Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Aleksia Asia Kamguna
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. ALEKSIA A. KAMGUNA aliuliza:- Je, Serikali ina mpango gani wa kupeleka Watumishi na Vifaa Tiba katika Vituo vya Afya vya Kasanga, Kisemo na Kisaki Morogoro Vijijini?
Supplementary Question 1
MHE. ALEKSIA A. KAMGUNA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi, ninaomba kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza. Swali langu la kwanza; katika hiyo Halmashauri ya Morogoro Vijijini kuna upungufu wa wodi za wanawake na watoto, hazijakamilika. Je, ni lini Serikali itachukua juhudi za makusudi kwenda kupeleka hizo fedha ili wakamilishe hiyo sehemu? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili, katika Kituo cha Afya cha Kisemo hakuna Daktari wa Dawa ya Usingizi, Madaktari wa Operesheni wapo lakini wa dawa ya usingizi hawapo inasikitisha sana. Pia katika Kituo cha Kasanga kuna wahudumu wawili tu wa afya, CO ni mmoja na EN mmoja. Je, ni lini Serikali itachukua juhudi za makusudi, ukifikiria kwamba....
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa nenda kwenye swali, nenda kwenye swali.
MHE. ALEKSIA A. KAMGUNA: Mheshimiwa Naibu Spika, ukizingatia kwamba wanawake na watoto wanakufa kwa kukosa huduma ya upasuaji kutokana na kukosekana kwa dawa ya usingizi? (Makofi)
Name
Zainab Athuman Katimba
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba kwanza nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Aleksia Kamguna kwa kupambania na kupaza sauti kwa ajili ya Sekta hii muhimu ya Afya. Kuhusiana na maswali yake mawili, Serikali imefanya uwekezaji mkubwa katika Sekta ya Afya Msingi na katika kipindi cha miaka minne ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Serikali ya Awamu ya Sita imefanya uwekezaji wa zaidi ya trilioni 1.29 katika kuimarisha hii Sekta ya Afya Msingi.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, kama vile Serikali ilivyoanza kutoa fedha kwa ajili ya kuhakikisha inaboresha miundombinu katika Sekta hii muhimu ya Afya Msingi. Ukizingatia kwamba, 75% ya Watanzania wote wanategemea kupata huduma ya afya kutoka kwenye hivi vituo vya kutolea huduma ya afya msingi, ninaomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, Serikali itaendelea na awamu zijazo kuhakikisha kwamba inafika katika hiki kituo cha afya, kuhakikisha kwamba wodi hii ya wanawake na watoto, wodi muhimu kabisa inajengwa, inakamilishwa na inaanza kutoa huduma.
Mheshimiwa Naibu Spika, vivyo hivyo, kwenye swali lake la pili amezungumzia kuhusiana na mtaalam wa dawa ya usingizi ambayo inasababisha kwamba, kituo kushindwa kutoa huduma muhimu sana ya upasuaji. Ninaomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, Serikali katika huu mwaka wa fedha imetangaza na kibali kimetoka kwa ajili ya kuajiri watumishi wa kada ya afya 9,483. Ninaomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, katika watumishi hawa watakapoajiriwa basi watakuja kupangwa na watafika katika hivi vituo vya afya alivyovitaja ili waweze kutoa huduma bora, iliyodhamiriwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. (Makofi)
Name
Japhet Ngailonga Hasunga (CPA)
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Vwawa
Primary Question
MHE. ALEKSIA A. KAMGUNA aliuliza:- Je, Serikali ina mpango gani wa kupeleka Watumishi na Vifaa Tiba katika Vituo vya Afya vya Kasanga, Kisemo na Kisaki Morogoro Vijijini?
Supplementary Question 2
MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa, Kituo cha Afya cha Hezya na Ndolezi vina upungufu mkubwa sana wa watumishi pamoja na vifaatiba. Je, ni upi mkakati wa Serikali wa kuhakikisha kwamba inapeleka watumishi wa kutosha na vifaatiba? Ahsante sana.
Name
Zainab Athuman Katimba
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa swali lake hili lenye maslahi mapana katika kuimarisha na kuhakikisha Jimboni kwake wananchi wake wanapata huduma bora za afya msingi.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimhakikishie kwamba, dhamira ya Serikali ni kuhakikisha inaendelea kufanya uwekezaji mkubwa kuimarisha hii Sekta ya Afya Msingi. Kwa hiyo Mheshimiwa Mbunge kwa muktadha huo, ninaomba ukae mkao wa kupokea kwa maana Serikali itafika kuja kuimarisha hivi vituo vya afya, pia kuhakikisha inaleta wataalam wa hii kada ya afya ili waweze kutoa huduma iliyo bora. (Makofi)
Name
Samweli Xaday Hhayuma
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Hanang'
Primary Question
MHE. ALEKSIA A. KAMGUNA aliuliza:- Je, Serikali ina mpango gani wa kupeleka Watumishi na Vifaa Tiba katika Vituo vya Afya vya Kasanga, Kisemo na Kisaki Morogoro Vijijini?
Supplementary Question 3
MHE. SAMWELI X. HHAYUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa nafasi. Kituo cha Afya Endasak, tulikipandisha hadhi kutoka zahanati na kina upungufu mkubwa wa vifaatiba na watumishi. Je, kwa watumishi watakaoajiriwa kituo hiki kitapewa kipaumbele?
Name
Zainab Athuman Katimba
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza ninaomba nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Hhayuma Xaday kwa swali lake lenye maslahi mapana ya kuhakikisha anawasemea wananchi wake kwenye hii sekta muhimu ya afya.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, ni dhamira ya Serikali kuhakikisha inaimarisha huduma hii ya afya msingi kwa kuboresha miundombinu, kununua vifaatiba na kuleta wataalam wa kutoa huduma hizi muhimu kabisa za afya. Nimhakikishie, Serikali itaendelea kufanya hivyo na itafika katika Jimbo lake kwa ajili ya kuleta vifaa na vifaatiba pia kuleta watumishi wa hii kada muhimu ya afya. (Makofi)
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved