Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Soud Mohammed Jumah

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Donge

Primary Question

MHE. SOUD MOHAMMED JUMAH aliuliza:- Je, Serikali ina mikakati gani ya kuvilinda na kuvihifadhi vyanzo vya maji nchini kwa kuzihusisha sekta za misitu, kilimo na mifugo?

Supplementary Question 1

MHE. SOUD MOHAMMED JUMAH: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, pamoja na majibu mazuri ya Serikali nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama unavyojua kwamba takwimu zinatuonesha kuwa nchini kwa mwaka tunapoteza karibu hekta 400,000 za misitu kutokana na uharibifu wa misitu na kwa kuwa uharibifu huu unachangia pia uharibifu wa vyanzo vya maji, je, Serikali ina mkakati gani wa kuzishirikisha taasisi au sekta za misitu, maliasili pamoja na TAMISEMI ili kuwa na mkakati wa pamoja wa kuhifadhi vyanzo vya maji nchini?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali namba mbili, kadiri ninavyofahamu ni kwamba Serikali imeweka fedha nyingi sana katika Bwawa la Mwalimu Nyerere ambalo ni matumaini makubwa sana kwa wananchi wa Tanzania ili kupata umeme ambao ni endelevu. (Makofi)

Je, kwa vile uharibifu wa misitu unachangia utiririkaji wa maji katika Bwawa la Mwalimu Nyerere, tuna mkakati gani wa kuzishirikisha taasisi za Maliasili, wenzetu wa Misitu na TAMISEMI ili kuhakikisha kwamba upatikanaji wa maji unakuwa endelevu na uzalishaji wa umeme katika Bwawa la Mwalimu Nyerere unakuwa endelevu? Ahsante sana

Name

Kundo Andrea Mathew

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bariadi

Answer

NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kama ambavyo Mheshimiwa Mbunge ameuliza na kama nilivyojibu katika jibu la msingi, ni kwamba kwanza kabisa mwaka 2022 Serikali kupitia tamko la Mawaziri wa Kisekta ambapo walikaa pamoja na kukubaliana kuweka mpango ambao utahakikisha kwamba tunakuwa na timu ya kitaifa. Hii timu ya kitaifa, ni kuhakikisha kwamba kunakuwa na ushirikishwaji wa sekta ambazo zinaguswa na huduma ya maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile kuhakikisha kwamba mabwawa na miradi ya kimkakati ambayo inahitaji maji likiwemo Bwawa la Mwalimu Nyerere, basi maji yaweze kuwa endelevu kwa kufanya shughuli na kutengeneza mikakati ambayo itawezesha shughuli hizo ziwezeshe maji kuendelea kuwepo.

Mheshimiwa Naibu Spika, timu hiyo bado iko kazini na inafanya kazi vizuri kabisa, bado hatujapata changamoto yoyote.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika swali lake la pili, Wizara ya Maji iliandaa mpango wa utekelezaji wa utunzaji wa vyanzo vya maji. Mpango huo unahusisha upandaji wa miti rafiki, lakini pia utekelezaji wa shughuli za maendeleo ambazo hazitakuwa na madhara yoyote katika kuathiri vyanzo vyetu vya maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, lengo kubwa rasilimali za maji ni lazima zilindwe ili wananchi waendelee kupata huduma ya maji safi na salama, mamlaka zetu za maji, wakala wetu wa maji, waweze kuwa na vyanzo vya uhakika na endelevu ambavyo havitoingiliwa na shughuli za kibinadamu ambazo zitasababisha vyanzo hivyo kupoteza upatikanaji wa maji. Nakushukuru sana.