Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Festo Richard Sanga
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Makete
Primary Question
MHE. FESTO R. SANGA aliuliza: - Je, Serikali haioni haja ya kuzuia usajili holela wa laini za simu mitaani kutokana na utapeli unaoendelea mitandaoni?
Supplementary Question 1
MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Spika, kwanza nampongeza Mheshimiwa Waziri kwa majibu, lakini jambo la kwanza, Mheshimiwa Waziri ana-admit, kwa maana ya kukubaliana kwamba kuna ulaghai wa upatikanaji wa laini?
Mheshimiwa Spika, swali la pili. Waziri atakubaliana nami kwamba, bado vitendo vya utapeli kupitia laini za simu mitandaoni ni kwa kiwango kikubwa sana na yawezekana hata yeye Mheshimiwa Waziri ameshatumiwa namba za matapeli kwamba tuma fedha kwenye namba hii? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ni takribani miaka 10 sasa hivi tunazungumzia suala la utapeli mitandaoni ambao unafanyika kwa mbinu mbili tofauti. Ya kwanza, ni hiyo ya kutuma meseji, ya pili, kuna watu wanaozunguka vijijini wanasema ni mawakala wanaosajili laini, wanawapa simu wazazi wetu, wanaingiza PIN kwenye zile laini, ukituma hela kwenye namba ya mzazi, hela inatoka inaenda kwenye maeneo mengine. Huo wizi umekuwa ukifanyika.
Mheshimiwa Spika, sasa, nina maswali mawili Mheshimiwa Waziri. La kwanza, ni hatua gani imechukuliwa na Wizara kudhibiti hao watu ambao wanalaghai au wanagawa laini kwa watu ambazo zinatumika kwenye utapeli? Kwa sababu ni zaidi ya laini milioni, mimi nimetumiwa, wewe umetumiwa, yule ametumiwa kwa laini tofauti tofauti, Wizara wameshindwaje kudhibiti hilo?
Mheshimiwa Spika, la pili, Wizara inaona mkakati upi ni rahisi wa kuweka vibanda maalumu kwenye maeneo ama wilayani ama kwenye kata ambako huduma hiyo inapatikana ili mwananchi asipate huduma kutoka kwa mtu anayezurura mitaani na baadaye anaishia kutapeliwa? Ahsante. (Makofi)
Name
Maryprisca Winfred Mahundi
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Answer
NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, kwanza, ninamshukuru Mheshimiwa Festo Sanga kwa pongezi na kutambua kwamba tunafanya kazi kubwa sana ya kudhibiti. Vilevile nampongeza Mheshimiwa Mbunge, hii ni mara ya pili namjibu swali hili. Nilishajibu tena, aliuliza kama swali la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, napenda sisi kama Serikali tumeshachukua hatua kali sana kupitia TCRA. Utakuwa shahidi pia, wimbi la meseji hizi za utapeli zimepungua kwa kiasi fulani, ilikuwa balaa zaidi ya ambavyo ipo sasa hivi.
Mheshimiwa Spika, TCRA wanaendelea na namna mbalimbali za kuona kwamba zinadhibiti hizi laini ambazo zimepatikana kwa njia isiyo sahihi. Kwa hiyo, kama Serikali tumeshachukua hatua na kazi inaendelea. Nampongeza sana DG wa TCRA kaka yangu Bakari, anafanya kazi kubwa na timu yake nzima na kazi inaendelea.
Mheshimiwa Spika, mkakati wa kuona kwamba angalau tunapunguza hawa freelancers ambao wanapita huko kuona kwamba tunarahisisha kuwafikia wananchi, lengo lilikuwa zuri, hawa vijana waweze kuwafikia wananchi kule ili kuwapunguzia ugumu wa upatikanaji wa laini, lakini matumizi yamekwenda kuwa mabaya. Kwa hiyo, tayari pia tumepunguza sana namna ya hawa freelancers kuzagaa huko kwenye jamii.
Mheshimiwa Spika, vilevile, tutaendelea kuhakikisha tunaongeza udhibiti kuona kwamba laini za simu zitapatikana maeneo maalumu kama alivyoshauri Mheshimiwa Mbunge.
Name
Dr. Angeline Sylvester Lubala Mabula
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Ilemela
Primary Question
MHE. FESTO R. SANGA aliuliza: - Je, Serikali haioni haja ya kuzuia usajili holela wa laini za simu mitaani kutokana na utapeli unaoendelea mitandaoni?
Supplementary Question 2
MHE. DKT. ANGELINE S. L. MABULA: Mheshimiwa Spika, napenda kuuliza swali la nyongeza kwamba, matapeli ni kweli wapo, nami ni mmoja wa wahanga, wanatumia majina ya viongozi kutapeli watu. Baadhi ya viongozi wengi hasa wa dini wametapeliwa kwa njia hiyo hiyo.
Mheshimiwa Spika, hiyo namba 15040 ambayo anasema turipoti, tunaripoti kweli na wanakiri kupokea, lakini hatupati mrejesho wa kujua nini kimefanyika baada ya kuwa tumeripoti. Je, Serikali haioni kwamba inatujengea mazingira magumu katika jamii pale ambapo majina yetu yanatumika kutapeli watu?
Name
Maryprisca Winfred Mahundi
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Answer
NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, nampongeza Mheshimiwa Dkt. Angelina Mabula kwa namna ya ufuatiliaji. Pia ameshakuwa akifuatilia hili kwangu, lakini matumizi ya majina ya viongozi, hili nalo tunaendelea kulifanyia kazi. Taarifa zote mnazotupatia, hata juzi tu hapa nimepokea karibia Waheshimiwa Wabunge watatu wote wananijia na vithibitisho, majina ya baadhi ya viongozi yanavyoendelea kutumika. Tayari nimeshayaripoti TCRA, kazi kubwa sana inaendelea kufanyika.
Mheshimiwa Spika, suala la mrejesho wa nini kimefanyika, tutaendelea kusisitizana na Watendaji kuona kwamba wewe uliyeleta taarifa yako, basi uweze kupata mrejesho. Iwe kiongozi, iwe mwananchi wa kawaida, wote waweze kupata mrejesho namna ambavyo suala limeweza kushughulikiwa. Sisi kama Serikali, tutahakikisha hatuweki mazingira magumu ya kuona kwamba jamii inaendelea kutapeliwa kwa sababu siyo jambo jema. Sisi kama Serikali, kazi yetu kubwa ni kuhakikisha jamii inapata maendeleo na mazingira rafiki ya kuona kila mmoja anakuwa salama akiwa anatumia mtandao wa simu.
Name
Dr. Tulia Ackson
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Mbeya Mjini
Primary Question
MHE. FESTO R. SANGA aliuliza: - Je, Serikali haioni haja ya kuzuia usajili holela wa laini za simu mitaani kutokana na utapeli unaoendelea mitandaoni?
Supplementary Question 3
SPIKA: Mheshimiwa Naibu Waziri, pamoja na shukurani kwa maswali ya Waheshimiwa Wabunge, lakini tatizo kwa kweli ni kubwa na ni kwa watu wengi. Mimi hapa leo nikisema ni watu wangapi nchi hii wametapeliwa kwa jina langu, yaani mimi mwenyewe napata hizo jumbe mpaka sasa hivi nimeshachoka na kutoa taarifa. Kwa nini? Kwa sababu nawaza, utapeli nimesharipoti, lakini unaendelea na haya matangazo yao hayawekwi kifichoni, watu wanatangaziwa kwenye sijui mitandao ile ya kijamii: Facebook kuna matangazo, sijui Instagram kuna matangazo. Huko kote wanatangaza, na wapo wameweka namba za simu, wanapigia watu simu na sasa hivi kuna ile akili nini? Akili mnemba imebadilishwa jina inaitwa sijui akili kufanyaje...?
Mtu anasema umenipigia wewe simu, na ninaongea na wewe. Sasa mimi Spika naweza kumpigia simu mwananchi kwamba nakopesha hela? Lakini ndiyo hivyo watu wanatapeliwa kila siku.
Sasa, sijajua yaani kama Wizara ama ni TCRA, kama ni juhudi, basi nchi yetu jambo hili mbona limekuwa kubwa sana! Yaani huko kwingine tunakosafiri hatusikii mambo haya, kwa nini Wananchi wa Tanzania wanatapeliwa kiasi hiki na sisi tuna TCRA? Yaani kama shida ni TCRA, shida iko wapi ili tuifanyie kazi? Maana utapeli umezidi hasa wa jina langu mimi. Yaani hata sasa hivi ninavyoongea, kuna watu huko wanatapeliwa.
Mheshimiwa Waziri, naona umesimama.
Name
Jerry William Silaa
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Ukonga
Answer
WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, kwanza nakiri kwamba tunayo maendeleo makubwa ya teknolojia ya habari na mawasiliano, na maendeleo haya yametokana na uwekezaji mkubwa wa Serikali ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kazi kubwa inafanyika. Jana nilipata Waheshimiwa Wabunge wengi wakionesha hata ujenzi wa kasi wa minara ile 758 inafanyika kwa kiasi kikubwa.
Mheshimiwa Spika, sasa kila maendeleo yana changamoto. Maendeleo ya ukuaji wa teknolojia yamekuja na watu ambao wanatapeli. Utapeli ulikuwepo, sasa utapeli umekuwa digitalized. Ukisoma Taarifa ya Takwimu za Mawasiliano inayotolewa na TCRA kwa kila robo ya mwaka, kwa robo ya pili ya mwaka, ni kweli kazi kubwa imefanyika na ukisoma ukurasa wa 40, utapeli umepungua kwa 19% ingawa bado upo.
Mheshimiwa Spika, sasa nini kinafanyika na Serikali? Tarehe 22 Novemba, 2024 Wizara yangu ilikaa pamoja na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi na iko mikakati ilifanyika kwa sababu ili suala mtambuka…
SPIKA: Sekunde moja Mheshimiwa Waziri. Mheshimiwa Naibu Waziri, kwa sababu hakukuwa na Mheshimiwa Mbunge mwingine aliyesimama, unaweza kwenda kuketi. Ahsante sana.
Mheshimiwa Waziri.
WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, tarehe 22 Novemba, 2024, Wizara yangu iliratibu kikao cha sekta mbalimbali ikiwemo Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Benki Kuu ya Tanzania kwa sababu miamala ya fedha inasajiliwa na Benki Kuu, Ofisi ya DPP, Jeshi la Polisi, kampuni za Simu, TCRA, na wadau wengine. Kikao kile kimezaa taskforce ya wataalamu ambao imeshaanza kazi, na hivi ninavyozungumza, tumeshakubaliana na Mheshimiwa Bashungwa, mapema mwezi wa Pili tutakaa kikao tena cha high level kuangalia njia za kufanya.
Mheshimiwa Spika, kubwa ambalo tumeelekeza kampuni za simu ni kutoa elimu kwa sababu ukiangalia utapeli wa aina zote una element kubwa ya ulaghai. Kupitia Bunge lako, nawaomba Watanzania, kwa kuwa maendeleo ya teknolojia yanakwenda kwa kasi, na sisi tuongeze umakini. Umakini wa kwanza, hata leo asubuhi kuna mtu nimemsaidia, tusibonyeze link ambazo tunatumiwa tukiambiwa ni bahati nasibu, umeshinda, kuna mkopo wa Mheshimiwa Spika au wa kiongozi mwingine.
Mheshimiwa Spika, jambo la pili, tusitoe namba zetu za siri pale tunapopigiwa simu na mtu tusiyemfahamu. Namba tatu, ni kuongeza umakini.
Mheshimiwa Spika, kupitia Bunge lako, naendelea kutoa maelekezo kwa kampuni zote za simu, ziendeleze kampeni za kutoa elimu kwa watumiaji wa simu ya kuongeza umakini wa mitandao ya simu. Sisi kama Serikali kama nilivyoahidi hapa, tutaendelea kufanya kazi ya kuhakikisha tunawasaidia wananchi na kupunguza uhalifu huu.
Mheshimiwa Spika, Jeshi la Polisi kupitia Wizara ya Mambo ya Ndani, kupitia mkutano ule wa tarehe 22 Novemba, 2024 liliahidi kufanya operesheni hasa kwa mikoa ya Rukwa na Morogoro ambapo ukisoma zile takwimu za utapeli wa mtandao, inaongoza kwenye Taifa letu.
Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha. (Makofi)