Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Jacquline Andrew Kainja
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. JACQUELINE K. ANDREA aliuliza: - Je, lini Serikali itamaliza kusambaza umeme kwenye vitongoji nchini?
Supplementary Question 1
MHE. JACQUELINE K. ANDREA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Je, Serikali haioni kuna haja ya kuongeza kasi katika kupeleka umeme kwenye vitongoji?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili. Nini mkakati na mpango madhubuti wa vitongoji vilivyobaki katika Mkoa wangu wa Tabora?
Name
Judith Salvio Kapinga
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Answer
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa maswali ya Mheshimiwa Mbunge. Kuhusiana na Serikali kuongeza kasi ya kupeleka umeme kwenye vitongoji, tayari kwa mwaka huu wa fedha katika mradi wetu wa kupeleka umeme kwenye vitongoji 20,000 kwa awamu tulikuwa tumepanga vitongoji 4,000, lakini Serikali imetafuta fedha takribani shilingi trilioni 1.5 na sasa tutapeleka umeme kwenye vitongoji 8,000.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tayari Serikali imejidhatiti kuongeza kasi katika kupeleka kwenye vitongoji. Kuhusiana na umeme Tabora, Tabora kuna vitongoji takribani 3,700. Tumeshapeleka umeme kwenye vitongoji takribani 1,300 na mwaka huu wa fedha tutapeleka umeme kwenye vitongoji takribani 663. Kwa hiyo, niwahakikishie wananchi wa Mkoa wa Tabora Serikali imejipanga kuendeleza miradi ya vitongoji katika mkoa huo, ahsante.
Name
Jesca Jonathani Msambatavangu
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Iringa Mjini
Primary Question
MHE. JACQUELINE K. ANDREA aliuliza: - Je, lini Serikali itamaliza kusambaza umeme kwenye vitongoji nchini?
Supplementary Question 2
MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU: Mheshimiwa Naibu Spika, ni lini Serikali itaanza ule utaratibu wa kusambaza umeme kwenye mitaa 15 kwenye kila jimbo ikiwepo Iringa Mjini, Mtaa wa Mtalagala na Msisina?
Name
Judith Salvio Kapinga
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Answer
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, tayari mkandarasi yuko site na ameshamaliza uhakiki katika mitaa yote 15. Kwa hiyo, sasa hivi yupo katika hatua ya manunuzi. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, mkandarasi yupo site na atamaliza manunuzi hivi karibuni na kazi itaanza, ahsante.
Name
Rashid Abdallah Shangazi
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mlalo
Primary Question
MHE. JACQUELINE K. ANDREA aliuliza: - Je, lini Serikali itamaliza kusambaza umeme kwenye vitongoji nchini?
Supplementary Question 3
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, naipongeza Serikali kwa kupeleka umeme katika vijiji vyote vya Wilaya ya Lushoto, lakini pamoja na jitihada hizo, kupata umeme ni jambo moja, lakini upatikanaji wa umeme ni jambo lingine. Kwa takribani wiki ya tatu sasa Wilaya ya Lushoto iko gizani, hakuna umeme kwa sababu maeneo mengi miti imedondoka na imedondosha nguzo. Je, Serikali ina mkakati gani kuhakikisha kwamba Wilaya ya Lushoto inapata umeme wa uhakika?
Name
Judith Salvio Kapinga
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Answer
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa swali la Mheshimiwa Mbunge. Mheshimiwa Mbunge yuko sahihi kwa takribani mwezi sasa Wilaya ya Lushoto imekuwa ina mvua nyingi pamoja na upepo mkali. Kwa hiyo, inasababisha nguzo kuweza kudondoka. Tayari nimeshafanya kikao na Meneja wa Lushoto na viongozi wa Makao Makuu na tumekubaliana yafuatayo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, tutawapatia Mkoa wa Tanga concrete poles (nguzo za zege) 1,000 na 400 zitaenda eneo la Lushoto, hususan eneo la Mlalo ambapo line hii imeathirika kwa kiasi kikubwa. Nimeshamwelekeza Meneja kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri kuhakikisha hizo concrete poles zinakaa kwenye maeneo ya kawaida. Hata hivyo, kwa kuwa Lushoto kuna milima mikali, nimewaelekeza TANESCO waje na mkakati wa nguzo za chuma ili tuweze kuzipandisha kwenye maeneo ya milima mikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya nimewaagiza waende ili waweze kuwaomba wale wenye mashamba makubwa waturuhusu kupanua njia ya umeme ili tuweze kusafisha na kupunguza athari katika miundombinu yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge na wananchi wa Lushoto, tumelichukua jambo hili kwa uzito mkubwa, na nimewaambia waje na timeline mahususi ya kufanyia kazi mikakati hii kwa ajili ya kupunguza changamoto hii katika Wilaya ya Lushoto, ahsante.
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved