa barabara ambazo zinapitika mwaka mzima. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, Serikali ipo kazini na tutafanya jitihada zote ili kuhakikisha kwamba tunaboresha miundombinu ya barabara hizi za wilaya.