Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Hasna Sudi Katunda Mwilima
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Kigoma Kusini
Primary Question
MHE. HASNA S. K. MWILIMA aliuliza:- Gereza la Ilagala limehodhi eneo kubwa la shamba na kufanya wananchi wa Kata ya Ilagala kukosa maeneo ya kulima. Je, Serikali haioni umuhimu wa kutoa sehemu ya eneo kwa ajili ya wananchi wa Ilagala ili na wao waweze kupata maeneo ya kulima?
Supplementary Question 1
MHE. HASNA S. K. MWILIMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa majibu ya Mheshimiwa Waziri, lakini nitake tu kumhakikishia kuwa eneo hilo la ekari 10,760 na hizo ekari 5,760 ambazo yeye amezitolea majibu kwamba zinatumika kwa ajili ya mifugo na kilimo, nimhakikishie tu kwamba eneo kubwa halijaendelezwa kwa miaka mingi.
Mheshimiwa Naibu Spika, tuna zadi ya ekari 4,500 hazijaendelezwa kwenye kitu chochote. Gereza hawajalima wala hawana mifugo. Wananchi wa vijiji vitatu, kijiji cha Kabeba, Ilagala na Sambala hawana maeneo ya kulima na historia inaonesha walichukua zaidi ya ekari 4,000 bila makubaliano na vijiji hivi vitatu.
Swali langu je, ni kwanini Mheshimiwa Waziri asielekeze gereza litoe angalau ekari 1,500 ili na hawa wananchi wa Jijiji vitatu wapate maeneo ya kulima? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili, kumekuwa na tabia ya baadhi ya Maafisa Magereza kuwakamata wananchi wa vijiji hivi vitatu kuwapiga, kuwanyang‟anya zana zao za kilimo, lakini pia kuwafungulia kesi na kuwapeleka mahakamani. Je, Mheshimiwa Waziri, kama Serikali anatoa tamko gani kwa wananchi wa vijiji hivyo vitatu ambao wamekuwa harassed na Maafisa wa Gereza la Ilagala? (Makofi)
Name
Dr. Mwigulu Lameck Nchemba Madelu
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Iramba Magharibi
Answer
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote nimpongeze sana Mheshimiwa Hasna Mwilima kwa jinsi anavyofuatilia mambo ambayo wananchi wake wamemtuma na kwa kweli yeye ni Mbunge makini, hata juzi nilipita kule wakasema hata uchaguzi ungefanyika leo, angeshinda kwa kiwango kikubwa kuliko kilichopita. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niseme tu kwenye suala hili alilolisemea, ni kweli kuna ekari ambazo hazijaendelezwa, lakini kama nilivyosema kwenye jibu la msingi, zile zilizoachwa ni zile ambazo zimewekwa kwa sababu ziko kwenye chanzo cha maji ambayo yanatumika siyo tu kwa gereza, yanatumika hata kwa wananchi wengine.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa utaratibu wa malengo mapana ya taasisi zetu hizi za magereza ni hasara kuwa na wafungwa wanaolishwa kwa kodi za walipakodi halafu wakawa hawana kazi ya kufanya. Kwa hiyo, hicho tunachosema hata eneo lile lililopo halijatosheleza tunamaanisha malengo marefu ya kuweza kuwatumia wafungwa wanaoweza kufanya kazi ikiwa ni sehemu ya kuwarekebisha ili magereza yetu yaweze kujiendesha.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kuhusu tamko la Serikali kwa wale wananchi ambao wananyang‟anywa vifaa; moja niseme Serikali ya Wilaya ambako ndiko na Jimbo lilipo ni vizuri wakapanga matumizi bora ya ardhi na wanaweza hata wakawasiliana na Wizara ya Ardhi ili kuwatafutia wananchi maeneo mbadala ya kufanya kazi hizo ili wasiingie bila ruhusa katika maeneo ya Magereza na hivyo kusababisha mgongano huu ambao unasababisha wao kukamatwa. Lakini maeneo yote ambayo yana Magereza, tunaendelea kuhimiza mahusiano bora kati ya Taasisi hizo za Serikali pamoja na wananchi wanaozunguka maeneo husika.
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved