Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Sophia Hebron Mwakagenda
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA aliuliza:- Je, lini Serikali itatafuta wawekezaji wa viwanda vidogovidogo vya kuongeza thamani katika zao la ndizi?
Supplementary Question 1
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kuweza kupata nafasi ya kuuliza swali la nyongeza na nina maswali mawili.
Mheshimiwa Naibu Spika, nchi za Caribbean zinaishi kwa kutegemea zao la ndizi katika soko la kimataifa. Hamuoni sasa kuna haja ya Serikali yetu kuhakikisha zao hili linauzwa kimataifa kwa sababu soko bado lipo? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, umezungumzia suala la SIDO kuweza kusaidia wananchi wa ngazi za chini, lakini SIDO imeishia katika Mikoa na Wilayani hazipo. Mheshimiwa Waziri, unaonaje mkashusha fedha na ofisi katika wilaya ili kusaidia wananchi hao waweze kutengeneza hizo crispy na hayo mambo mengine uliyoyaeleza?
Name
Exaud Silaoneka Kigahe
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mufindi Kaskazini
Answer
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru, kwanza nichukue nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Sophia Mwakagenda kwa ufuatiliaji wa kuweka viwanda vya kuchakata mazao ya kilimo kutoka kule Tukuyu, lakini zaidi nachukua mawazo yake na ndiyo kazi ya Serikali tunayofanya kwamba moja; tungependa kama tunavyofanya kwenye mazao mengine kuuza ndizi kwa maana ya mazao ya kilimo kama ilivyo kwenye masoko ya kimataifa na hili linafanyika na tunaendelea kutafuta masoko zaidi kama ambavyo umesema mfano wa nchi za Caribbean wanafanya.
Mheshimiwa Naibu Spika, lengo la Serikali ni hili la pili, ambalo aliuliza swali, tunataka mazao ya kilimo yaongezwe thamani. Mheshimiwa Rais ameshafanya kazi kubwa sana ya kuongeza bajeti kwenye sekta ya kilimo, kwa hiyo, uzalishaji wa mazao ya kilimo umeongezeka. Kwa hiyo, tunadhani tukiweza kuyachakata, moja tutapunguza upotevu wa mazao baada ya mavuno, lakini pili kuongeza thamani kutakuwa na tija kwa wakulima lakini na mnyororo mzima wa thamani wa wafanyabiashara katika sekta ya kilimo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, moja; hili alilolisema ndiyo lengo la Serikali, tunataka SIDO iende kwenye ngazi za halmashauri ili waweze kukaa kule na haya ni maelekezo ya Mheshimiwa Waziri wa Viwanda na Biashara. Niwakumbushe SIDO kutekeleza maagizo hayo ambayo Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Dkt. Selemani Jafo alisema kwamba sasa waanze kufungua ofisi kwenye ngazi ya halmashauri ili wawahudumie kirahisi zaidi wafanyabiashara katika ngazi hiyo na hilo tunaweza kulifanya. Katika mwaka wa fedha unaokuja tunaongeza bajeti kwa ajili ya SIDO waweze kufanya kazi vizuri, ahsante.
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved