Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Fakharia Shomar Khamis

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. FAKHARIA SHOMAR KHAMIS aliuliza: - Je, wananchi watarajie nini baada ya kumalizika kwa Mradi wa TASAF?

Supplementary Question 1

MHE. FAKHARIA SHOMAR KHAMIS: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, kwanza sina budi kuishukuru Serikali kwa maelezo yao mazuri ambayo yanaweza kuwafanikisha wale wote walengwa wa TASAF, lakini nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa baadhi ya walengwa ambao walikuwa kwenye TASAF II na ambao bado hawakufanikiwa kimaisha na wametolewa; je, kwenye hii TASAF III watakuwa na nafasi ya kuingizwa ili waweze kutengeneza maisha yao?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa Serikali ina mpango mzuri katika TASAF III lakini pale pale waangalie baadhi ya washirika wetu wa maendeleo wamebadilisha sera zao za nje za misaada kwa nchi. Ninataka kujua, je, Serikali inalijua hilo na kama inalijua imejipanga vipi ili iweze kufanikisha Mpango wa TASAF III? (Makofi)

Name

Deus Clement Sangu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kwela

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Fakharia kwa namna anavyofuatilia programu ya TASAF. Kuhusu suala la walengwa waliotolewa na bado hali zao ziko duni, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali inalitambua hilo. Kati ya walengwa waliotambuliwa 1,300,916 tayari waliohitimu wapo 400,000 na kati ya hao 400,000 nao tumewafanyia tathmini na kati yao 100,000 walionekana wana hali duni. Serikali haikuwaacha, imewapa mkono wa kwaheri ambao unaitwa Lived Productive Branch ya shilingi 350,000 na kuwapa elimu ya ujasiriamali.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tunaamini katika hao 400,000 ambao wame-graduate bado wana fursa nyingine ya awamu itakayokuja mwaka 2026 mpaka 2030 watapewa kipaumbele kulingana na hali zao zitakavyofanyiwa tathmini.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu programu hii tutakayoanza mwaka 2026 mpaka 2030 awamu hii ya miaka mitano, Serikali inatambua mazingira tunayoenda na dunia. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge tayari tumeshakaa na wadau hawa wanaoweka fedha kwa ajili ya mfuko huu wa TASAF na tayari wadau wapatao 14 wakiongozwa na World Bank wako tayari na hivyo tutakapomaliza programu hii ya awamu ya pili kwa mwezi Septemba, tutakapoanza mwaka 2026 tayari tuna fedha za kuanza na wadau wameonesha commitment. Kwa hiyo, nikuondoe shaka programu hii itatekelezeka na hakuna jambo lolote litakalofanya ikwame, ahsante.