Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Constantine John Kanyasu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Geita Mjini

Primary Question

MHE. CONSTANTINE J. KANYASU aliuliza: - Je, Serikali inafahamu ongezeko la magugu maji Ziwa Victoria na zipi athari za Magugu hayo na mpango wa kuyadhibiti?

Supplementary Question 1

MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Spika, kwanza naomba nimpongeze Mheshimiwa Waziri kwa majibu yake mazuri na kukiri ukubwa wa tatizo la magugu maji kwenye Ziwa Victoria. Kwa kuwa ni dhahiri kuwa magugu maji yanaongezeka Ziwa Victoria wala hayapungui, na ni dhahiri kuwa huo mpango mkakati wa 2019/2029 anaouzungumzia ni aidha umeshindwa au haupo, mimi kama Mbunge kwa miaka 10 nimekuwa humu, lakini sijawahi kuona tathmini ya aina yoyote inafanyika juu ya ongezeko la magugu maji. Ni lini Mheshimiwa Waziri atafanya tathmini kuonesha ukubwa wa tatizo wa sasa ulivyo?

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili. Mheshimiwa Naibu Waziri amekiri kwamba athari kubwa ya magugu maji ni kupungua kwa samaki. Sasa hivi kuna uhaba mkubwa wa samaki kutokana na mazalia ya samaki kuendelea kupotea na pia, kuweka zuio la boti kwenye maeneo mbalimbali. Sasa ni njia gani mbadala ya haraka ambayo Serikali inafanya ili kuokoa Ziwa Victoria?

Name

Khamis Hamza Khamis

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Uzini

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Kanyasu, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kama nilivyoeleza katika jibu la msingi kwamba hii ni tathmini na ninataka nimwambie kwamba tathmini hii inaendelea, kwa sababu jambo la uwepo wa viumbe vamizi hasa magugu maji siyo jambo la kusema tunafanya leo, ni jambo ambalo limeenea takribani katika vyanzo vingi vya maji hapa nchini.

Mheshimiwa Spika, hata ukiangalia maeneo ya kule Ziwa Jipe na maeneo mengine, bado changamoto hii ipo. Kwa hiyo, tunamwomba Mheshimiwa aendelee kuwa na subira, bado tunaendelea kufanya tathmini. Kweli, tunakiri kwamba zipo athari kama tulivyoeleza katika jibu la msingi. Tathmini hii itakapokamilika, tutakuja kumweleza yeye na tutalieleza Bunge lako hili ili liweze kujua namna ambavyo tumefikia katika kuhakikisha kwamba tunapambana na changamoto kubwa ya uwepo wa magugu maji.

Mheshimiwa Spika, zipo juhudi kadhaa ambazo tumezichukua kama Serikali ili kuona tunaweza tukapunguza ama kuondoa kabisa changamoto hii kwa kushirikiana na Wizara ya Mazingira, Wizara ya Maji na Lake Victoria Commission na halmashauri mbalimbali ambazo ndani yake kunapatikana hii. Kwanza, tumeendelea kutoa elimu kwa maeneo mbalimbali tukiwa na lengo kwamba, ikiwezekana hata wananchi wenyewe waone namna ya kuanza kupunguza hii changamoto.

Mheshimiwa Spika, kingine tumeanza kusimamia sheria kwa sababu kinachoonekana, kuna baadhi ya mambo yanafanyika ambayo ndiyo yanayosababisha hasa pengine kuenea kwa haya magugu maji.

Mheshimiwa Spika, kikubwa, Serikali tunaendelea kutafuta fedha ili kuona namna ambavyo tunaondoa kabisa changamoto ya uwepo wa magugu maji kwa sababu imekuwa ni athari kubwa kwanza kwenye shughuli za uvuvi, na hata shughuli za kiusalama wa wananchi. Inafika wakati wanyama wakali wanatoka kwenye magugu wanakuja kwenye mitaa kusababisha athari kwa wananchi, nakushukuru.

Name

Issaay Zacharia Paulo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mbulu Mjini

Primary Question

MHE. CONSTANTINE J. KANYASU aliuliza: - Je, Serikali inafahamu ongezeko la magugu maji Ziwa Victoria na zipi athari za Magugu hayo na mpango wa kuyadhibiti?

Supplementary Question 2

MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Spika, mwaka 2023 timu ya Kitaifa kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais ilitembelea Ziwa Babati na Ziwa Tlawi katika Mkoa wa Manyara. Je, ni lini taarifa ya hiyo timu itarudi kwa ajili ya utekelezaji?

Name

Khamis Hamza Khamis

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Uzini

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Zacharia kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba timu hiyo ilikwenda baada ya Mheshimiwa Mbunge kuleta hapa taarifa ya changamoto zilizokuwepo kule. Tukaunda timu ili kuona namna ambavyo tunaweza tukasaidia kuondoa magugu maji na changamoto nyingine zilizopo hapo. Nimwambie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba, taarifa hii italetwa na itawasilishwa kwake ama itawasilishwa kwa maeneo husika ili wananchi pamoja na viongozi wa eneo hilo waweze kupata taarifa kamili ya utekelezaji wa timu hii, nashukuru.