Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Grace Victor Tendega
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. GRACE V. TENDEGA aliuliza: - Je, ni upi mkakati wa Serikali kuhakikisha maeneo ya majiji na miji yanakuwa safi?
Supplementary Question 1
MHE. GRACE V. TENDEGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa fursa ya kuuliza maswali ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu ya Mheshimiwa Waziri, Serikali imekuwa ikijitoa sana kutengeneza miundombinu bora hasa barabara, masoko na vitu vingine, lakini changamoto kubwa imekuja kwenye kumudu kuzitunza barabara hizo ama kutunza masoko hayo. Kwa mfano ukiangalia Dodoma barabara inayotoka Meriwa kwenda mpaka Ilazo unakuta mifereji ni mizuri na barabara nzuri lakini kuna mchanga mwingi sana.
Mheshimiwa Spika, swali langu la kwanza, pamoja na kutoa elimu yote hiyo, je, Serikali haioni haja sasa waweke mkakati wa kutoa elimu ama kuhamasisha wananchi waweze kufanya usafi bila shuruti? Kwa sababu nchi nyingine kwa mfano Uganda…
SPIKA: Mheshimiwa umeshajieleza.
MHE. GRACE V. TENDEGA: …wanafanya usafi usiku na wanaweza kufanya usafi vizuri.
Mheshimiwa Spika, swali la pili, Mheshimiwa Waziri amesema kwamba wamekuwa wakitoa shilingi bilioni 22.3 hadi shilingi bilioni 10.3 kwa ajili ya usafi. Je, hawaoni haja sasa ya kuhamasisha wananchi waweze kuuza taka kama wanavyofanya nchi nyingine ili waweze kuzi-recycle na kuzifanya zile taka zikawa kama mbolea kwa maeneo mengine na wananchi hawa wanaweza wakawa wamepata ajira kwa sababu hizo fedha wanazozitoatoa zinaweza zikawasaidia na Serikali ikaweza kutoa ajira hasa kwa vijana?
Name
Zainab Athuman Katimba
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Spika, naomba nianze kumpongeza Mheshimiwa Grace Tendega kwa maswali yake mazuri sana. Ofisi ya Rais TAMISEMI pamoja na majukumu mengine chini ya Sheria ya Usimamizi wa Mazingira, imepewa jukumu la msingi la uratibu na kusimamia masuala ya usafi wa mazingira.
Mheshimiwa Spika, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali kupitia miradi mbalimbali imekuwa ikifanya hivyo. Ukiacha tu kuelimisha jamii kwa ujumla wake, lakini kuna mradi maalum ambao upo chini ya TARURA kupitia mradi wa RISE ambao unaitwa CBRM (Community Based Routune Maintainance). Mradi huu ni wa jumla ya dola za Kimarekani 350.
Mheshimiwa Spika, mradi huu unashirikisha vikundi vya kijamii kusafisha na kurekebisha barabara, yaani kuzibua mifereji, kufyeka katika barabara, kufyagia barabara, kuhakikisha kwamba miundombinu yote ya kupokea taka na miundombinu ya barabara kwenye mifereji ile maji yanapopita inaweza kurekebishwa.
Mheshimiwa Spika, hii inakuwa ni namna mojawapo ya kushirikisha jamii katika kutunza mazingira pamoja na jamii husika kupata ajira kwa kutunza mazingira. Huo ni mradi mmoja.
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mbunge ameuliza swali kuhusiana na suala zima la recycling. Serikali inafanya hivyo. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kuwa kuna mradi maalum kabisa wa DMDP II. Mradi huu unakwenda kugusa siyo tu ujenzi wa miundombinu ya barabara, bali ni pamoja na masoko na madampo katika Mkoa wa Dar es Salaam.
Mheshimiwa Spika, katika mradi huu, teknolojia ya kufanya recycling itatumika kwa maana sasa taka zinakuwa ni rasilimali ambayo inaweza ikamletea kipato Mtanzania, kwamba maana auze taka ziweze kuwa recycled na kutengeneza bidhaa nyingine ambazo zinaweza zikawa zina manufaa katika jamii.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, mawanzo ya Mheshimiwa Mbunge ni mazuri sana na yanaendana na mikakati ambayo Serikali tayari inayo ya kuhakikisha kwamba inatunza mazingira; inatunza mazingira ya barabara zetu, mifereji na miundombinu mingine yote, pamoja na kuhakikisha kwamba miji na majiji yetu yanakuwa yana usafi ambao unatakiwa.
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved