Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Sylivia Francis Sigula
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. SYLVIA F. SIGULA aliuliza:- Je, lini Serikali itarejesha mikopo ya 10% iliyokuwa ikitolewa kwa Vijana, Wanawake na Watu Wenye Ulemavu?
Supplementary Question 1
MHE. SYLVIA F. SIGULA: Mheshimiwa Naibu Spika, ninashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali, lakini nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; kwa kuwa mikopo hii ya vikundi imekumbwa na changamoto ya wanakikundi kutokuwa na malengo ya Pamoja, lakini tuna vijana wengi ambao wana ujuzi wa biashara, wana elimu nzuri na hawana mitaji. Je, Serikali iko tayari kutoa mikopo hii kwa mtu mmoja mmoja na kuacha sharti la vikundi?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; tunazo Halmashauri 184, kati ya hizo ni halmashauri 64 tu ndiyo zimerejesha hii mikopo tayari zimetoa tangu mwaka jana ambapo dirisha lilifunguliwa, bado halmashauri 120. Je, Serikali inatoa kauli gani kwa hizi halmashauri 120 kuhusu mikopo hii? (Makofi)
Name
Zainab Athuman Katimba
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza ninaomba nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Sylvia Sigula kwa hili swali lake lenye maslahi mapana kwa ajili ya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu ambao pia ni wanufaika wa hii mikopo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na swali lake la kwanza kwamba, mikopo hii iweze kutolewa kwa mtu mmoja mmoja tofauti na utaratibu wa vikundi. Ninaomba nimtaarifu Mheshimiwa Mbunge kwamba, kwa mujibu wa maboresho ya kanuni zinazosimamia utoaji wa hii mikopo ya 10% ya mapato ya ndani. Kikundi kitaomba mkopo na kitakopeshwa kama kikundi, lakini wale wanakikundi wao wenyewe wanaruhusiwa kufanya shughuli zao wao wenyewe kama kuwekeza katika miradi binafsi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo ninaomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, Serikali inatambua kwamba kuna vijana ambao wanataka wafanye shughuli zao au miradi yao wao wenyewe binafsi, ndiyo maana kwenye kanuni kipengele hicho kimetolewa na kwamba mikopo ile ya kikundi itakuwa kama dhamana, lakini kwenye kikundi wao wenyewe wanakikundi wanaweza kuweka utaratibu na kila mwanakikundi akawa na mradi wake yeye mwenyewe unaojitegemea.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na swali lake la pili, ninaomba nitumie nafasi hii kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, kutoa msisitizo kwa Kamati zote zile ambazo zimeundwa za usimamizi wa mikopo hii ya 10% ya mapato ya ndani, waweze kutimiza wajibu wao kwa mujibu wa kanuni. Kwa sababu, kwa mujibu wa utaratibu na kanuni inatoa mwongozo ndani ya miezi miwili tangu kikundi kimeomba mkopo, ni lazima wawe wamekamilisha taratibu zote za ndani na kile kikundi kimeweza kupatiwa mikopo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo nitoe msisitizo, viongozi wetu wote waliopo katika ngazi za mikoa, ngazi ya halmashauri na mpaka katika ngazi ya kata. Kwa sababu kuna Kamati ya kutoa huduma ya mikopo hii kuanzia katika ngazi ya kata, halmashauri kuja mpaka katika ngazi ya wilaya, ngazi ya mkoa, waweze kusimamia wajibu wao ili hizi fedha nyingi ambazo Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan amedhamiria, ziweze kwenda kunufaisha makundi haya maalum, ziweze kufanya hivyo na wananchi waweze kupata mitaji kwa ajili ya shughuli zao za kiuchumi. (Makofi)
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved