Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Kenneth Ernest Nollo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bahi

Primary Question

MHE. KENNETH E. NOLLO aliuliza: - Je, Serikali ina mpango gani wa kuweka Sheria kabambe kudhibiti uharibifu wa mazingira nchini?

Supplementary Question 1

MHE. KENNETH E. NOLLO: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu mazuri kiasi ya Serikali. Nina maswali mawili ya nyongeza. Sheria za mazingira kwa wale wanaokosa au kuharibu kutokana na sheria hii wamekuwa wakipewa adhabu ya kulipa faini. Je, Serikali ina mpango gani kuchukua baadhi ya makosa ya uharibifu wa mazingira kuwa makosa ya kijinai?
Mheshimiwa Spika, nchi jirani ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, niseme tu, ni Kenya, tayari wana Mahakama ya Mazingira. Je, Serikali ina mpango gani wa kuanzisha Mahakama ya Mazingira ambayo kwa wenzetu imefanya vizuri zaidi katika kudhibiti uharibifu wa mazingira.

Name

Khamis Hamza Khamis

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Uzini

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Spika, naomba nijibu maswali mawili ya Mheshimiwa Nollo kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli kuna watu wanachafua mazingira na wanapochafua mazingira zipo hatua ambazo zimeelezwa kwenye sheria hii, sheria ambayo kwa sasa ndiyo tumeanza mchakato wa kuanza kuifanyia marekebisho kwenye baadhi ya vifungu.

Mheshimiwa Spika, tumeona wazo la kwenda kwenye Mahakama, of course, tutalichukua twende tukalifanyie kazi tuone linavyowezekana, lakini zaidi kwenye jambo la sheria za mazingira tumeona bora tuende zaidi kwenye maridhiano pamoja na kutoa maelekezo na kutoa onyo, fidia, faini ikiwezekana hata kuifungia kabisa ama kuzuia shughuli zisiendelee.

Mheshimiwa Spika, kama unavyojua sasa hivi mazingira yamekuwa ni biashara. Sasa ikiwa kila anayechafua mazingira tunasema tunampeleka Mahakamani, tunaweza tukafika mahali hata Mheshimiwa Mbunge mwenyewe tukamburuza huko.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa kwamba jambo hili tumo katika mchakato wa kufanya mabadiliko madogo ya Sheria ya Mazingira Sura 191 ili hata hayo mapendekezo aliyoyapendekeza yaweze kuwemo kwenye sheria yetu hii, likiwemo suala zima la uwepo wa Mahakama ya Mazingira Tanzania, nashukuru.

Name

Abdul Yussuf Maalim

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Amani

Primary Question

MHE. KENNETH E. NOLLO aliuliza: - Je, Serikali ina mpango gani wa kuweka Sheria kabambe kudhibiti uharibifu wa mazingira nchini?

Supplementary Question 2

MHE. ABDUL YUSSUF MAALIM: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Je, Serikali ina mikakati gani wa kuweza kuimarisha sheria ya udhibiti wa uchafuzi wa mazingira unaosababishwa na meli baharini? (Makofi)

Name

Khamis Hamza Khamis

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Uzini

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Spika, hivi karibuni tumeanza, ama tumekuwa na mchakato wa kufanya marekebisho madogo ya Sheria ya Mazingira Sura 191. Miongoni mwa mambo ambayo tunataka tuhakikishe kwamba tunayafanyia kazi ni jambo la uchafuzi wa vyanzo vya maji ikiwemo jambo la uchafuzi wa masuala ya mazingira kwenye maeneo ya bahari.

Mheshimiwa Spika, nimwambie tu Mheshimiwa, itakapokamilika sheria hii, hayo mambo ambayo ameyashauri na amependekeza yawemo, basi tutahakikisha kwamba yanakuwemo ili kuendelea kunusuru mazingira, hasa mazingira ya Bahari, nashukuru.