Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Cecil David Mwambe
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Ndanda
Primary Question
MHE. CECIL D. MWAMBE aliuliza:- Je, Serikali haioni kuwa uwepo wa aina nyingi za viuatilifu kwenye zao la korosho ni kuwachanganya wakulima?
Supplementary Question 1
MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri sana ya Mheshimiwa Waziri na kwa namna ya pekee kabisa, nawapongeza Wizara kwa jitihada zao. Kwa kuwa Mheshimiwa Waziri aliunda Tume iliyokwenda kufanya utafiti kuhusiana na masuala mbalimbali kwenye kilimo, kuna baadhi ya mapendekezo yalitolewa yameshatekelezwa, lakini kuna mapendekezo mengine bado hayajatekelezwa. Nataka kufahamu ni lini mapendekezo yote yaliyotolewa na tume aliyounda Waziri yatafanyiwa kazi?
Mheshimiwa Spika, swali la pili. Kutokana na mabadiliko ya tabia nchi, aina mbalimbali za viuatilifu vimekuwa vinafanya kazi kwenye maeneo tofauti, na jambo hili limekuwa linaathiri sana wakulima kwa sababu, kutokana na hali ya hewa utakuta viuatilifu vinavyotumika eneo la Masasi vina viambata tofauti kidogo na vile vinavyotumika maeneo ya Tandahimba na kuathiri uzalishaji. Je, Serikali iko tayari kufanya utafiti na kuelekeza matumizi sahihi ya viuatilifu kutokana na mabadiliko ya tabia nchi?
Name
David Ernest Silinde
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Tunduma
Answer
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Nami namshukuru sana Mheshimiwa Mbunge, Cecil Mwambe, kwa kazi nzuri anayoifanya kwa wananchi wake wa Jimbo la Ndanda na kwa kufuatilia hii taarifa ambayo inatokana na Tume ambayo Mheshimiwa Waziri aliiunda.
Mheshimiwa Spika, ni kweli katika taarifa ya tume, tayari kuna baadhi ya mapendekezo yaliyofanyiwa kazi na mengine yanaendelea kufanyiwa kazi. Nimthibitishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, yote ambayo yalipendekezwa na watalaam kwenye ile Tume yatafanyiwa kazi, likiwemo hili la kuangalia vile viuatilifu ambavyo havifanyi kazi katika baadhi ya maeneo.
Mheshimiwa Spika, jambo hili ni kwamba, linaenda kwenye sekta nzima ya mazao yote kwenye viuatilifu na wala siyo korosho peke yake. Kwa hiyo, nimuagize Mkurugenzi wa Mamlaka ya Mimea Tanzania kwamba, katika yale mapendekezo yaliyotolewa ambayo bado hayajafanyiwa kazi, likiwemo la kufuta leseni kwa wale wenye viuatilifu feki, lifanyike kabla ya mwezi wa Nne mwaka 2025, kabla ya Bunge la Bajeti halijaanza. Kwa hiyo, hili nimeona nilitoe kama maelekezo maalum kwa Mkurugenzi wa Afya ya Mimea Tanzania. Ahsante.
Name
Prof. Patrick Alois Ndakidemi
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Moshi Vijijini
Primary Question
MHE. CECIL D. MWAMBE aliuliza:- Je, Serikali haioni kuwa uwepo wa aina nyingi za viuatilifu kwenye zao la korosho ni kuwachanganya wakulima?
Supplementary Question 2
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Spika, nashukuru, je, Serikali ina mpango gani wa kununua viuatilifu au viuadudu vinavyozalishwa na kiwanda cha Plant Bio-Defenders cha Moshi ambavyo ni salama?
Name
David Ernest Silinde
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Tunduma
Answer
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, bahati nzuri Mheshimiwa Mbunge anafahamu, nami nilishafika katika hiki Kiwanda cha Plant Bio-Defenders ambacho wao wanatengeneza viuatilifu salama kwa kutumia natural resources. Serikali tulishakubali kwamba, tutaweka ruzuku katika viuatilifu vile ili viweze kupatikana kwa wakulima wote. Kwa hiyo, mpango ule bado upo, na tunaendelea kuutekeleza, ahsante.
Name
Agnes Elias Hokororo
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. CECIL D. MWAMBE aliuliza:- Je, Serikali haioni kuwa uwepo wa aina nyingi za viuatilifu kwenye zao la korosho ni kuwachanganya wakulima?
Supplementary Question 3
MHE. AGNES E. HOKORORO: Mheshimiwa Spika, katika Mkoa wa Mtwara ambao ndiyo giant kwa korosho, magonjwa yaliyozoeleka ni ubwiri unga na kukauka kwa maua. Je, Serikali haioni iko haja ya kuondoa huo utitiri wa dawa unaowachanganya wakulima na kubakiza dawa zake ambazo ndiyo magonjwa yamekuwa yakijitokeza ili korosho iwe na tija? (Makofi)
Name
David Ernest Silinde
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Tunduma
Answer
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, kama ambavyo nilijibu katika swali la msingi, ni kwamba; moja, sisi kama Serikali tulishapokea mapendekezo yote na ndiyo maana Mheshimiwa Waziri aliunda tume kupitia viuatilifu vyote vinavyohusika katika zao la korosho, vikiwemo vile ambavyo havifanyi kazi vizuri.
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri alishaelekeza maeneo yote ambayo kuna viuatilifu feki wafutiwe leseni, ili wasifanye biashara katika mnyororo mzima wa mazao hapa chini. Kwa hiyo, nasi tunaendelea kufanya tafiti kuhakikisha kwamba, haya aliyoyasema Mheshimiwa Mbunge yanaondoka katika maeneo yote likiwemo lile swali ambalo Mheshimiwa Mwambe alikuwa ameuliza hapa kuhusu kwamba, tunawezaje kupeleka viuatilifu kulingana na maeneo husika? Jambo hilo sisi tulishalipokea kama pendekezo na tumekuwa tukiwashauri wataalam kuhakikisha wanafanya hivyo, ili kuondoa hizi adha ambazo zimekuwa zikitokea kila mara.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nimthibitishie Mheshimiwa Mbunge, Serikali iko kazini na tutahakikisha hizi changamoto zinaondoka kabisa, ahsante.
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved