Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Nusrat Shaaban Hanje
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. NUSRAT S. HANJE aliuliza: - Je, lini wananchi waliopisha mwekezaji katika Mgodi wa Shanta Kata ya Mang’onyi Jimbo la Singida Mashariki watalipwa fidia?
Supplementary Question 1
MHE. NUSRAT S. HANJE: Mheshimiwa Spika, sisi Wananchi wa Singida Mashariki, Mang’onyi na vijiji vyake tunashukuru kwamba Serikali baada ya muda sana wameanza kulipa wananchi na zoezi kwa kweli linaendelea vizuri kwa sababu mimi nipo kule. Hata hivyo, pamoja na majibu ya Mheshimiwa Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza upande wa CSR.
Mheshimiwa Spika, mwekezaji alitakiwa kulipa dola 150,000 kwa ajili ya CSR kugharamia miradi muhimu ikiwemo Mradi wa Ujenzi wa Sekondari ya Sambaru ambayo ni muhimu sana na watoto wanatembea kilometa 30 kwenda shuleni; na una watoto takribani 72 wamepata ujauzito mwaka jana, 2024. Sasa, mwaka jana kwenye ile shule ilikuwa inatakiwa dola 40,000 ilipwe lakini mpaka leo haijalipwa hata shilingi. Sasa, nataka kufahamu, Serikali ina jitihada gani za makusudi na za haraka kwa sababu mwaka umeshapinduka na mwaka huu inabidi walipe tena CSR ili kuhakikisha kwamba watoto wetu wanapatiwa hiyo shule ili waache kukaa magetoni? Maana yake pale kuna wachimbaji na wale watoto wana mazingira magumu sana especially watoto wa kike. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali langu la pili, upande wa rasilimali, tunategemea wananchi wanufaike sana kwenye CSR. Sasa, nataka kufahamu jitihada za makusudi na madhubuti za Serikali kuhakikisha wanawalazimisha wawekezaji kuhakikisha wanalipa CSR kwa wakati kwa sababu njia rahisi ya Mtanzania kunufaika kwenye uwekezaji ni kupitia CSR.
Mheshimiwa Spika, sasa nataka kufahamu, Serikali ina njia gani madhubuti ikiwezekana kuwapiga faini kwa sababu muda unakwenda na unakuta miradi iliyopangwa ya muhimu haijafanikiwa? Ahsante.
Name
Dr. Stephen Lemomo Kiruswa Mamasita
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Longido
Answer
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Spika, kwa suala la CSR ambayo kampuni husika inapaswa kutoa, kampuni hii imekuwa ikitoa CSR kila mwaka, kwa mfano mwaka 2024 walitenga dola 180,000 na mwaka huu wametenga dola 150,000. Kinachogoma ni kwamba wananchi wanaozunguka migodi kupitia halmashauri zao, zinachelewa katika kuibua vipaumbele na zinachelewa katika kuthibitisha au kuidhinisha ile miradi ambayo imependekezwa.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nawaasa halmashauri zote nchini zinazopokea fedha za CSR, waongeze bidii katika kuhakikisha kwamba wanaibua miradi mapema, lakini pia wanaidhinisha ile miradi, maana mingine ina michoro ambayo lazima halmashauri iidhinishe ili iweze kutekelezwa kwa wakati.
Mheshimiwa Spika, sasa, ninajibu swali lake la pili, kwamba fedha za CSR zinawanufaishaje wananchi? Zinawanufaisha wananchi ambao wameshaibua vipaumbele na mwekezaji atatoa zile fedha kwa kadiri alivyokuwa amepanga kuzichangia kwa mujibu wa Kanuni yetu ya CSR.
Mheshimiwa Spika, shida inatokea pale ambapo wananchi hawajakubaliana katika vipaumbele, fedha zipo na zisipotumika katika mwaka husika, zinahamishika kwenda mwaka unaoendelea. Ndiyo maana fedha za mwaka 2024 za Shanta, zinaendelea kutumika katika miradi ambayo ilishakubalika kama Stendi ya Igunga, tayari iko kwenye hatua ya upauzi, lakini pia katika kununua trekta la kufanya usafi wa mazingira na la kuzoa taka ambalo limeshanunuliwa liko njiani limeagizwa na baadhi ya vyoo vya shule aliyoisema vimeshajengwa.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, fedha hizi zipo na zinaendelea kutumika bila kujali kwamba mwaka wake umepita au la. Ila wananchi waongeze kasi katika kukubaliana kwenye miradi husika. Ahsante sana.
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved