Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Seif Khamis Said Gulamali

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Manonga

Primary Question

MHE. SEIF K. S. GULAMALI aliuliza: - Je, ni lini Kata za Ntobo, Ngulu, Igoweko, Ugaka na Sungwizi ambazo zinaongoza kwa mifugo nchini zitapatiwa fedha za ujenzi wa majosho?

Supplementary Question 1

MHE. SEIF K. S. GULAMALI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi kuweza kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza. Kwa kuwa, Wizara imekuwa ikitoa fedha za ujenzi wa majosho na kuipeleka katika Mfuko wa Halmashauri na kusababisha wakati mwingine majosho haya kutokukamilika, je, kwa nini fedha hizo msiwe mnazipeleka kwenye akaunti za vijiji husika, zinazojenga majosho hayo ili kuhakikisha kwamba, miradi hiyo inakamilika kama ambavyo Serikali inataka, ama ambavyo Wizara nyingine, kama Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, inavyofanya?

Mheshimiwa Spika, swali la pili. Wilaya ya Igunga ni moja ya Wilaya zenye mifugo mingi sana Tanzania. Ni nini mkakati wa Wizara katika kuhakikisha kwamba, inaboresha sekta ya mifugo Wilayani Igunga, hususan Jimbo la Manonga? Ahsante.

Name

Alexander Pastory Mnyeti

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Misungwi

Answer

NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa nafasi hii. Mheshimiwa Mbunge anataka kujua kuna umuhimu gani wa kupeleka fedha kwenye halmashauri badala ya kijijini moja kwa moja?

Mheshimiwa Spika, fedha hizi zinapotoka Wizara ya Mifugo, kwenye Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, kwa maana ya halmashauri, zinakwenda kwa mujibu wa sheria. Miradi inapokwenda kutekelezwa huko, inatekelezwa kwa mujibu wa Sheria ya Manunuzi.

Mheshimiwa Spika, sasa urahisi wa Wizara ya Mifugo kutoa fedha kupeleka TAMISEMI ni kwa sababu ya Sheria ya Manunuzi ambayo inatulazimu kupeleka mahali ambapo mchakato wote wa manunuzi ya umma unaweza ukafanyika. Kule kijijini bado Kamati za Manunuzi hazijakamilika, ndiyo maana fedha inatoka Wizara ya Mifugo inakwenda moja kwa moja halmashauri ambako kamati na michakato yote ya manunuzi inaweza kufanyika kwa kufuata sheria bila uvunjifu wowote wa Sheria ya Fedha.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tutaendelea kupeleka fedha kwenye halmashauri. Kikubwa zaidi ni kwa sababu Waheshimiwa Wabunge ni Wajumbe wa Kamati za Utawala na Fedha kule, ili kuhakikisha kwamba, fedha tunazozipeleka kwenye maeneo hayo zinasimamiwa inavyotakiwa. Kama ni fedha, kwa ajili ya majosho, ziende zikafanye kazi, kwa ajili ya majosho katika maeneo ya halmashauri zetu.

Mheshimiwa Spika, la pili, anataka kujua mkakati wa Wizara ya Mifugo. Mikakati iko mingi na Mheshimiwa Mbunge bahati nzuri ni shahidi. Mkakati mmojawapo wa kuboresha sekta ya mifugo, ni kwamba tumeshagawa madume bora 20 katika Jimbo lake la Igunga.

Mheshimiwa Spika, sasa madume hayo yatafanya kazi ya kuzalisha mbegu bora, baada ya hapo yatakwenda kwenye maeneo mbalimbali na kwenyewe kwenda kuzalisha mbegu bora ya madume.

Mheshimiwa Spika, mikakati iko mingi ikiwa ni pamoja na kuendelea kuboresha miundombinu ambayo ipo kwa ajili ya ufugaji wetu, ahsante.