Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Mrisho Mashaka Gambo
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Arusha Mjini
Primary Question
MHE. MRISHO M. GAMBO aliuliza:- Je Serikali ina mpango gani wa kuingia ubia na Hospitali ya ALMC Arusha ili kuiokoa na changamoto za kifedha zinazoikabili?
Supplementary Question 1
MHE. MRISHO M. GAMBO: Mheshimiwa Spika, swali langu la msingi ni kuhusiana na Hospitali ya ALMC na linahusiana na kuingia ubia. Swali la kwanza; je, Serikali inaweza ikatupa time frame, kwamba ni baada ya mwezi mmoja, miezi mitatu au miezi sita, hasa ukizingatia kwamba tunakwenda kwenye Mashindano ya AFCON na pia kuna Royal Tour pale Arusha na huduma za afya ni muhimu.
Mheshimiwa Spika, swali la pili; ni kuhusiana na Serikali kusema kwamba imepeleka shilingi milioni 536.8. Hata hivyo kwa taarifa nilizonazo Serikali imepeleka shilingi milioni 130 kwa ajili ya ruzuku za dawa. Je, tunaweza tukapata mchanganuo wa shilingi milioni 406.8 ambazo zimesemwa hapa na Mheshimiwa Naibu Waziri?
Name
Sophia Hebron Mwakagenda
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MIPANGO NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Spika, kwanza nimshukuru Mheshimiwa Mbunge kwa kuwa amekuwa mstari wa mbele sana katika kuhakikisha kwamba anaipambania hospitali hii ili ipate fedha na iingie ubia na Serikali.
Mheshimiwa Spika, Serikali imefanya kazi kubwa ya kufuatailia matumizi ya hospitali hii (matumizi na fedha wanazokusanya) ambapo tumekuja kugundua kwamba kuna baadhi ya changamoto katika hospitali hiyo. Namwomba Mheshimiwa Mbunge tukitoka hapa nimweleze kuhusiana na changamoto zilizomo mule ndani ili aende akatoe ushauri. Serikali baada ya kuona imetatua changamoto hizo za ndani za hospitali hiyo, ninadhani Serikali itakuwa tayari katika kuendelea kutoa msaada zaidi kuhakikisha hospitali hiyo inaendelea kutoa huduma kwa wananchi.
Mheshimiwa Spika, tuendelee kutambua kwamba hospitali hizi ambazo zinamilikiwa na mashirika binafsi zimekuwa zikitoa msaada kwa Serikali na Serikali imekuwa ikitoa fedha ili kuhakikisha kwamba wananchi wanapata huduma kupitia hospitali hizo kwa sababu wote tunaenda kutoa huduma kwa wananchi.
Mheshimiwa Spika, suala la time frame ninaomba niendelee kusema kwamba time frame siwezi kutoa mpaka pale changamoto zitakapokuwa zimetatuliwa, hapo sasa inawezekana tukaenda kufikia muafaka.
Mheshimiwa Spika, mwisho, swali la pili ameuliza kuhusiana na mchanganuo wa fedha zilizotolewa. Serikali inatoa fedha kwa awamu. Fedha hizi ambazo tumesema tunakwenda kuzitoa mwaka huu zipo ndani ya bajeti na fedha ambayo imekwenda ni ile ambayo inakwenda hatua kwa hatua. Kwa hiyo, fedha inavyoendelea kupatikana tunaendelea kutoa fedha katika hospitali hiyo kwa ajili ya uendeshaji. Ahsante.
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved