Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Fatma Hassan Toufiq
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. FATMA H. TOUFIQ aliuliza: - Je, watoto wa kike wangapi na wanawake wangapi walioathirika na utoaji mimba usio salama nchini?
Supplementary Question 1
MHE. FATMA H. TOFIQ: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa fursa ya kuuliza maswali ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza. Ni nini mkakati wa Serikali kutoa elimu ili kupunguza vifo vya wanawake wanaotoa mimba au mimba zinazoharibika?
Mheshimiwa Spika, swali la pili. Baadhi ya wanawake ambao wamekuwa wakibakwa wamekuwa wakipata mimba ambazo hawakuzitarajia, ni nini kauli ya Serikali kutokana na kadhia hii? Ahsante. (Makofi)
Name
Dr. Godwin Oloyce Mollel
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Siha
Answer
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Spika, kwanza nampongeza Mheshimiwa Mbunge kwa sababu kwa kweli hata akiwa anatusimamia kwenye Kamati za Afya amekuwa akilisimamia eneo hili na suala zima la afya ya mwanamke.
Mheshimiwa Spika, niseme tu, mkakati wa Serikali ni endelevu, tumekuwa tukitoa elimu kwa kutumia vyanzo mbalimbali lakini mkakati mwingine ni kupeleka vituo karibu zaidi na wananchi. Kama ambavyo mnajua, kwa mwaka huu tu, Serikali yetu, Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan, amejenga vituo zaidi ya 480 ili kupeleka huduma hizi karibu na wananchi na wananchi waweze kupata huduma.
Mheshimiwa Spika, namwomba Mheshimiwa Mbunge, Bunge hili na Watanzania waendelee kufuata maelekezo ambayo yametolewa, na tushirikiane pamoja kutoa elimu. Mheshimiwa Mbunge, nakuhakikishia Wizara ya Afya tutajipanga kutoa elimu zaidi kwenye eneo hili.
Mheshimiwa Spika, swali lake la pili la akina mama kubakwa na kupata mimba, nafikiri linahitaji zaidi elimu ya saikolojia baada ya hilo jambo kutokea. Pia, linahitaji sisi kulinda hayo maovu yasiendelee kutokea. Sisi tuwe mabalozi kwenye jamii kuhakikisha eneo hili la wanawake kunyanyaswa na kubakwa, haya mambo hayatokei kwenye jamii yetu. (Makofi)
Name
Dr. Thea Medard Ntara
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. FATMA H. TOUFIQ aliuliza: - Je, watoto wa kike wangapi na wanawake wangapi walioathirika na utoaji mimba usio salama nchini?
Supplementary Question 2
MHE. DKT. THEA M. NTARA: Mheshimiwa Spika, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha kwamba matumizi ya P2 yanaelezwa vizuri ili wasichana wetu wasije wakaathirika baadaye kwa kukosa kupata watoto? Ahsante.
Name
Dr. Godwin Oloyce Mollel
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Siha
Answer
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Spika, nakubaliana na Mheshimiwa Mbunge kwa 100% kwamba kumekuwa na matumizi mabaya kwenye eneo la P2. Hata hivyo, tayari Serikali imeshaanzisha kampeni maalumu inayosema, “Holela holela itaku-cost” ikilenga kuelezea matumizi mabaya ya holela holela kwenye dawa zote ikiwepo eneo hili la kutumia P2.
Mheshimiwa Spika, natumia fursa hii kuwaasa wananchi na wasichana wetu, pia nawaomba Waheshimiwa Wabunge tuendelee kuhimiza matumizi mazuri ya dawa pamoja na hili eneo la P2 kwenye mikutano yetu.
SPIKA: Mheshimiwa Naibu Waziri, P2 ni nini? (Kicheko)
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Spika, ni zile dawa za kuzuia mimba, wengine wanaweza wakafanya bahati mbaya ikatokea kwamba hawakutumia kinga, basi anakimbilia kutumia P2 kabla ya masaa 72. (Kicheko)
Name
Aida Joseph Khenani
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Nkasi Kaskazini
Primary Question
MHE. FATMA H. TOUFIQ aliuliza: - Je, watoto wa kike wangapi na wanawake wangapi walioathirika na utoaji mimba usio salama nchini?
Supplementary Question 3
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Spika, wanawake wanaopoteza maisha ni Watanzania na ili tumalize tatizo, ni lazima tulijue tatizo. Napenda kufahamu, Wizara imefanya tathmini na kugundua nini kinasababisha utoaji wa mimba usiokuwa salama? Nashukuru kwa nafasi.
Name
Dr. Godwin Oloyce Mollel
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Siha
Answer
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Spika, kwanza namshukuru Mheshimiwa Mbunge kwa sababu hili suala ni sensitive na sisi linatutesa sana kwa maana ya kwenye vituo vyetu. Hata hivyo, linaleta gharama kubwa kwa sababu kwanza anayetoa mimba anazidiwa, na akifika hana hata shilingi kumi. Kwa hiyo, ni gharama kubwa sana kwa Serikali kuhudumia eneo hilo na unaona ni zaidi ya wananchi 180,000 na zaidi.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, sisi tunachosema ni kwamba ni mimba ambazo hazikupangiliwa, maana yake tuna kazi kubwa sana ya kuendelea kuhimiza uadilifu kwenye jamii yetu na hasa kutoa elimu kuanzia level ya primary na secondary. Pia, akina mama wakati mwingine inatokea ana mimba ambayo anajua siyo ya mume wake sasa wakati mwingine inatokea mambo kama hayo. (Makofi/Kicheko)
Name
Felista Deogratius Njau
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. FATMA H. TOUFIQ aliuliza: - Je, watoto wa kike wangapi na wanawake wangapi walioathirika na utoaji mimba usio salama nchini?
Supplementary Question 4
MHE. FELISTA D. NJAU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru nami kwa kunipatia nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Ni lini Serikali itakuja na sheria ya kumlinda mwanamke ambaye amepata mimba isiyotarajiwa, kwa mfano kubakwa au kupata mimba za ndugu, baba na watu wengine. Ahsante sana. (Makofi)
Name
Dr. Godwin Oloyce Mollel
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Siha
Answer
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Spika, nadhani kwanza swali lake ni zuri sana na ni la muhimu sana; lakini niseme tu kwamba, sidhani kama suala ni sheria. Zipo sheria nyingi sana za kumlinda mwanamke, lakini ni suala la kijamii.
Mheshimiwa Spika, ni suala la jamii yetu kuendelea kuhimizana utu, uadilifu, upendo, na mambo mengine. Kwa sababu tukubaliane tu kwamba hakuna Kanisa wala Msikiti uliowahi kumuua shetani. Kwa hiyo, shetani bado yupo na anasumbua watu. Tuendelee kupambana. Hata hivyo, ninachosema, tuendelee kusisitizana kumpinga huyo shetani. (Makofi)
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved