Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Rashid Abdallah Shangazi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mlalo

Primary Question

MHE. RASHID A. SHANGAZI aliuliza:- Je, fursa zipi zitapatikana kwa Mtanzania mmoja mmoja na vikundi kupitia Fainali za Mpira wa Miguu kwa Nchi za Afrika?

Supplementary Question 1

MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; kwa sababu makundi ya kijamii aliyoyataja mengi bado hayajaunganishwa, kwa mfano eneo la usafirishaji, hapa tunazungumzia madereva wa tax, daladala na hata bodaboda. Je, Serikali ina andaa utaratibu gani ambao utatumika kuyashirikisha makundi haya ya jamii ili kufanikisha mashindano haya ya AFCON kwa kuzingatia diplomasia ya Uchumi?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; mashindano yenyewe haya ni ambayo yanahusisha mchezo wa mpira wa miguu na tunayo changamoto kubwa ya habari za mpira huwa zinapotoshwa potoshwa sana. Je, Serikali iko tayari sasa kuwapa mafunzo maalum na mahsusi Waandishi wa Habari za Michezo kwa ajili ya kuripoti mashindano haya?

Name

Hamis Mohamed Mwinjuma

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Muheza

Answer

NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Rashid Shangazi, mtu wa mpira kweli kweli, kwa ufuatiliaji wake wa mara kwa mara kuhakikisha tunafanya vizuri wakati tukielekea kwenye uandaaji wa mashindano haya ya AFCON 2027 halikadhalika CHAN 2024.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli Serikali iko tayari kukutana na makundi yote ambayo Mheshimiwa Mbunge ameyataja. Na kwa kuonesha kwamba Serikali imedhamiria kweli kufanya hilo Januari 15 mwaka huu tulianza kwa kufanya kongamano na wadau wa michezo kuelekea CHAN 2024 na AFCON 2025 lililofanyika katika Hoteli ya Johari Rotana – Dar es Salaam na tuliongozwa na Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Mashaka Biteko.

Mheshimiwa Naibu Spika, tutaendelea kukutana na makundi mbalimbali na kukaa nayo kuyaelimisha, halikadhalika kuyatengenezea utaratibu ikiwemo utaratibu wa kuyatengenezea utambulisho maalum kama watoa huduma maalum wa mashindano haya ya CHAN 2024 na AFCON 2027. Makundi ninayoyataja yamo pia makundi ambayo Mheshimiwa Mbunge ameyataja, ikiwemo mama lishe na maafisa usafirishaji. Kwa hiyo, itakuwa ni makundi halikadhalika mtu mmoja mmoja.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye swali lake la pili nilishawahi kujibu hapa. Nafikiri nilimjibu yeye Mheshimiwa Shangazi, kuhusiana na wachambuzi na aina ya uchambuzi wa mpira wa miguu ambao unafanyika kwenye nchi yetu. Serikali bado ina dhamira ya dhati kabisa ya kuhakikisha wachambuzi wetu wanapitia kozi japo fupi fupi kabla ya kukaa kwenye vyombo vya habari viwe ni redio ama televisheni.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninajua kwamba ndugu zangu/marafiki zangu wachambuzi hawapendi kulisikia jambo hili, lakini ni ukweli usiopingika kwamba hili linapaswa kufanywa kwa sababu liko kwa mujibu wa Sheria ya Huduma za Habari ya Mwaka 2016, Kifungu cha 19(1), kikishomwa pamoja na Kanuni zake za Mwaka 2017. Kanuni ya 17(2)(a) vinataja kabisa aina ya watu wanaotakiwa kukaa kwenye vyombo vya Habari na vigezo ambavyo wanatakiwa kuwa navyo kabla ya kuruhusiwa kufanya hivyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, hili la kuwatengenezea utaratibu wa kuwapitisha kwenye kozi angalau fupi fupi kabla ya kuwaruhusu kukaa kwenye vyombo vya habari liko palepale. Kwa minajili ya jambo hili, tutawapitisha kwenye Chuo chetu cha Michezo Malya. Ninakushukuru.