Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Mariamu Nassoro Kisangi
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. MARIAM N. KISANGI K.n.y. MHE. BONNAH L. KAMOLI aliuliza:- Je, hatua gani za kinidhamu zimechukuliwa kwa madaktari wanaoendelea kuzuia Maiti kutokana na deni la matibabu kinyume na maelekezo ya Serikali?
Supplementary Question 1
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali la nyongeza.
Kwa kuwa matamko haya na nakala hizo za kutokuzuia maiti katika hospitali zinasemwa mara nyingi sana hapa Bungeni, lakini ukienda kwenye utekelezaji haipo kama Mheshimiwa Naibu Waziri unavyoongea, je, Serikali inatoa tamko gani la wazi kabisa kwa wananchi ambao wanashindwa kupata maiti zao kwa wakati? Naomba nipate tamko hilo toka kwa Mheshimiwa Waziri hapa leo na litekelezwe. (Makofi)
Name
Dr. Godwin Oloyce Mollel
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Siha
Answer
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kuanzia aliyeuliza swali, pamoja na mama yangu aliyeuliza kwa niaba kwa sababu kwa kweli amekuwa akifuatilia wananchi hasa wa Mkoa wa Dar es Salaam. Kila wakati amekuwa akija kwetu kwa matatizo kama haya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nitoe maelekezo kwamba, kwa haya maelekezo nataka kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba tutaanza kuchukua hatua kali kwa wanaohusika. Pia, nawaomba wananchi ambao wanakutana na matatizo hayo wakubali kufuata zile taratibu ambazo wanapewa na wataalamu wetu kwa sababu hizo taratibu zisipofuatwa, hapa ndani mtakuja kuhoji pia kwa hoja za ukaguzi.
Name
Anatropia Lwehikila Theonest
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. MARIAM N. KISANGI K.n.y. MHE. BONNAH L. KAMOLI aliuliza:- Je, hatua gani za kinidhamu zimechukuliwa kwa madaktari wanaoendelea kuzuia Maiti kutokana na deni la matibabu kinyume na maelekezo ya Serikali?
Supplementary Question 2
MHE. ANATROPIA L. THEONEST: Mheshimiwa Spika, wakati mwingine kushindwa kuchukua maiti hutokana na vifo vinavyotokea ghafla. Juzi tulisikia kauli ya Mkuu wa Mkoa akieleza alivyomjibu mjamzito ambaye hakuwa na vifaa vya kujifungulia. Wakati mwingine kukosa hivyo vifaa hupelekea maambukizi wakati wa kujifungua na mwanamke kuchelewa kujifungua inaweza kupelekea mauti.
Mheshimiwa Spika, ni nini kauli ya Serikali kwa wanawake wanaoshindwa kupata vifaa vya kujifungua, lakini kwa viongozi ambao walipaswa kuwasaidia kuja na kauli za kuwakatisha tamaa, akimwambia aende mume wake akamsaidie kujifungua? Nataka kujua kauli ya Serikali kwa sababu ndiyo mambo yanayosababisha vifo na watu kushindwa kuchukua maiti zao.
Name
Dr. Godwin Oloyce Mollel
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Siha
Answer
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Spika, kwanza nimkumbushe Mheshimiwa Mbunge kwamba yeye ni Mbunge na ni mwanasiasa. Wakati mwingine anaweza akawa anazungumza watu wakakata sehemu ndogo sana ya mazungumzo yake halafu wakapotosha hali halisi ya ambacho alikuwa anasema.
Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba suala alilolizungumzia ni nyeti mno. Suala la akina mama na mambo mengine ya dharura tunatoa maelekezo mahususi. Kwanza, kwa hospitali za private pia za umma, kwamba mama na mtu yeyote wa dharura akija ni lazima kwanza apate huduma, siyo suala la kuulizwa fedha au kufanya nini. Huduma kwanza, fedha baadaye. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, niwaambie Waheshimiwa Wabunge kwamba, kwenye hili eneo la akina mama na watoto tunajua sisi wenyewe tumepitisha shilingi bilioni 200 kwa ajili ya dawa, lakini kwa mwaka ukipiga gharama za kuwatibu akina mama na watoto ni shilingi bilioni 227 na sisi kwa huduma zote tumetenga shilingi bilioni 200.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kunakuwa na hatua mbalimbali zinazofanywa ili ku-balance hizo hela. Kwa sababu anapokwenda mke wa Dkt. Mollel, ni wakati gani unatambua huyu ni mke wa Dkt. Mollel amejifungua? Huyu ni wa nani na tunao watu wengi kule. Unakuta mtu huyo huyo hana bima, hana chochote, lakini anachangia harusi shilingi milioni moja, bali ikifika suala la mke wake kujifungua, hana hizo fedha, anataka asaidiwe bure.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naomba Waheshimiwa Wabunge mwendelee kutuvumilia, lakini mjue Serikali kwa mwaka juzi tu ilitumia shilingi bilioni 661 kwa eneo la msamaha tu. Serikali imekuwa ikifanya hivyo, lakini wote tukubaliane, kupanga ni kuchagua.
Name
Abdallah Jafari Chaurembo
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mbagala
Primary Question
MHE. MARIAM N. KISANGI K.n.y. MHE. BONNAH L. KAMOLI aliuliza:- Je, hatua gani za kinidhamu zimechukuliwa kwa madaktari wanaoendelea kuzuia Maiti kutokana na deni la matibabu kinyume na maelekezo ya Serikali?
Supplementary Question 3
MHE. ABDALLAH J. CHAUREMBO: Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Serikali imetoa Waraka kwa Marehemu ambao ndugu zao hawana uwezo waweze kutolewa, je, Serikali haioni ipo haja ya kutupa sisi wawakilishi wa wananchi Waraka huo ili tuweze kuwaelimisha wananchi wetu? (Makofi)
Name
Dr. Godwin Oloyce Mollel
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Siha
Answer
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Spika, namshukuru Mheshimiwa Mbunge kwa swali lake zuri. Serikali iko tayari kuwapa Waraka, lakini pia kuwaomba kuwaelimisha wananchi wawe tayari kufuata zile taratibu ambazo zimewekwa. Kwa sababu kule kwenye hospitali zetu zote kumewekwa Maafisa Maendeleo ya Jamii ili tuweze kukwepa zile hoja za ukaguzi, kwa sababu tusipopata hivyo, watu wanaweza wakatumia mwanya huo na kusema kwamba wamesamehe, kumbe fedha za umma zimetumika vibaya.
SPIKA: Kwa hiyo, huo Waraka watapewa Waheshimiwa Wabunge?
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Spika, kabisa na nitahakikisha Jumatatu tunauleta, tutagawa kwa Waheshimiwa Wabunge. (Makofi)
Name
Husna Juma Sekiboko
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. MARIAM N. KISANGI K.n.y. MHE. BONNAH L. KAMOLI aliuliza:- Je, hatua gani za kinidhamu zimechukuliwa kwa madaktari wanaoendelea kuzuia Maiti kutokana na deni la matibabu kinyume na maelekezo ya Serikali?
Supplementary Question 4
MHE. HUSNA J. SEKIBOKO: Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Serikali imetoa kauli, Waraka na matamko lakini bado suala la kuzuia maiti linaendelea. Kwa nini Serikali isituletee sheria ili anayezuia maiti ashughulikiwe kwa mujibu wa sheria? (Makofi)
Name
Dr. Godwin Oloyce Mollel
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Siha
Answer
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Spika, kwanza nampongeza Mheshimiwa Mbunge anavyowahudumia wananchi na hasa wanawake kwenye eneo la mkoa wake. Hata hivyo, kama nilivyosema, tatizo kubwa tuliloona baada ya kufuatilia, siyo kwamba watumishi wetu hawakubali kuachia maiti, ila wananchi wanakataa kufuata utaratibu uliowekwa na Serikali. Naomba Mheshimiwa Mbunge, kwa sababu tunaenda kwenye suala la Bima ya Afya kwa Wote, huduma ya afya kwa wote itakuwa suluhisho ya hili tatizo. (Makofi)